Arajiga, Mpanga mkatuheshimishe AFCON U17
Muktasari:
- Kwanza yatarudisha utulivu wao na kuwaweka sawa kisaikolojia baada ya wote wawili kupitia misukosuko ya kufungiwa siku za hivi karibuni kwa upungufu uliojitokeza katika mechi tofauti walizochezesha.
MAREFA wetu wawili wameteuliwa kuchezesha Fainali za Mataifa ya Afrika kwa vijana chini ya umri wa miaka 17 (AFCON U17) ambazo zitafanyika Morocco mwezi ujao kuanzia Mei 13, 2026 hadi Juni 2, 2026.
Marefa hao ni Ahmed Arajiga ambaye amechaguliwa katika kundi la marefa wa kati na mwingine ni Kassim Mpanga aliyeteuliwa kuingia katika kundi la waamuzi wa pembeni watakaochezesha fainali hizo.
Haya ni mashindano muhimu sana kwa Arajiga na Mpanga kupata fursa ya kuchezesha na yatakuwa na faida kubwa kwao binafsi ingawa pia nchi itanufaika pia.
Kwanza yatarudisha utulivu wao na kuwaweka sawa kisaikolojia baada ya wote wawili kupitia misukosuko ya kufungiwa siku za hivi karibuni kwa upungufu uliojitokeza katika mechi tofauti walizochezesha.
Arajiga alifungiwa baada ya kutoa penalti dhidi ya Mashujaa FC katika mechi ya Ligi Kuu kati yao na Simba iliyochezwa katika Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo, Januari 29, mwaka huu na Mpanga alifungiwa kwa miezi sita baada ya kufanya kosa katika mechi ya mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu msimu huu baina ya Yanga na Simba.
Ukiondoa hilo, faida nyingine kwa Arajiga na Mpanga kwa kuteuliwa kuchezesha AFCON U17 mwaka huu ni kujitengenezea fursa kwa ajili ya kuendelea kuteuliwa kuchezesha mashindano mengine ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) siku za usoni.
Kwa sasa wamekuwa hawapati nafasi hiyo mara kwa mara lakini wakifanya vyema katika jukumu lililo mbele yao hapana shaka CAF itawatazama kwa jicho la kipekee kama ambavyo hutazamwa marefa wa nchi nyingine.
Pia hiyo ni fursa nzuri kwa Mpanga na Arajiga kuzidi kupata uzoefu wa kuchezesha fainali za mashindano makubwa jambo ambalo litazidi kuimarisha uwezo wao wa kuchezesha zaidi ya ubora walionao sasa.
Kazi kwao marefa wetu hao wawili na kijiwe kinawatakia kila la kheri katika kibarua kilicho mbele yao mwezi ujao huko Morocco.