Nyoni atoa neno kwa chipukizi

What you need to know:

Kiungo wa Simba, Erasto Nyoni ametoa elimu kwa chipukizi waliopo kwenye ligi kujua fursa zilizopo kwenye soka ambazo zinaweza kuwatoa kimaisha.

KIUNGO wa Simba, Erasto Nyoni amesema endapo kama chipukizi waliopo Ligi Kuu Bara, watavitendea haki vipaji vyao anaamini maisha yao yatabadilika kiuchumi.

Amefafanua kauli yake kwamba soka kwa sasa ni biashara inayolipa duniani, hivyo ni rahisi kufanikiwa kwa wachezaji wanaojitambua na kujituma.

Amesema kuna vipaji vikubwa kwenye ligi isipokuwa anaona wachezaji hawajitumi kuonyesha madini yaliopo miguuni kwao.
"Soka ukiliheshimu linakuheshimu, mfano mzuri waangalie kijana mwenzao Mbwana Samatta ambaye anacheza Ulaya kwa sasa, alijituma na kuheshimu kazi yake,"

Ameongeza kuwa "Kazi yoyote ili iwe bora ni lazima mtu afanye kwa bidii ndivyo inavyotakiwa kufanyika kwa wachezaji kama wamechagua soka kuwa kazi basi waiheshimu na kuzingatia miiko yake,"amesema.

Mbali na kuwataka wajitume, pia amewashauri kuitumia vyema mitandao ya kijamii anayoamini itawarahisishia wao kupata timu nje ya nchi.

"Kwanza kazi zao zikiwa nzuri moja kwa moja zinaonekana kwenye mitandao ya kijamii, pia badala ya kutafuta marafiki wasio na faida wanaweza wakawa wanajenga ukaribu na watu wa soka kutoka nchi mbalimbali,"amesema.