Nabi: Nilimaliza mechi mapema, ijayo fasta tu

MAPEMA tu. Ndio mpango aliouweka Kocha wa Yanga, Nabi Nasreddine kwa ajili yao mechi yao iliyopita dhidi ya Simba na baada ya jambo hilo kufanikiwa, amesema ameandaa fomesheni hilo tofauti kabisa kwa ajili mechi ijayo kule Kigoma.

Katika mechi iliyopita ya mzunguko wa pili wa Ligi Kuu Bara kwenye Uwanja wa Benjamini Mkapa, Yanga walifunga bao la mapema katika dakika ya 11 kupitia kwa Zawadi Mauya na wakalilinda hadi dakika 90 zilipomalizika.

Lakini kwa ajili ya mechi ijayo, Nabi ana mikakati tofauti ambayo tayari wameanza kuifanyia kazi.

Simba na Yanga zitakutana mara mbili zaidi msimu huu, ya kwanza ikiwa ni mechi ya fainali ya Kombe la Shirikisho (ASFC) itakayopigwa Julai 25 kule Kigoma na kisha zitavaana tena katika mechi ya ufunguzi wa msimu ujao wa Ligi Kuu Bara.

Simba waliingia uwanjani Jumamosi iliyopita wakiamini watashinda mechi hiyo na kutangazwa ubingwa mbele ya Yanga, lakini walishindwa kuifikia historia iliyodumu kwa miaka 36 sasa ya Yanga kutwaa ubingwa mbele ya mahasimu wao baada ya Simba kutia mpira kwapani baada ya kucheza mechi kwa dakika nne tu na kuvunja mechi, na hivyo Yanga kupewa pointi mbili (wakati huo mshindi wa mechi alikuwa akipata pointi mbili kabla ya kanuni kubadilishwa na kuwa pointi tatu za sasa) na mabao mawili na Wanajangwani kutangazwa mabingwa wa Ligi Kuu Bara mwaka 1985.

Simba yenye pointu 73 ilihitaji kuifunga Yanga iliyokuwa na pointi 67 ili kutwaa ubingwa, lakini Mauya alimwagia mchanga pilau la sherehe.

Akizungumza na Mwanaspoti, Nabi alisema kabla ya mchezo huo walitumia muda kuangalia mechi za wapinzani wao za mashindano ya ndani na kimataifa ikiwemo mechi dhidi ya Al Merreikh wakati anaifundisha.

Alisema mechi ya kwanza aliangalia dhidi ya Merreikh wakati huo alikuwa anaifundisha licha ya kumalizika kwa suluhu walicheza vizuri na wachezaji wake walitengeneza nafasi za kufunga ila walishindwa kuzitumia.

“Mbinu ambazo nilizitumia katika mechi ile nilizirudisha katika mechi ya juzi na niliwapatia wachezaji wangu katika mazoezi na nashukuru kwa kiasi kikubwa tulifanikiwa licha ya kufunga bao lakini tulikosa nafasi nyingine kama ile ya Yacouba Sogne,” alisema Nabi na kuongeza;

“Baada ya hapo jambo jingine watu hawafahamu, sijawahi kuongea au kuwasiliana na kocha wa Simba (Didier Gomes), lakini ni mtu ambaye namfahamu hata aina yake ya ufundishaji soka.”

Alisema kwenye kuwafuatilia Simba alibaini wana wachezaji wengi wenye uwezo binafsi kutofautisha na Yanga na pia kocha wao ni mtu mwenye mbinu nyingi na hubadilika mara kwa mara kulingana na mechi ilivyo.

Ali-sema baada ya kuliona hilo aliwaeleza wachezaji wake wanatakiwa kuwa makini na ubora wa wachezaji wa Simba kwani upo juu na wanatakiwa kutowapa nafasi.

Alisema ilikuwa lazima akubali ubora wa wachezaji wa Simba na amewaheshimu katika hilo na kuweka mbinu sahihi za kutowaruhusu kufanya hatari nyingi langoni mwao, ambazo zingeweza kuwapa wapinzani nafasi za kufunga.

“Niliwaambia wachezaji wangu wanachotakiwa kufanya ni kutumia nguvu zaidi kila wanapokwenda kuutafuta mpira kwani wachezaji wa Simba hawapendi kucheza aina ya timu ambayo inatumia nguvu zaidi.

“Kama uliona vizuri tulipokuwa hatuna mpira tulitumia nguvu kuutafuta, hii haikuwa rafiki kwao na hapo tuliwaweza.

“Baada ya hapo niliwaambia hatutakiwi kuacha mianya ambayo wangepata nafasi ya kupiga pasi kwa urahisi kwani moja ya silaha yao ni hiyo hivyo wakati mwingine wangu walitakiwa kuwa nyuma ya mpira idadi isiyopungua nane.

“Kama uliona kuna wakati mbele alikuwepo Yacouba peke yake tulipokuwa hatuna mpira, ile iliwanyima Simba nafasi ya kucheza kwa kujinafasi,” alisema Nabi.


TSHABALALA / KAPOMBE

Nabi alisema kwa alivyowafuatilia Simba, amebaini kuwa wanatumia sana mabeki wao wa pembeni kushambulia.

Alisema Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ na Shomary Kapombe huwa wanaanzisha mashambulizi ya mara kwa mara kwa kupiga krosi na pasi kwa washambuliaji, jambo ambalo aliliwekea mkakati maalum na anafuraha kwamba walifanikiwa.