Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Vita ya makocha Championship

Muktasari:

  • Nsajigwa ‘Fuso’ amejiunga na kikosi hicho akiwa ndiye kocha mkuu baada ya Emmanuel Mwijarubi aliyeifundisha kwa msimu wa 2024-2025 kuondoka, huku uongozi ukionyesha matumaini makubwa kwake kutokana na uzoefu mkubwa katika soka la Tanzania.

WAKATI Ligi ya Championship imeanza jana, wapo makocha wakubwa na wazoefu kutokana na wasifu walionao (CV), wamebeba matumaini makubwa ya ubingwa au kuzipandisha Ligi Kuu timu wanazozifundisha, kama ambavyo Mwanaspoti linawaelezea.


SHADRACK NSAJIGWA

(TRANSIT CAMP)

Nyota huyo wa zamani wa Yanga na timu ya taifa ya Taifa Stars, amejiunga na timu hiyo inayoshiriki Ligi ya Championship kwa mkataba wa mwaka mmoja, baada ya kuachana na Namungo, aliyoifundisha akiwa kocha msaidizi chini ya Juma Mgunda.

Nsajigwa ‘Fuso’ amejiunga na kikosi hicho akiwa ndiye kocha mkuu baada ya Emmanuel Mwijarubi aliyeifundisha kwa msimu wa 2024-2025 kuondoka, huku uongozi ukionyesha matumaini makubwa kwake kutokana na uzoefu mkubwa katika soka la Tanzania.

Kocha huyo ana kazi kubwa ya kukipambania kikosi hicho kurejea Ligi Kuu baada ya kushuka mwaka 2006, kilipomaliza mkiani kwa pointi 20, kikishinda mechi tano, sare tano na kupoteza 20, kikifunga mabao 21 na kuruhusu nyavu zake kutikiswa mara 48.


HABIBU KONDO

(TMA)

Kondo amejiunga na timu hiyo inayoshiriki Ligi ya Championship akishirikiana na kocha msaidizi, Augustino Thomas, ambaye alikuwa na kikosi hicho tangu msimu wa 2024-2025, akifanya kazi na Maka Mwalwisi na baadaye pia, Mohamed Ismail ‘Laizer’.

Kocha huyo wa zamani wa Azam, Coastal Union, Majimaji, Mbeya Kwanza na timu ya taifa ya vijana chini ya miaka 18 (U-18) kwa nyakati tofauti, ni miongoni mwa makocha wazoefu waliobeba matumaini ya kikosi hicho cha Arusha.

Msimu uliopita timu hiyo ilimaliza katika nafasi ya tano kwa pointi 53, baada ya kushinda mechi 15, sare nane na kupoteza saba, ikifunga mabao 40 na kuruhusu 29, huku kocha huyo akiwa na kibarua kigumu cha kuipambania icheze Ligi Kuu Bara.

Timu hiyo itaanza Ligi ya Championship msimu huu kwa kucheza mechi mbili mfululizo kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha, kwa kuanza kwa kupambana na Bigman, Oktoba 12, 2025, kisha kuikaribisha Mbeya Kwanza, Oktoba 17, 2025.


ZUBERY KATWILA

(GEITA GOLD)

Katwila amejiunga na Geita Gold kwa mkataba wa mwaka mmoja baada ya kuachana na Bigman, aliyoiongoza kwa msimu uliopita, kufuatia kocha huyo dili lake la kujiunga na Coastal Union ya jijini Tanga iliyomuhitaji mwanzoni mwa msimu huu kukwama.

Kocha huyo mzoefu aliyetamba na timu mbalimbali zikiwamo, Ihefu (ambayo kwa sasa ni Singida Black Stars) na Mtibwa Sugar, alijiunga na Bigman akichukua nafasi ya Fredy Felix ‘Minziro’, aliyejiunga na Pamba ambayo kwa sasa ameachana nayo pia.

Kwa msimu wa 2024-2025, Katwila aliiwezesha Bigman kumaliza ikiwa nafasi ya nane katika Championship kwa pointi 47, baada ya kushinda mechi 12, sare 11 na kupoteza saba, ikifunga mabao 29 na kuruhusu nyavu zake kutikiswa mara 21.

Geita iliyoshuka daraja msimu wa 2023-2024, msimu wa 2024-2025, wa Championship ilimaliza ikiwa nafasi ya nne kwa pointi 56 chini ya aliyekuwa kocha mkuu, Mohamed Muya na kushindwa kurejea Ligi Kuu Bara, baada ya kufeli mechi za ‘play-off’.

Timu hiyo ilicheza ‘play-offs’ za kupanda Ligi Kuu Bara dhidi ya Stand United ‘Chama la Wana’ iliyomaliza nafasi ya tatu kwa pointi 61 na kushuhudia ikiondoshwa kwa jumla ya mabao 4-2, baada ya sare nyumbani ya 2-2 kisha kuchapwa ugenini 2-0.


MBWANA MAKATA

(POLISI TZ)

Mabosi wa Polisi Tanzania wamempa mkataba wa miaka miwili, Mbwana Makata, baada ya kocha huyo kutokuwa na timu yoyote tangu mara ya mwisho alipoachana na Tanzania Prisons Desemba 28, 2024, kutokana na mwenendo mbaya katika Ligi Kuu Bara.

Makata aliyewahi kuifundisha Polisi Tanzania, alitambulishwa Julai 9, 2025, jijini Dodoma na mwenyekiti wa kikosi hicho, Kamishna wa Polisi Jamii, CP Faustine Shilogile, huku lengo kubwa ni kuhakikisha timu hiyo inarejea tena Ligi Kuu Bara.

Kabla ya kutua Polisi, Makata aliiongoza Prisons katika mechi 14 za Ligi Kuu Bara, ambapo kati yake alishinda mbili tu, sare tano na kupoteza saba, kisha kuondoka na nafasi yake kuchukuliwa na aliyekuwa kocha wa Geita Gold, Amani Josiah.

Makata amejiunga na Polisi akimrithi aliyekuwa kocha wa timu hiyo, Mussa Rashid aliyeiongoza msimu wa 2024-2025 katika Championship, kumaliza nafasi ya 10 na pointi 33, baada ya kushinda mechi nane, sare tisa na kupoteza 13 kati ya 30.

Hata hivyo, Makata ana rekodi tamu na timu hiyo, kwani ndiye aliyeipandisha Ligi Kuu Bara msimu wa 2019-2020, ambapo kwa sasa anakipambania tena kikosi hicho kukirejesha katika ufalme iliojiwekea, baada ya kushuka daraja msimu wa 2022-2023.

Msimu huo wa 2022-2023, Polisi ilimaliza Ligi Kuu Bara ikishika nafasi ya 15 kwa pointi 25, ikishinda mechi sita tu, sare saba na kupoteza 17, ikifunga mabao 25 na kuruhusu 54, ikiungana na Ruvu Shooting na Mbeya City ambayo tayari imerejea.


MAKA MWALWISI

(MBEYA KWANZA)

Kocha huyo wa zamani wa Ihefu kwa sasa Singida Black Stars, licha ya uzoefu mkubwa alionao wa kufundisha timu mbalimbali ikiwamo TMA ya Arusha, ila ana kazi ya kuipigania Mbeya Kwanza irejee tena Ligi Kuu baada ya kushuka msimu wa 2021-2022.

Timu hiyo ilianzishwa rasmi mwaka 2012, ikiitwa Coca Cola Kwanza, ikiwa ni timu ya wafanyakazi wa Coca Cola, japo mwaka 2014, kikosi hicho kilibadilishwa jina tena na kuitwa Mbeya Warriors ambapo kilishiriki Ligi ya Mabingwa wa Mkoa (RCL).

Hata hivyo, mwaka 2015, timu hiyo ikiwa Ligi Daraja la Pili (SDL), ilibadilishwa tena jina kutoka Mbeya Warriors, hadi Mbeya Kwanza..

Timu hiyo iliyomaliza nafasi ya saba na pointi 50 msimu wa 2024-2025, wa Ligi ya Championship, itaanza kufungua pazia la msimu huu wa 2025-2026, kwa kupambana na kikosi cha Mbuni, Oktoba 10, kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha.


JUMA KASEJA

(KAGERA SUGAR)

Kipa huyo aliyeitumikia Kagera akiwa mchezaji na kocha wa makipa, alijiunga na timu hiyo Machi 4, 2025, akichukua nafasi ya Mmarekani Melis Medo aliyeondoka Februari 25, 2025, baada ya kutoridhishwa na mwenendo wa matokeo ya kikosi hicho.

Kagera iliyodumu katika Ligi Kuu Bara kwa miaka 20 tangu ilipoanza kushiriki 2005, ilishuka daraja msimu wa 2024-2025, baada ya kushinda mechi tano tu, sare minane na kupoteza 17, ikishika nafasi ya 15, kufuatia kukusanya pointi zake 23.

Kaseja aliyewahi kuichezea timu ya Taifa Stars na klabu za Simba na Yanga, ni kocha mwingine mzoefu wa soka la Tanzania, ambaye anaangaliwa kwa jicho la tatu kile atakachokifanya kwa kikosi hicho, hasa kukirejesha tena katika Ligi Kuu Bara.

Kagera itaanza kufungua pazia la Ligi ya Championship msimu wa 2025-2026 kwa mechi zote mbili nyumbani kwenye Uwanja wa Kaitaba kwa kupambana na maafande wa Transit Camp Oktoba 10, kisha kuikaribisha, Barberian zamani Kiluvya United Oktoba 18.


FRED MINZIRO

(BIGMAN FC)

Fred Felix ‘Minziro’, amerejea tena katika kikosi hicho, baada ya kukifundisha mwanzoni mwa msimu wa 2024-2025, ingawa aliondoka Oktoba 17, 2024 na kujiunga na Pamba Jiji, akichukua nafasi ya Mserbia Goran Kopunovic aliyeondoka Oktoba 16, 2024.

Miongoni mwa rekodi bora kwa kocha huyo, ni kupandisha timu tatu Ligi Kuu Bara kutokea Championship, akianza na Singida United msimu wa 2017-2018, akaipandisha KMC msimu wa 2018-2019, kisha akaendelea tena kwa Geita Gold msimu wa 2021-2022. 


IDD NASSOR CHECHE

(STAND UNITED)

Klabu ya Stand United imefikia makubaliano ya kumuajiri aliyekuwa kocha wa Azam, Idd Nassor ‘Cheche’, baada ya timu hiyo ya ‘Chama la Wana’ kwa msimu wa 2024-2025, kufundishwa na Juma Masoud aliyeisaidia kumaliza nafasi ya tatu na pointi 61.

Pia, Masoud aliiwezesha kucheza mechi za ‘Play-Off’, kusaka tiketi ya kucheza Ligi Kuu Bara, ambapo aliiondoa Geita Gold iliyomaliza ya nne na pointi 56, kwa jumla ya mabao 4-2, kisha kukutana na Fountain Gate na kuondoshwa kwa jumla ya 5-1.

Cheche mwenye uzoefu mkubwa na soka la Tanzania, amezifundisha pia Cosmopolitan na Pan Africans kwa nyakati mbalimbali, huku akitazamiwa kukipigania kikosi hicho kirejee tena Ligi Kuu Bara, baada ya Stand kushuka daraja msimu wa 2018-2019.