Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

HADITHI: Bomu Mkononi - 7

Muktasari:

  • Mishi, binti mrembo wa Kitanga, anakolea kwa kijana dereva wa malori, Musa, ambaye amefika bei anataka kumuoa. Hapa Mishi yuko kwa kungwi.

Niliingizwa ndani ya nyumba hiyo nikapelekwa uani ambako kulikuwa na vyumba vinne. Huyo kungwi mwenyewe alitupokea na kutuingiza katika chumba kimojawapo. Tulipoingia katika chumba hcho ndipo nilipofunguliwa ushungi.

Kungwi mwenyewe alikuwa mwanamke wa makamo kidogo lakini hakuwa mtu mzima sana. Licha ya umri wake kuonekana kuwa mkubwa alikuwa amevaa kisichana na kuweka nywele zake vizuri. Alikuwa amependeza.

Nikakitazama kile chumba tulichoingia. Kilikuwa chumba kidogo kilichotosha kitanda cha futi nne, kabati la futi tatu na kochi moja. Hakukuwa na kitu kingine.

Nafasi ndogo iliyokuwa mbele ya kitanda ilitandikwa mkeka tuliokwenda nao.

“Kaa hapa kwenye mleka.” Kungwi wangu akaniambia.

Nikakaa. Kungwi alichukua ile ndundu ya vitu tuliyokwenda nayo akaiweka kwenye kochi na kuanza kuisasambua. Aliweka kando kitu kimoja kimoja kama aliyekuwa akivihakiki.

“Kama kuna kilichopungua utatuambia.” Mmoja wa wale wadada niliokwenda nao akamwambia.

“Naona viko sawa lakini kama nitagundua kuna kitu kilichokosekana nitawambia hata kama ni kesho.”

“Tumeambiwa na shangazi yake kuwa atakuwa hapa kwa wiki moja. Jumapili ijyo ndio harusi. Ataolewa saa mbili usiku. Kwa hiyo mchana atapelekwa saluni. Akitoka saluni anarudishwa nyumbani.”

“Kumbe nitakaa naye kwa muda mfupi tu. Lakini wiki moja pia inatosha. Sema tu mmemchelewesha.”

“Ndivyo shangazi yake alivyopanga.”

“Lakini hakuna tatizo.”

Wale wadada walikuwa bado wamesiamama wakimsikiliza yule kungwi.

“Mbona hamkai jamani, kochi hili hapa. Mnaweza kuja kukaa.” Kungwi  huyo akawaambia.

“Hatutakaa, tumemleta huyu mwari wako tu kisha turudi. Tumeacha kazi mikononi.” Dada mmoja akamwambia.

“Teksi inatusubiri huko nje.” Dada mwingine akaongeza.

“Basi sawa, ngojeni niwatoe nisiwapotezee muda.” Kungwi akawaambia na kuinuka.

Aliwatoa wale wadada na kuwasindikiza nje. Baada ya muda kidogo akarudi. Alipoingia mle chumbani alianza kupanga vile vitu na kuviweka kwenye kabati.

Alipomaliza alikaa kwenye kochi na kuniuliza.

“Unaitwa nani mdogo wangu?”

“Naitwa Mishi.”

“Na huyo mchumba wako anaitwa nani?”

“Anaitwa Musa.”

“Anafanya kazi gani?”

“Ni dereva wa malori.”

“Malori yale makubwa yanayosafiri nchi za nje au ya hapa hapa nchini?”

“Ni yale makubwa. Anaenda Rwanda, Burundi na wakati mwingine Zambia.”

“Akiondoka anakaa wiki moja, mbili, ndio anarudi?”

“Anakaa hata mwezi.”

“Alikuja kukuposa nyumbani kwenu au mlikuwa marafiki kabla ya hapo?”

“Tulikuwa marafiki.”

“Mlikuwa marafiki kwa muda gani”

“Kama miezi minne hivi.”

“Kwa hiyo mnajuana vizuri tabia zenu?”

“Tunajuana.”

Kungwi huyo alinitazama kisha akaniuliza.

“Unamuonaje, ametulia na anakujali?”

“Ninavyomuona mimi ametulia na ananijali. Zamani aliwahi kuoa mke ambaye waliachana.”

“Ni kijana mdogo au mtu mzima?”

“Bado ni kijana tu.”

Kungwi huyo alijiweka sawa kwenye kochi kisha akaniambia.

“Kuolewa na mtu mzima ni tofauti na kuolewa na kijana mdogo.”

“Tofauti yake ni nini?” Nikamuuliza ili nijue.

“Kuna tofauti kubwa. Kwa vile mimi ndiye kungwi wako inabidi nikuambie ili nikufundishe stadi za ndoa.” Kungwi wangu akaniambia na kuniacha na shauku ya kutaka kujua.

Alinyamaza kidogo kisha akaendelea.

“Tofauti yake ni kwamba mtu mzima tayari anayajua maisha, kijana ndio anajifunza sasa maisha. Mtu mzima hawezi kukuringia wewe au kukuletea jeuri hata kama ana pesa. Na anajua ni kwa jinsi ipi ataweza kuishi na wewe vizuri. Mtu mzima si rahisi kukumbwa na vishawishi vya nje ya ndoa kama ilivyo kwa kijana mdogo na uwezo wake wa kuvumilia vishindo vya ndoa ni mkubwa kuliko wa kijana. Sijui umenielewa?”

“Nimekuelewa.”

“Ndio sababu nikakwambia kuolewa na mtu mzima ni tofauti na kuolewa na kijana mdogo ambaye anayaanza sasa maisha.”

“Lakini huyo mchumba wangu ameshawahi kuwa na mke, si mdogo sana.”

“Haina tatizo. Wala simaanishi kuwa kuolewa na kijana ni tatizo ila nilitaka kukwambia kuwa kuolewa na mtu mzima si sawa na kuolewa na kijana kutokana na hizo sababu nilizokueleza.”

“Sawa, nimekuelewa.”

“Siri za kudumisha ndoa yako, ni kumpenda mume wako kwa dhati, kutomdharau hata kama ni masikini, kuwa mwaminifu na kumuomba msamaha pale unapoona umemkasirisha.” Kungwi wangu aliendelea kuniambia kisha akaongeza.

“Katika maisha yako ya ndoa epuka sana kumfanyia gubu mume wako. Gubu linapozidi atatoka nje, nina maana atatafuta nyumba ndogo ya kumpa faraja. Kama zamani alikuwa anarudi nyumbani saa nne usiku, mwisho atakuwa anarudi saa saba usiku. Anaanza kupitia katika nyumba ndogo yake ambako anaheshimiwa.”

“Ni kweli,” nikamkubalia.

“Kwa vile tutakuwa pamoja kwa wiki nzima nitakueleza mengi ambayo yatakusaidia huko unakokwenda.’

“Nitashukuru sana.”

“Kwa hiyo muda huu utakwenda kuoga ili nianze kukusinga. Sasa inuka uvae khanga zako, jifunge taulo yako uvae mitalawanda yako.”

Nikainuka na kuvua nguo nilizokuwa nimevaa. Nikajifunga khanga moja mabegani. Kiunoni nikajifunga taulo. Kungwi wangu alinitanda khanga nyingine kisha akanitolea mitalawanda yangu. Mitalawanda ni aina ya sendoz za kiasili zinazitengezwa kwa mbao kwa ajili ya kwenda kuogea.

“Sasa nifuate nyuma yangu.” Kungwi akaniambia huku akitangulia kutoka.

Nikamfuata nyuma nyuma.

Alinipeleka bafuni, akasiamama pembeni mwa mlango wa bafu na kuniacha niingie.

“Utakapomaliza kuoga usitoke peke yako, ukifungua mlango nitakuja kukutoa,” akaniambia.

Nikaingia bafuni. Nikavua khanga na kuoga. Kwa vile nilikuwa nimeshaoga nyumbani sikuchukua muda mrefu nikamaliza.

Nilijifuta maji kwa taulo kisha nikajifunga khanga yangu. Ile taulo niliyojifunga kiunoni kwa vile khanga niliyojifunga ilikuwa inaonyesha na mimi sikuwa na nguo nyingine ya ndani.

Nikajitanda ile khanga ya ziada kisha nikafungua mlango wa bafu. Kungwi wangu hakuwa mbali. Aliponiona akanifuata.

Alisimama mbele yangu akaniambia.

“Haya twende.”

Nikamfuata nyuma nyuma hadi tukaingia chumbani.

“Fungua khanga zako ukae hapo hapo kwenye mkeka wako.”

“Nikae mtupu?’ Nikamuuliza.

“Ndio, kaa mtupu.”

Nikajifungua ile khanga niliyokuwa nimejifunga kisha nikakaa.

“Nyoosha mbele miguu yako.” Kungwi akaniambia.

Nikanyoosha miguu yangu.

Kungwi alikuwa ameshatayarisha msio uliochanganywa na mafuta ya nazi akaanza kunipaka mwilini. Alinipaka mwili mzima mpaka usoni.

“Hii ndio krimu ya kiasili, sio zile kemikali za madukani zinazowachuna ngozi na kuwaharibu. Huu msio unatunza ngozi yako na kukufanya uonekane mrembo maridhawa. Unaweza kujisinga kila wiki mara moja ukiwa nyumbani kwako.” Kungwi aliniambia.

Baada ya kumaliza kunipaka alikaa kwenye kochi tukaanza kuzungumza.

“Ngoja sasa ukauke,” akaniambia.

“Umesema huu msio utanifanya nionekane mrembo?” Nikamuuliza.

“Utaona mwenyewe. Katika mwili kuna taka zinazishika kwenye ngozi ambazo haziondoki kwa sabuni. Taka hizo zinatokana na mafuta ya mwili na minunurisho ya jua. Hizo ndio zinafanya ngozi ya mtu kufifia. Lakini unapojisinga zinaondoka na ngozi yako inakuwa nyeupe sana.”

Baada ya kama nusu saa, kungwi huyo akaanza kunisinga, yaani kunisugua taka zangu za mwili kwa mikono kama vile ananifanyia masaji. Alinisugua mwili mzima pamoja na uso wangu. Kila aliponisugua, taka zilikuwa zinapukusika mwilini.

Alipomaliza alichukua kioo na kunipa.

“Jitazame mwenyewe ulivyotakasika,” akaniambia.

Nikajitazama.

Lo! Nilishangaa kweli kweli. Uso wangu ulikuwa mweupe na mng’avu kama niliyezaliwa sasa. Ndio mimi ni mweupe kama Mwarabu, rangi niliyoichukua kwa mama yangu, lakini baada ya kile nilichofanyiwa na kungwi, nilinoga zaidi.

“Hapo ukijipaka losheni yako isiyo na kemikali utapendeza sana,” akaniambia.

“Uzuri wa huu msio ni kuwa unakung’aza hapo hapo.”

“Sasa tukirudia tena kesho utapendeza sana.”

“Baada ya kesho inakuwa basi?”

“Itabaki ile siku utakayoondoka hapa. Sasa inuka uvae khanga nyingine.”

Nikainuka na kuchukua khanga nyingine na kujifunga.

“Umeshakula?” Akaniuliza.

“Nimeshakula nyumbani.”

“Sasa kaa hapo kitandani, tutakuwa tunalala pamoja hapo hapo.”

‘Panatosha.”

Kabla ya kulala yule mwanamke alinipeleka tena bafuni kwa mtindo ule ule wa kuniongoza mbele nikiwa nimezibwa uso wangu kwa kuteremshiwa ushungi.

Nilikuwa nimekwenda kujisaidia haja ndogo na pia kuoga ili kuondoa zile taka za msio zilizokuwa zimebaki mwilini mwangu.

Tuliporudi chumbani tulikaa kidogo kwenye kochi kabla ya kwenda kulala.

Wakati tumekaa aliniambia.

“Usafi ni kitu muhimu sana hasa katika maisha ya ndoa. Wakati wote unapomaliza kazi zako hakikisha unakwenda kuoga na kuwa msafi, jitie manukato ambayo mume wako anayependa. Mume wako akirudi kutoka kazini akukute una mvuto. Wanawake wengine wanajisahau, ni mpaka pale wanapotaka kutoka ndipo wanakumbuka kujiweka vizuri.”