Simba, ASEC kazi imeisha

SIMBA inacheza mechi yake ya kwanza ya makundi ya Shirikisho Jumapili ijayo dhidi ya Asec ya Ivory Coast Jijini Dar es Salaam.
Simba imesisitiza kwamba wameshamaliza mambo mengi ya ndani ya nje ya Uwanja kwenye mchezo huo na kwa asilimia kubwa wanategemea kuanza kwa kishindo.
Mulamu Ng’ambi ambaye ni mmoja wa Wajumbe wa Bodi ya Simba, ameliambia Mwanaspoti kwamba wao kama viongozi wameshafanya yanayowahusu kuhusu wachezaji na mipango mingine ya nje ya uwanja.
Lakini ndani ya uwanja, Kocha Msaidizi, Selemani Matola alisema baada ya mechi ya Mbeya Kwanza kuna vitu wameviona vya kiufundi na wanavifanyia kazi.
Matola alisema miongoni mwa mambo hayo hasa ni mastraika kupoteza nafasi nyingi za kufunga jambo ambalo limekuwa na shida muda mrefu lakini kama Benchi la Ufundi hawatachoka kulifanyia kazi katika mazoezi.
Alisema mastraika wao wanapitia wakati mgumu kipindi hiki na kwamba hatua hiyo inaweza kumtokea mchezaji yoyote kwenye maisha ya soka hivyo wanalifanyia kazi ili kuwa na mabadiliko na kufanya vizuri mchezo wao na Asec Mimosas.
“Benchi la Ufundi tutakuwa tumewafuatilia na tunazo taarifa za kutosha dhidi ya wapinzani wetu kuna mambo ya kiufundi tunayo na tunaendelea kuyafanyia kazi kabla ya kukutana nao,” alisema Matola na kuongeza;
“Lazima tuwaangalie katika maeneo mbalimbali vile ambavyo wanashambulia wapo imara maeneo gani wanashida wapi kisha nasi tutakuwa na silaha zetu za kwenda kukabiliana nao ili tufanye vizuri,”alisema.
“Watakuwa na maeneo yenye wachezaji wazuri, kulingana na malengo tuliyojiwekea katika mashindano haya tunakwenda kupambana na kuanza vizuri mchezo wa nyumbani kwa kupata ushindi.
“Mazoezi tutaendelea nayo wakati huu ni kulingana na mahitaji ya mechi yalivyo na yale ya kiufundi tutakayokwenda kuyatumia kama silaha zetu kwenye mchezo huo.”
Matola alisema malengo ya Simba ni kufanya vizuri kwenye mashindano hayo na mara zote wanatakiwa kuwa na mwanzo mzuri na faida nyingine ya kucheza uwanja wa nyumbani.
Kwenye Ligi Kuu ya Ivory Coast iliyopo mzunguko wa nane, Asec Mimosa ndio vinara katika msimamo wakiongoza kwa pointi 21 huku wakiwa wamecheza mechi saba, wameshinda zote hawajatoka sare wala kufungwa.
Mimosa kwenye ligi wamefunga mabao 13 na kufungwa matatu, kutokana na data hizo inaonyesha timu hiyo ni nzuri kushambulia ndio maana wamefunga idadi hiyo ya mabao lakini wana wastani wa kufunga mabao mawili kila mchezo mmoja na wana safu ngumu ya ulinzi ndio maana wamefungwa mabao matatu.
Kwenye kikosi chao kuna wachezaji wa safu tofauti ambao Simba wanatakiwa kuwachunga kutokana na uwezo wao tofauti ambao ni Konate, Diakite, Singone, Serge Pokou na Aubin Kramo.
Simba imepania kufanya vizuri kwenye mashindano hayo na kutinga hatua ya nusu fainali na zaidi msimu huu ambao ndiyo wa kwanza wanashiriki kwani walizoea Ligi ya Mabingwa.