Yanga, Azam ni zaidi ya mechi Muungano
Muktasari:
Yanga ndiyo ilitangulia kuingia nusu fainali kwa kuibuka na ushindi wa mabao 4-0 dhidi ya Muembe Makumbi na kisha Azam ikafuata kwa kupata ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya KVZ.
FURAHA kubwa hapa kijiweni ni ratiba ya Yanga na Azam FC kukutana katika hatua ya nusu fainali ya Kombe la Muungano itakayopigwa visiwani Zanzibar.
Yanga ndiyo ilitangulia kuingia nusu fainali kwa kuibuka na ushindi wa mabao 4-0 dhidi ya Muembe Makumbi na kisha Azam ikafuata kwa kupata ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya KVZ.
Hii nusu fainali ya Yanga na Azam FC kwenye Kombe la Muungano ni mechi ambayo bila shaka itakuwa na mvuto sana na ni kama fainali ambayo imetangulia nadhani hapa watu wa mpira wameshanielewa.
Kwanza ni fursa ya Yanga kuendeleza ubabe au Azam FC kulipa kisasi msimu huu kwa vile ni mchezo wa tatu kuzikutanisha timu hizo msimu huu katika mashindano tofauti huku Yanga ikiwa mbabe kwa kushinda mechi moja.
Zilikutana katika Kombe la Mapinduzi mwanzoni mwa mwaka huu na Yanga ikaibuka na ushindi kwa mikwaju ya penalti na baadaye zikaumana katika Ligi Kuu na mechi ilimalizika kwa sare ya bila kufungana.
Ikumbukwe mechi hii ya Kombe la Muungano haitokuwa na matokeo ya sare. Muda wa kawaida ukimalizika na timu hizo zikiwa na matokeo ya sare, mikwaju ya penalti itatumika kusaka mshindi.
Kwa upande mwingine kiu ya kutwaa taji kwa kila timu ni jambo ambalo litafanya mechi ya leo iwe na mvuto na ushindani wa hali ya juu kwa timu hizo mbili ambazo ni miongoni mwa wakubwa wa soka la Tanzania.
Tayari Yanga ina kombe moja mkononi ambalo ni la Mapinduzi huku ikiwa katika nafasi nzuri ya kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Bara ikiipita Azam FC iliyo katika nafasi ya tatu kwenye msimamo wa ligi kwa pointi 10.
Hii ni bonge moja la mechi. Huku kuna Florent Ibenge na kule kuna Pedro Gonvalves. Mtoto hatumwi dukani hapo.