KMC yaanza kuiwinda Namungo

Muktasari:

  • TIMU ya KMC leo imeanza maandalizi kwa ajili ya mchezo wao ujao wa Ligi Kuu dhidi ya Namungo utakaochezwa Oktoba 1 katika uwanja wa Majaliwa Ruangwa, Lindi.

TIMU ya KMC leo imeanza maandalizi kwa ajili ya mchezo wao ujao wa Ligi Kuu dhidi ya Namungo utakaochezwa Oktoba 1 katika uwanja wa Majaliwa Ruangwa, Lindi.

KMC inayonolewa na kocha Mkuu, Thiery Hitimana imeanza kujifua baada ya kurejea kambini jana jioni baada ya kumaliza mapumziko ya siku mbili tangu ilipocheza na Ihefu Septemba 20 katika uwanja wa Uhuru, KMC ikishinda 2-1.

KMC inajiandaa na mchezo wao dhidi ya Namungo badala ya Mtibwa Sugar ambao ulipangwa kuchezwa Septemba 27 lakini kutokana na wachezaji kuwa kwenye majukumu ya timu ya Taifa mechi hiyo ilibadilishwa.

Ofisa Habari wa KMC, Christina Mwagala amesema mabadiliko ya mchezo wao na Mtibwa Sugar wameyapokea na kuyafanyia kazi.
“Tulipokea taarifa ya mabadiliko ya mchezo wetu dhidi ya Mtibwa Sugar ambao awali ilikuwa tucheze siku ya Jumanne ya Septemba 27 kwenye uwanja wetu wa Uhuru, kwasasa tunajiandaa kwa mchezo mwingine ambao tutakuwa ugenini dhidi ya Namungo, tunajipanga vizuri kutafuta alama tatu muhimu ugenini." amesema Mwagala na kuongeza.

“Wachezaji wote wamesharejea kambini baada ya kumaliza mapumziko ya siku mbili ambayo tulitoa siku tuliyocheza mechi na Ihefu,  wote wapo salama wakiwa na nguvu, Afya njema, hali na morali kwa ajili ya kuhakikisha kwamba tunafanya maandalizi bora ambayo yatatupa matokeo chanya kwenye  mchezo huo licha ya kwamba tunafahamu fika hautakuwa mwepesi."

KMC FC imecheza mechi nne na kati ya hizo tatu ikiwa ugenini huku mmoja ikiwa kwenye uwanja wa nyumbani, ikiibuka na ushindi katika mchezo mmoja dhidi ya Ihefu na kutoa sare michezo miwili ambayo ni dhidi ya Simba pamoja na Polisi Tanzania huku ikipoteza dhidi ya Coastal Union.

Katika msimamo wa Ligi Kuu, KMC ipo kwenye nafasi ya nane ikiwa na jumla ya pointi tano, mabao ya kufunga sita na ya kufungwa sita.