Tunisia, Cape Verde zinatupa majibu Afrika
Muktasari:
- Tuanzie kwa Cape Verde ambayo ndio inashiriki kwa mara ya kwanza mashindano hayo na hadi sasa haijapoteza mechi zake zote mbili za mwanzo za hatua ya makundi dhidi ya Hispania na Uruguay.
KUNA majibu fulani ambayo Afrika tunayapata katika fainali za Kombe la Dunia zinazoendelea huko Marekani, Canada na Mexico kutokana na ushiriki wa timu za Tunisia na Cape Verde.
Tuanzie kwa Cape Verde ambayo ndio inashiriki kwa mara ya kwanza mashindano hayo na hadi sasa haijapoteza mechi zake zote mbili za mwanzo za hatua ya makundi dhidi ya Hispania na Uruguay.
Wachezaji wake wanacheza soka la kulipwa Ulaya na kundi kubwa wamezaliwa na kukulia barani humo.
Hii inatuonyesha mchango wa wachezaji waliopo katika klabu mbalimbali Ulaya na nje ya Afrika bado unahitajika kwa kiasi kikubwa kwa timu zetu za taifa ili zifanye vyema katika Kombe la Dunia.
Wanakuwa na uzoefu wa kushindana na timu za mataifa ya Ulaya kwa vile wanawafahamu vyema wachezaji wanaounda vikosi vya timu hizo kwani wamelelewa katika mazingira yaleyale na madaraja hayapishani sana.
Tuje kwa Tunisia sasa. Imeaga mapema katika Kombe la Dunia baada ya kuchapwa mechi zake mbili za mwanzo dhidi ya Sweden na kisha Japan huku ikiruhusu nyavu zake kutikiswa mara tisa.
Kinachoshangaza zaidi ni Tunisia ilifuzu Fainali za Kombe la Dunia mwaka huu ikiwa haijapoteza mchezo huku pia ikiwa haijaruhusu bao lolote kwa huku Afrika.
Hapa tunapata jibu kwamba ushindani wa timu za taifa Afrika bado upo chini kiasi ambacho nyingi zinashindwa kuwa kipimo kizuri cha kuzijenga timu zetu ambazo zinakwenda kushiriki mashindano makubwa kama ya Kombe la Dunia.
Ukipata mechi rahisi katika kufuzu, usitegemee utatoboa mbele ya timu ambazo zimepitia kaa la moto katika kufuzu kwenye mabara mengine.