UBABE MWINGI: Arne Slot na makocha wengine waliobeba mataji misimu ya kwanza

Muktasari:
- Ikiwa bado na mechi nne mkononi, kikosi hicho cha kocha Arne Slot kilinyakua taji hilo, huku kocha huyo Mdachi akiweka rekodi kwa kubeba ubingwa wa ligi katika msimu wake wa kwanza.
LONDON, ENGLAND: LIVERPOOL imeandika rekodi tamu kwenye Ligi Kuu England baada ya kunyakua taji lao la 20 huku ikiwa na mechi kibao mkononi.
Ikiwa bado na mechi nne mkononi, kikosi hicho cha kocha Arne Slot kilinyakua taji hilo, huku kocha huyo Mdachi akiweka rekodi kwa kubeba ubingwa wa ligi katika msimu wake wa kwanza.
Wakati kocha Jurgen Klopp anaachana na Liverpool mwishoni mwa msimu uliopita na Slot kuchaguliwa, wengi waliweka wasiwasi, lakini Mdachi huyo ameonyesha makali yake kwa kubeba ubingwa, huku akiwa bado na mechi za ziada mkononi.
Liverpool ilikuwa moto kwelikweli, ambapo safu yao ya ushambuliaji iliongozwa vyema kabisa na Mohamed Salah, huku beki ikiwa imara kabisa chini ya nahodha Virgil van Dijk, ambapo walikuwa na kazi moja ya kuikimbia Arsenal kwenye vita ya kuwania ubingwa.
Kwa kunyakua taji hilo, Slot, ambaye alikuwa kocha wa Feyenoord iliyonyakua taji la Eredivisie pia, anakuwa Mdachi wa kwanza kushinda ubingwa wa Ligi Kuu England katika msimu wake wa kwanza.
Lakini, je, ubingwa huo unamweka Slot kwenye namba gani katika orodha ya makocha mashuhuri kabisa waliopata kutokea kwenye Ligi Kuu England?
Slot anakuwa kocha wa saba kufanikiwa kubeba ubingwa huo, huku timu yake ikiwa bado ina mechi za kucheza ikiifanikiwa kuifikia Manchester United kwa kubeba mataji 20 ya ligi. Cheki hapa msimamo unavyosoma kile walichofanya makocha waliowahi kubeba ubingwa wa Ligi Kuu England kwenye misimu yao ya kwanza.

Alex Ferguson
Timu: Manchester United
Msimu: 1992-93
Ushindi: 24
Sare: 12
Vichapo: 6
Pointi: 84
Wastani wa ushindi: 57.1%
Kocha Alex Ferguson alitua Manchester United misimu sita na nusu kabla ya kuanza kwa Ligi Kuu England. Aliongoza timu hiyo kushika nafasi ya pili kwenye msimu wa mwisho wa Ligi Daraja la Kwanza. Lakini, kwenye msimu wa kwanza wa Ligi Kuu England, ambapo kipindi hicho kulikuwa na mechi nne zaidi na ilivyo kwa sasa, kocha huyo alifanya mambo yake kuwa matamu huko Old Trafford. Msimu huo, Man United ilimaliza ukame wa miaka 26 ya kubeba taji la ligi na hadi anaondoka kwenye timu hiyo, Ferguson alibeba mataji 13 ya Ligi Kuu England, saba juu ya mtu anayemkaribia, Pep Guardiola mwenye mataji sita ya Ligi Kuu England.

Claudio Ranieri
Timu: Leicester City
Msimu: 2015-16
Ushindi: 23
Sare: 12
Vichapo: 3
Pointi: 81
Wastani wa ushindi: 60.5%
Leicester City ilinyakua ubingwa wa Ligi Kuu England msimu wa 2015–16, ikiwa moja ya timu isiyotarajiwa kabisa kubeba taji hilo. Tofauti na makocha wengine waliopo kwenye orodha hii, Claudio Ranieri alikuwa tayari ana uzoefu wa Ligi Kuu England, ambapo aliwahi kudumu kwa karibu miaka minne huko Chelsea bila ya kunyakua taji lolote kabla ya kuja kurithiwa na Jose Mourinho. Baada ya kunusurika kushuka daraja msimu moja uliopita, Ranieri alifanya maajabu kwa kuipa ubingwa wa Leicester City, ambapo kwenye kikosi chake kulikuwa na mastaa wa maana kabisa kama N’Golo Kanté, Riyad Mahrez na Jamie Vardy kwa kuwataja kwa uchache.

Manuel Pellegrini
Timu: Manchester City
Msimu: 2013-14
Ushindi: 27
Sare: 5
Vichapo: 6
Pointi: 86
Wastani wa ushindi: 71.1%
Baada ya kumaliza nafasi ya pili nyuma ya Manchester United katika msimu wa 2012–13, Manchester City ilijaribu kutafuta namna ya kubeba ubingwa baada ya kumchukua Manuel Pellegrini kutoka Málaga. Kiwango chake cha mwanzoni mwa msimu hakikuwa kizuri, ambapo timu hiyo ilikuwa imekumbana na vichapo vinne hadi kufikia mwishoni mwa Novemba. Baada ya hapo, walipata kiwango chao bora na kucheza mechi 12 bila ya kupoteza, huku ikipata ushindi mnono kabisa dhidi ya Tottenham (6–0) na Arsenal (6–3). Baada ya hapo, Man City iliingia kwenye vita ya ubingwa na Liverpool, ambapo miamba hiyo ya Etihad ilivuka pointi 100 na kushinda ubingwa ikiwa imefunga mabao 102. Yaya Touré alikuwa na msimu bora kabisa, ambapo alifunga mabao 20 akitokea kwenye sehemu ya kiungo, wakati Sergio Agüero alifunga 17.

Carlo Ancelotti
Timu: Chelsea
Msimu: 2009-10
Ushindi: 27
Sare: 5
Vichapo: 6
Pointi: 86
Wastani wa ushindi: 71.1%
Katika majira ya kiangazi 2009, Carlo Ancelotti alichukua mikoba ya kuinoa Chelsea, akichukua mikoba ya Guus Hiddink. Katika msimu wake wa kwanza, Mtaliano huyo, anayeinoa Real Madrid kwa sasa, alifanya vizuri na kuifanya Chelsea kutamba kwenye ligi hiyo, ambapo ilimaliza msimu pointi moja juu ya wapinzani Manchester United. Katika msimu huo, Chelsea iliweka rekodi ya kufunga mabao 103 kwenye msimu mmoja wa Ligi Kuu England, huku straika Didier Drogba alimaliza akiwa kinara wa mabao, akifunga 29.

Arne Slot
Timu: Liverpool
Msimu: 2024-25
Ushindi: 25
Sare: 7
Vichapo: 2
Pointi: 82
Wastani wa ushindi: 73.5
Kufuatia kuondoka kwa Jürgen Klopp, Liverpoo ilianza msimu wa 2024–25 ikiwa timu inayopewa nafasi ya tatu kwenye uwezekano wa kushinda ubingwa wa Ligi Kuu England, nyuma ya Manchester City na Arsenal. Hata hivyo, uongozi wa kocha Arne Slot, uliisaidia timu hiyo kushinda ubingwa wa ligi ya msimu huu baada ya kucheza kwa kiwango bora kabisa. Liverpool ilinyakua taji na kutangazwa kuwa mabingwa wa Ligi Kuu England msimu huu baada ya ushindi wa 5-1 dhidi ya Tottenham uwanjani Anfield mwishoni mwa msimu uliopita na hivyo kuifikia Manchester United kwenye rekodi ya kushinda mataji 20 ya ligi. Hata hivyo, wadau wa michezo wanaamini Liverpool haikupata upinzani wa kutosha kwa msimu huu kwenye mbio za ubingwa.

Jose Mourinho
Timu: Chelsea
Msimu: 2004-05
Ushindi: 29
Sare: 8
Vichapo: 1
Pointi: 95
Wastani wa ushindi: 76.3%
Akitokea kubeba ubingwa wa Ligi ya Mabingwa Ulaya akiwa na kikosi cha Porto, José Mourinho, alijitangaza kwa jina la “Special One,” na alitua kwenye Ligi Kuu England kubeba ubingwa kwenye msimu wake wa kwanza huko Chelsea, akipata sapoti kubwa kutoka kwa tajiri Roman Abramovich. Mourinho msimu huo wa kwanza ndiyo ulioisaidia Chelsea kubeba taji lao la kwanza pia la Ligi Kuu England baada ya kufanya hivyo msimu wa 1954–55 ilipobeba ubingwa wa ligi, miaka 50 nyuma. Na hapo, Mourinho alikuwa kocha wa kwanza kutua kwenye Ligi Kuu England ndani ya msimu huo huo na kubeba ubingwa. Kikosi cha Chelsea kwenye msimu huo kilinyakua pointi 95, ambazo zilibaki kuwa rekodi hadi hapo Pep Guardiola na kikosi chake cha Manchester City ilipokuja kuipiku kwenye msimu wa 2017–18.

Antonio Conte
Timu: Chelsea
Msimu: 2016-17
Ushindi: 30
Sare: 3
Vichapo: 5
Pointi: 93
Wastani wa ushindi: 78.9%
Kocha Mtaliano, Antonio Conte alitua Chelsea na kutambulisha mfumo wa 3-4-3, ambao ulikuja kuwa balaa na kunyakua ubingwa wa Ligi Kuu England katika msimu wake huo wa kwanza. Conte alitua na kujipambanua kuwa mmoja wa makocha mahiri kuwahi kutokea kwenye Ligi Kuu England kutokana na kile alichokifanya. Baada ya kufanya vizuri huko Juventua na kisha kuiongoza Italia kwenye fainali za Euro 2016 alipofika robo fainali, Conte aliichukua Chelsea na kufanya vizuri kabisa. Kila kitu kilibadilika kwenye kikosi cha Chelsea katika msimu wa 2016-17, ambapo Chelsea iliibuka na ushindi kwenye mechi 30 kati ya 38 za msimu huo, rekodi ya kibabe kabisa katika msimu moja wa Ligi Kuu England.