Tusubirie mtihani huu kwa Kocha Minziro
Muktasari:
- Kwa nafasi ambayo Fountain Gate ipo, ni wazi Minziro hana kibarua chepesi na ana kazi kubwa ya kufanya ili kuiwezesha timu hiyo ibaki Ligi Kuu.
WALE Fountain Gate hadi wameamua kumchukua Fred Felix 'Minziro' na kumpa kibarua cha kuinoa timu yao, basi wameamua kujilipua sana hasa kwa dakika hizi.
Hapa kijiweni tunaamini kwamba huo ni uamuzi wa kujitoa muhanga sana kwa sababu mechi zimebaki chache na mabadiliko ya benchi la ufundi mara nyingi huwa yanahitaji muda.
Kwa nafasi ambayo Fountain Gate ipo, ni wazi Minziro hana kibarua chepesi na ana kazi kubwa ya kufanya ili kuiwezesha timu hiyo ibaki Ligi Kuu.
Ugumu mkubwa kwa Minziro ni kwamba hana tena muda wa kutosha wa kuwaingizia mbinu mpya wachezaji wake kwa sababu ratiba inabana na hana tena fursa ya kusajili wachezaji wapya wa kuiimarisha timu.
Maana yake atalazimika kuwatumia wachezaji waliopo katika hiki kipindi cha kuelekea mwishoni mwa msimu ili kuinusuru timu.
Hata hivyo, kijiwe kinaogopa kumkatia tamaa Minziro kwa sababu ni kocha fulani hivi ambaye amekuwa na historia nzuri ya kuzinusuru timu zisishuke daraja hata akipewa katika dakika za jioni.
Huyuhuyu Minziro hivi karibuni aliitoa shimoni Pamba Jiji FC ambayo ilikuwa inakaribia kushuka daraja na akaweza kuibakisha katika ligi.
Amewahi kuinusuru pia Tanzania Prisons isishuke daraja baada ya kukabidhiwa katika kipindi ambacho ilikuwa na hali mbaya.
Jukumu alilokubali kulibeba ni zito hasa lakini tukikumbuka historia yake, tunaona kama anaweza vile kuibakisha Fountain Gate.