Championship ni mwendo wa shangwe, vilio
Muktasari:
- Wakati ligi hiyo ikipamba moto, kuna timu na wachezaji ambao wamekuwa na kipindi kizuri na wengine kupitia changamoto mbalimbali za kukosa mwendelezo mzuri kutokana na ugumu uliopo, kama Mwanaspoti linavyoelezea kilichotokea hadi sasa.
UHONDO wa Ligi ya Championship unaendelea kushika kasi na hadi sasa tayari zimepigwa mechi za raundi tisa kwa kila timu, huku ushindani ukiendelea kuonekana siku hadi siku, jambo linaloonyesha msimu huu umekuwa mgumu na usiotabirika.
Wakati ligi hiyo ikipamba moto, kuna timu na wachezaji ambao wamekuwa na kipindi kizuri na wengine kupitia changamoto mbalimbali za kukosa mwendelezo mzuri kutokana na ugumu uliopo, kama Mwanaspoti linavyoelezea kilichotokea hadi sasa.
CHIRWA AWEKA REKODI
Mshambuliaji wa Kagera Sugar, Mzambia Obrey Chirwa ameweka rekodi ya mchezaji wa kwanza wa Ligi ya Championship msimu huu kufunga mabao matatu (Hat-Trick), wakati kikosi hicho kilipoifunga Hausung kutoka Njombe mabao 3-1, Desemba 2, 2025.
Katika mechi hiyo iliyopigwa kwenye Uwanja wa Kaitaba Bukoba, mshambuliaji huyo wa zamani wa Yanga, Azam, Namungo, Ihefu ambayo kwa sasa ni Singida Black Stars na KenGold, alifunga mabao hayo na kufikisha matano hadi sasa na kikosi hicho.
ABRAHAMAN HAKAMATIKI
Mshambuliaji huyo aliyejiunga na Gunners ya jijini Dodoma iliyopanda daraja msimu huu akitokea kwa maafande wa Mashujaa, amekuwa na kiwango kizuri hadi sasa kwani ndiye anayeongoza kwa kufunga mabao mengi, akiwa nayo manane na kikosi hicho.
Nyota huyo ambaye msimu wa 2024-2025, wa Ligi Kuu Bara alifunga bao moja tu akiwa na Mashujaa, amekuwa na kiwango bora na kikosi hicho chenye makao yake makuu jijini Dodoma, kinachoshiriki ligi hii kwa mara yake ya kwanza.
Abrahaman anakumbukwa zaidi kwa msimu wa 2016-2017, akiwa na Ruvu Shooting na alikuwa mfungaji bora wa Ligi Kuu Bara baada ya kufunga mabao 14, sawa na Simon Msuva aliyekuwa anaichezea Yanga japo kwa sasa anaichezea Al-Talaba SC ya Iraq.
MAAFANDE HALI TETE
Baada ya Polisi Tanzania kuanza msimu huu vizuri kwa kushinda mechi tatu mfululizo za mwanzoni, mashabiki walikitabiria kikosi hicho cha maafande kingekuwa na mwenendo mzuri, ingawa ghafla hali hiyo imekuwa ni tofauti na matarajio ya wengi.
Katika mechi sita zilizopita, timu hiyo imechapwa mbili na kutoka sare nne, ikiwa haina mwendelezo mzuri, jambo ambalo limeanza kuonyesha wasiwazi huenda kikosi hicho kisitimize adhima ya kurejea tena Ligi Kuu baada ya kushuka 2022-2023.
Timu hiyo msimu uliopita wa 2024-2025, haukuwa mzuri sana baada ya kumaliza nafasi ya 10, katika Ligi ya Championship na pointi 33, ikishinda mechi nane, sare tisa na kupoteza 13, huku safu ya ushambuliaji ikifunga mabao 44 na kuruhusu 33.
Kikosi hicho kinapambana ili kurejea tena Ligi Kuu Bara baada ya kushuka daraja msimu wa 2022-2023, kilipomaliza nafasi ya 15 na pointi zake 25, baada ya kushinda mechi sita tu, sare saba na kupoteza 17, kikifunga mabao 25 na kuruhusu 54.
MBILI BADO HAKIJAELEWEKA
Katika timu 16 zinazoshiriki Ligi ya Championship msimu huu, hadi sasa ni mbili tu ambazo hazijaonja ladha ya ushindi, ambazo ni Barberian zamani Kiluvya United iliyocheza mechi tisa na imetoka sare tatu na kuchapwa sita.
Barberian inayoshika nafasi ya 15 na pointi tatu, katika mechi hizo tisa imefunga mabao matano na kuruhusu 18, huku timu nyingine ni B19 zamani Tanesco, iliyochapwa mara saba na kutoka sare moja.
B19 inayoshiriki Ligi ya Championship kwa mara ya kwanza msimu huu, imekuwa haina mwenendo mzuri, ikifunga mabao manne na kuruhusu nyavu zake kutikiswa mara 17 na kikosi hicho kinaburuza mkiani mwa msimamo na pointi zake mbili.
MBEYA KWANZA MWENDO MDUNDO
Mbeya Kwanza iliyouzwa kwa Halmashauri ya Manispaa ya Tabora ikitokea Lindi ilipoweka kambi kwa msimu uliopita wa 2024-2025, baada ya kuchapwa mechi tatu mfululizo za mwanzoni, kwa sasa kikosi hicho hakikamatiki kutokana na kiwango kizuri.
Timu hiyo iliyoshuka daraja kutoka Ligi Kuu Bara hadi Championship msimu wa 2021-2022, ilipomaliza mkiani na pointi 25, kwa sasa imecheza mechi sita mfululizo na kushinda zote, ikiwa ni kiwango bora baada ya kupoteza mechi tatu za mwanzoni.