Kali Ongala: Mzaliwa wa England anayebeba matumaini KMC

Muktasari:
- Muda mfupi baada ya Moallin kuachia ngazi, uongozi wa KMC ulifanya mazungumzo ya haraka na kocha Kally Ongala na kumsainisha haraka mkataba wa kuinoa timu hiyo.
KMC hivi karibuni ilipata pigo la ghafla baada ya kocha wake Abdihamid Moalin kuwasilisha rasmi ombi la kuvunja mkataba wa kuitumikia timu hiyo akihitimisha mwaka mmoja na ushee alioitumikia timu hiyo.
Muda mfupi baada ya Moallin kuachia ngazi, uongozi wa KMC ulifanya mazungumzo ya haraka na kocha Kally Ongala na kumsainisha haraka mkataba wa kuinoa timu hiyo.
Jukumu kubwa ambalo Ongala analo ndani ya KMC ni kuhakikisha timu hiyo inamaliza ndani ya nafasi nne za juu kwenye msimamo wa ligi pamoja na kufanya vizuri katika Kombe la Shirikisho la CRDB.
Uamuzi wa kumchukua Ongala hauonekani kama umechukuliwa kwa bahati mbaya bali ni kocha huyo kuonekana anakidhi vigezo mbalimbali ambavyo kocha wa timu kama KMC anapaswa kuwa navyo.

Kipenzi cha vijana
KMC ni timu ambayo imekuwa kwa muda mrefu ikitoa kipaumbele kwa vijana wenye umri mdogo kuonyesha vipaji vyao na Kally anaonekana kuwa kocha sahihi ambaye ataendeleza utamaduni huo.
Historia ya Ongala katika ukocha inaonyesha ni mtu ambaye amekuwa akitoa fursa kwa wachezaji wenye umri mdogo kuanzia alipofundisha Majimaji ya Songea na baadaye Azam FC.
Miongoni mwa vijana ambao Kally Ongala aliwapa fursa kubwa ya kucheza Ligi Kuu ni Alex Kondo, Tariq Simba, Tepsi Evance, Lucas Kikoti na Lusajo Mwaikenda.
Kocha huyo alisema anataka kuona wachezaji wengi wenye umri mdogo wanapata nafasi kwani ndio hazina ya taifa kwa siku za usoni.
“Napenda kuwapa nafasi vijana kwa sababu naamini huo ndio muda sahihi kwao kucheza kwa faida yao wenyewe, klabu na timu ya taifa.
“Lakini ni lazima mchezaji anionyeshe kama anastahili kupata nafasi. Siwezi kumpa nafasi ambaye hajitumi au anayeshindwa kufanya kile anachoelekezwa,” anasema Ongala.

KMC mambo safi
Ongala anasema hakuamua kujiunga na KMC kwa kukurupuka bali alifanya tathmini ya kina ambayo mwisho wa yote ilimfanya akoshwe na mipango ya timu hiyo.
‘Licha ya kupokea ofa nyingi kutoka timu mbalimbali, nilivutiwa sana na mpango wa KMC FC. Matarajio yangu ni kuhakikisha timu inamaliza msimu huu ikiwa kwenye nafasi nzuri katika msimamo wa ligi,” anasema Ongala.
Kocha huyo anasisitiza kwamba ili kile ambacho timu imekipanga ili kitimie, ni lazima kuwepo na ushirikiano wa mashabiki, viongozi na timu.

Mzaliwa England
Ongala alizaliwa London, England Agosti 31, 1979 lakini baada ya hapo makuzi na malezi yake aliyapatia jijini Dar es Salaam.
Baba yake ni Marehemu Ramadhan Mtoro Ongala ambaye alikuwa mwanamuziki gwiji nchini na mama yake Muingereza alikuwa ni mwalimu.
Kisoka alianzia katika timu ya Abajalo na kisha akazichezea, Yanga, Kajumulo, Vasby United, Umea, Azam FC na Sundsvall.