Prime
EXCLUSIVE: Bajana afichua alivyoikataa Simba dakika za mwisho
ILIPOISHIA.... Jana katika mahojiano na nahodha wa zamani wa Azam FC, Sospeter Bajana alizungumzia mambo mbalimbali ikiwamo siri ya kuishi miaka 15 kwa matajiri wa Chamazi na jeraha la goti lilivyotishia soka lake. Lakini, unakumbuka dirisha kubwa la usajili mwaka jana tetesi zilimhusisha na Simba na kwa nini ameamua kutua JKT Tanzania? SASA ENDELEA..
KILICHOMVUTIA JKT
Bajana ambaye amesaini mkataba wa miaka miwili baada ya kumalizana na Azam FC, anatoboa siri ya yeye kuichagua JKT Tanzania licha ya ofa kubwa zilizowahi kuja mezani.
"Cha kwanza ni timu yao ni ya ushindani kama nilivyo mimi. Kwa hiyo nilichagua kikosi ambacho kitanitoa hatua moja kwenda nyingine, kingine ni kocha waliyenaye.
"Soka lake linanifurahisha na ninaona kabisa kuwa nastahili kuchezea JKT na tulicheza mechi nzuri ya kirafiki ya pre-season na Yanga."
SIRI YA JEZI 17
"Nilipofika JKT Tanzania mapokezi yalikuwa mazuri, lakini taarifa mbaya ikawa jezi ninayoipenda ikawa imechukuliwa, ila nilitumia busara nikamfuata aliyeichukua na kuzungumza naye.
"Nikamuomba na kwa heshima aliyonipa kama kaka akanipa, alipokubali nikaenda kwa viongozi wakanipatia rasmi.
"Siku ya kwanza yalikuwa mazoezi mazuri yenye ari. Ukiangalia timu, marafiki na jezi ni vipya kwa hiyo ilikuwa nzuri. Ma morali ilikuwa ya kutosha, kocha pia ni mtu mzuri ambaye falsafa zake zinajulikana."
OFA KIBAO
Bajana anakiri kwamba amewahi kupokea ofa nyingi sana zilizomuhitaji na wala sio timu ndogo, kwa sababu ya uwezo wake, lakini hakufanikiwa kwenda.
"Kwa mchezaji kama mimi kutakiwa na timu kubwa sio suala la ajabu, nimeshawahi kuzungumza na msaidizi wangu juu ya hizo ofa, lakini mwisho tukaamua kubaki Azam."
SIMBA BADO KIDOGO
"Simba ni moja kati ya timu ambazo zimenihitaji zaidi ya Yanga, ilibaki kidogo nisaini Simba, ila mambo hayakwenda sawa, pia ilinibidi nibaki Azam. Mapenzi yalinisukuma sana, ila asilimia 90 nilitakiwa kwenda Simba kabla sijavunja mkataba wa sasa. Nakumbuka hata msaidizi wangu aliwahi kuniambia shida yangu naipenda sana Azam.
"Simba ilikuja kufanya mazungumzo nami, unajua hiyo ni dili kubwa kwa hiyo kulikuwa na nenda rudi nyingi, lakini wakati huo huo Azam pia walikuwa wanataka nisaini mkataba mpya.
"Ilikuwa nikitoka tu kwenye mechi ya mwisho wa ligi naenda kusaini na Simba, lakini mbele yetu kulikuwa na fainali na Yanga, nikawaambia viongozi wa Azam kuwa nikitoka kwenye geti nitakuwa sio mchezaji wao, basi wakanipa mkataba na wakanipa ninachokitaka.
"Kilichonivutia zaidi Simba ni umakini wao, walionyesha wananihitaji kwa vitendo, pia kule kulikuwa na rafiki yangu kipenzi Aishi Manula," anasema Bajana.
NJE YA BONGO
Anasema kuwa: "Ni ndoto ya kila mchezaji kuchezea soka la nje na pia jitihada tunazifanya ili kwenda Ulaya, ila tukumbuke nchi yetu iko chini kwa hiyo ni ngumu kupata timu moja kwa moja kule.
"Bado ndoto yangu ipo na umri wangu unaruhusu kucheza nje, ila sijajua kama Mungu kaniandikia kucheza nje, kama ipo basi kwa wakati wake itakuja, ijapokuwa sijawahi kuzungumza na timu yoyote ya nje."
KUCHEZA STARS
Anasimulia jinsi alivyopata nafasi ya kuchezea kikosi cha Taifa Stars; "Sijacheza kwa muda mrefu kwa kweli, nilikuwa katika timu za vijana, kisha kwa wakubwa mchezo wangu wa kwanza ni mechi ile ya kufuzu Afcon dhidi ya Algeria.
"Hii ni ndoto ya kila mchezaji kulipigania taifa lako na ni daraja la mwisho kwa nchi yetu, namshukuru Mungu kuisaidia timu yetu, ilikuwa ngumu kwa sababu tulicheza na wakubwa wa soka la Afrika na ilikuwa ugenini na tulikuwa tunahitaji alama moja, ili tufuzu.
"Mwanzoni sikufikiria kama nitacheza. Nakumbuka tulikuwa kwenye uwanja wa ndege, kocha akaniambia 'utacheza', niliogopa kwa sababu nilijua mechi ingekuwa ngumu, labda mwalimu alinichagua kwa sababu ya upambanaji wangu ila nilionyesha na ikaniongezea fursa ya kuaminika zaidi."
AZAM IZINGATIE HAYA
Bajana anasema anakumbuka mafanikio aliyoyapata akiwa Azam, akiyataja: "Imenipa maisha ya kawaida ya Mtanzania, vile vitu ambavyo sikuwanavyo, nimevipata kupitia wao, ndoto zangu zimetimia kwa asilimia kubwa.
"Vile ambavyo havikuwapo nyumbani wakati nakua mkubwa, sasa ninavyo kwa hiyo namshukuru Mungu, kama kula yenu ilikuwa ya shida, sasa mko sawam sio jambo dogo."
Bajana anaitaka pia timu yake hiyo ya zamani ifanye mambo kadhaa ili ibaki juu au ipige hatua kisoka.
"Mimi sasa nabaki kama shabiki wa Azam FC, na kweli kabisa niseme tu kocha atakuwa na kazi kama baadhi ya mambo ya muhimu hayatabadilika. Jambo la kwanza, kubadilisha makocha, huyu aliyeko sasa anahitaji muda zaidi kusuka kikosi ambacho kitafanya mapinduzi na sio suala la miezi sita au mwaka.
"Kuna changamoto kubwa ya kubadilisha makocha, unakuta anakuja anakaa msimu mmoja anaondoka, kila mwalimu ana falsafa zake, hivyo haiwezi kuwa rahisi kujenga timu kwa muda mfupi.
"Ishu ya usajili pia ni tatizo, Azam mara nyingi inachukua wachezaji kutoka nje ambao wana viwango vya kawaida, wakija hapa hawana wanachoongeza kwenye timu."
Ibenge kwa sasa ndiye kocha wa Azam FC akitoka Al Hilal ya Sudan, ambayo alikuwa akiifundisha msimu uliomalizika na kucheza michuano ya Ligi ya Mabingwa.
MANULA ZAIDI YA RAFIKI
Bajana anamtaja Aishi Manula kama ndugu: "Mimi nina rafiki kama ndugu na marafiki tu, huyo ni Manula. Ukiacha tu kuishi jirani hapa Chamazi, pia tumecheza wote Azam tulipokuwa wadogo.
"Tulisoma wote tulikutana Azam wakati huo tukapelekwa shule moja, namkubali kwa sababu ana sifa kama zangu, mpole, mcheshi na mpenda familia.
"Kuondoka kwake Azam kuliniumiza, sikutaka kusikia wala kuiona, alivyoniambia anaondoka niliumia sana, haikuwa vizuri kwa sababu majukumu yanaenda tofauti ila hakuna kilichobadilika.
"Hata kukaribia kuikubali Simba ilikuwa ni ushawishi wake, mpaka anafika yeye kuja Azam nilikuwapo mpaka anasaini mkataba, utadhani msimamizi wake, nilifurahi kwa kweli, lakini ndio hivyo nimemuacha tena.
"Ilivyofika muda wa kuondoka nilishindwa kumuaga kwa simu, ila alivyoambiwa akaanza kunipigia, nikamwambia nataka tuonane ndio tuongee, ilikuwa taarifa mbaya kwetu."
USOJA
"Kama nisingekuwa mchezaji basi ningekuwa mwanajeshi, ila kwa sasa hivi sijioni huko, hata nilivyoenda JKT walianiambia unaweza kuwa mwanajeshi, lakini nilikataa.
"Nilikuwa nawaza kuwa mwanajeshi, Mungu kanileta huku. Ijapokuwa kwa sasa sio ndoto zangu, lakini huwezi kujua ya kesho, pengine nitakuwa mwanajeshi."
WAZAZI YANGA
Bajana anasema kipindi cha nyuma ilikuwa ni ngumu kwa wazazi kukubali mtoto akacheze soka, au mmoja anaweza kukubali na mwingine akagoma.
"Baba yangu ni shabiki wa Yanga, lakini hakuamini maisha ya kupitia mpira wa miguu, kwa hiyo ule muda wa mpira yeye ndio anakupa kazi nyingi ili tu usiende kucheza mpira. Aliona kama nilikuwa napoteza muda tu.
"Lakini vikwazo vyake vilinipa ari ya kupambana ili nimuonyeshe kwamba anaweza kujivunia mimi kupitia kazi yangu ya mpira, namshukuru kwa makofi yake aliyokuwa ananipiga ya kunionya, yamenisaidia kupambana ili nifikie malengo.
"Tukicheza na Yanga, wanakuwa upande wangu, lakini ukiwafunga unaona kabisa, mioyo yao inauma na wanakwambia wakati mwingine, ila ndio hivyo si unajua ushabiki."
MCHEZAJI BORA
Bajana anasema wapo mastaa ambao anawakubali sana kwa wazawa na wageni. "Namkubali sana Aggrey Moris, lakini kwa wale wa kutoka nje ya nchi ni Kipre Junior.
"Nimejifunza uongozi kwa Aggrey Moris na alikuwa rafiki yangu. Ni mtu unayeweza kumtegemea, Kipre ana uwezo wa kukuamulia mechi muda wowote wakati ambao hakuna matumaini kabisa."
AZAM KUBEBA UBINGWA
Msimu ambao Azam ilibeba ubingwa wa Ligi Kuu Bara mwaka 2013 kwa mara ya kwanza, Bajana anauita huo kama ndio msimu bora zaidi kwake kwenye maisha ya soka.
"Nilinyanyua kombe kwa mara ya kwanza nikiwa kijana mdogo na nilikuwa na malengo ya kuisaidia kuipambania timu yangu, sikucheza mechi nyingi msimu huo ila ulikuwa bora."
MBEYA CITY
Bajana pia amewahi kuichezea Mbeya City, hapa anasema wapi inapokwamia; "Mbeya City nimeiona wakati inacheza na Azam FC kwenye ufunguzi.
"Lakini ili wabaki kwenye nafasi zao inabidi Viongozi wakae chini kujitathimi ni wapi walipokosea wakati ule na walifanikiwa wapi mpaka timu inashika nafasi ya tatu kwenye ligi.
"Ili waweze kurudi kwenye nafasi zao ni lazima kwanza wajue ni wapi wanapokosea, baada ya hapo watafanya vyema kwa sababu wachezaji wanao."