Ntibazonkiza atua, awapa Yanga imani

Ntibazonkiza atua, awapa Yanga imani

Dar es Salaam. Mshambuliaji mpya wa Yanga raia wa Burundi, Said Ntibazonkiza amesema ameifuatilia Ligi Kuu Tanzania Bara na timu yake kwa ujumla tangu akiwa kwao na yupo tayari kwa mapambano.

Ntibazonkiza alisajiliwa na Yanga siku chache baada ya kuja Tanzania kucheza na Taifa Stars akiwa na kikosi cha Intamba Murugamba katika mchezo wa kimataifa wa kirafiki, ambao alifunga bao pekee.

Akizungumza baada ya kuwasili Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, juzi usiku, mshambuliaji huyo wa zamani wa SM Caen ya Ufaransa alisema hana shaka na Ligi Kuu kwani amekuwa akiitazama na kujifunza mengi akiwa Burundi.

Alisema anafurahi kuja nchini kuanza kazi ya kukitumikia kikosi cha mabingwa hao wa zamani na furaha yake itakuwa kuiona Yanga inaendelea kubaki juu hadi mwisho wa msimu kwa ajili ya ubingwa.

“Kawaida huwa sipendi kuwa muongeaji sana kazi yangu ndio itazungumza uwanjani,nipo tayari sasa kuanza kazi hapa Yanga hii ni klabu kubwa sio hapa Tanzania tu nimejipanga kiushindani ili niweze kuonyesha nafai yangu hapa,”alisema Ntibazonkiza.

“Nimekuwa naangalia kweli mechi za timu mbalimbali wakati nikiwa nyumbani naona ni timu bora ambayo inastahili kuwa juu ya msimamo,hatua hii ya kuongoza ligi ni kitu kikubwa nafasi yangu sasa ni kutumia uzoefu wangu kuongeza kitu nikishirikiana na wenzangu katika kuipa mafanikio timu yangu mpya,” alisema mshambuliaji huyo.

 BY Khatimu Naheka