Wawakilishi CAF kazi ndiyo kwanza imeanza
Muktasari:
- Katika mechi hizo za marudiano za raundi ya awali, Yanga SC iliendelea kuonyesha ubora wake Afrika baada ya kuishinda 2-0 dhidi ya Wiliete ya Angola, ushindi ulioipa tiketi ya kufuzu kwa raundi ya pili kwa jumla ya mabao 5-0 na awali ilishinda mabao 3-0 ugenini.
WIKIENDI iliyopita mashabiki wa soka Tanzania Bara na Zanzibar walishuhudia hatua muhimu kwa klabu zao katika mashindano ya kimataifa ya CAF.
Klabu sita kutoka Bara na Zanzibar zililiwakilisha taifa katika mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika na Kombe la Shirikisho. Yanga SC, Simba SC, Mlandege SC (Ligi ya Mabingwa Afrika) pamoja na Azam FC, Singida Black Stars, na KMKM SC (Kombe la Shirikisho Afrika).
Katika mechi hizo za marudiano za raundi ya awali, Yanga SC iliendelea kuonyesha ubora wake Afrika baada ya kuishinda 2-0 dhidi ya Wiliete ya Angola, ushindi ulioipa tiketi ya kufuzu kwa raundi ya pili kwa jumla ya mabao 5-0 na awali ilishinda mabao 3-0 ugenini.
Msimu wa 2022/23, ilifika fainali ya Kombe la Shirikisho na kuwa timu ya kwanza kutoka Tanzania kufika hatua hiyo.
Simba ambayo jana ilikuwa uwanjani dhidi ya Gaborone United ya Botswana, iliingia kwenye mchezo huo ikiwa na faida ya ushindi wa bao 1-0 ilioupata ugenini. Simba wamekuwa wakishiriki Ligi ya Mabingwa Afrika mara kwa mara katika miaka ya karibuni na ilifika robo fainali msimu wa 2022/23, rekodi inayowafanya kuwa miongoni mwa klabu bora za Afrika.
Azam FC pia jana ilikuwa ikikipiga dhidi ya Al Merreikh Bentiu ya Sudan Kusini, huku ikiwa na faida ya ushindi wa 2-0 ilioupata ugenini. Azam nao wana historia ya kucheza hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho mwaka 2015 na kwa sasa wanaonekana kurudi kwenye ubora wao.
Kwa jumla, hadi sasa timu tano kati ya sita zipo kwenye nafasi nzuri ya kuingia raundi ya pili ya mashindano haya, ikiwa ni mafanikio makubwa kwa Tanzania. Idadi hii ni ongezeko kutoka misimu iliyopita na mara nyingi timu moja au mbili pekee ndizo zilikuwa zinasonga mbele.
Mlandege SC licha ya ushindi wa 3-2 nyumbani dhidi ya Insurance ya Ethiopia, ilijikuta ikitolewa kwa jumla ya mabao 4-3, kutokana na kichapo cha 2-0 ilichokipata katika mchezo wa mkondo wa kwanza.
Hii inaonyesha umuhimu wa maandalizi bora hata kwa michezo ya ugenini, kwani matokeo ya kwanza yanaathiri safari ya timu kwa kiasi kikubwa.
Singida timu iliyoanza kushiriki mashindano haya kwa mara ya kwanza, ilijihakikishia tiketi ya kusonga mbele baada ya kuiondosha JKU ya Zanzibar kwa ushindi wa jumla wa 4-1. Pia, KMKM kutoka Zanzibar ilisonga mbele baada ya kuishinda Horseed ya Somalia. Mafanikio haya yanaashiria mabadiliko chanya katika soka la Zanzibar.
Mwanaspoti linaamini timu hizi zinaweza kufika mbali zaidi kama zitakuwa na maandalizi bora. Ni wazi usajili zilizofanya kwa ajili ya msimu huu wa ligi za Bara na Zanzibar utazibeba na kila timu imejiwekea malengo ya kufanya vyema.
Kazi bado ndiyo kwanza imeanza na baadhi ya timu zimeshafahamu zitakutana na nani raundi inayofuata, hivyo, maandalizi ya mapema yanatakiwa ikiwamo vikosi kuwa na usimamizi mzuri wa makocha na klabu kuwa na utulivu.
Tunatamani kuona timu nyingi zikiwa hatua ya makundi kwani zilishazoeleka mbili tu za Simba na Yanga.
Pia zikumbuke huko mbele ndiyo kugumu zaidi kwani zinaenda kukutana na timu vigogo Afrika na hakuna timu ya Tanzania iliyofika nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika na mipango inahitajika ikiwamo kutumia vyema madirisha ya usajili na kuwekeza zaidi ili kufikia malengo.