Hadithi
HADITHI: Bomu Mkononi - 21

Muktasari:
- Binti mrembo cheupe, ambaye ukimwangalia unaweza kusema ni Mwarabu, anawavuruga wanaume kwa kuolewa na mume zaidi ya mmoja. Hili ni bomu mkononi...
“HAYO ni maneno ya kunishutumu mke wangu lakini kama unanifikiria hivyo sawa.”
“Na mimi nakwambia sawa.”
Ukawa mwisho wa maneno yetu. Hata hivyo, usiku ule nilijidai kukasirika, kila mmoja akalala ubavu wake.
Asubuhi kulipokucha mimi ndiye niliyeanza kumsemesha, nikajifanya yale ya jana sikuwa nayo tena. Lakini moyoni mwangu nilikuwa nayo kwamba mume wangu pia hakuwa mwaminifu.
Tulizungumza, tukanywa chai pamoja. Tilipomaliza kunywa chai Musa akanipa chupa mbili za pafyumu alizokuwa ameninunulia Burundi. Nilikuwa nimeziona tangu jana yake lakini kwa vile tulitupiana maneno ya shutuma hakuweza kunipa.
Nikamuuliza kama atakuja kula chakula cha mchana, akaniambia kuwa hakuwa na uhakika wa kurudi mchana.
“Lakini niwekee chakula, wakati wowote nitakaorudi nitakula,” aliniambia.
“Unapenda chakula gani?”
“Utakachopenda wewe kupika.”
“Sawa.”
Baada ya hapo Musa akaondoka.
Baada ya Musa kuondoka nikawasha simu yangu na kumpigia Mustafa.
“Mbona hupatikani kwenye simu?” Mustafa akaniuliza kwa ukali kidogo. Kabla sijamjibu aliongeza.
“Tangu jana nakupigia sikupati!”
“Si unajua mishe mishe za kwenye msiba. Simu ilikuwa mbali na mimi na niliamua kuizima ili nisisumbue watu. Nikajisahau kabisa.”
“Sasa mbona hukuniambia kama utalala huko?”
“Hukunielewa mume wangu, kwa vyovyote vile nisingeweza kurudi. Kwanza mazishi ni leo na leo pia naweza kulala na kurudi kesho.”
“Mh!” Mustafa akaguna lakini hakusema kitu, alinyamaza kimya.
“Kwani unanihitaji?’
“Hapana, kama umeamua kukaa mpaka kesho, sawa.”
“Nitafanyaje sasa, kama nilivyokwambia huyu mama ni kama mama yangu.”
“Usiwe na wasiwasi. Sijachukia. Nilikuwa sikukuelewa tu.”
“Basi nielewe mpenzi, tutaonana kesho.”
“Poa.”
“Ukiona nimezima simu usijali, nikiwasha nitakupigia.”
“Sawa.”
Baada ya kumpoza Mustafa nilizima tena simu. Musa alikuja saa kumi jioni. Alipokula alitoka tena. Alipotoka nikawasha simu na kumpigia Mustafa. Tulizungumza kidogo nikamdanganya kuwa tumeshazika.
“Lakini kama ulivyoniambia utakuja kesho?” Akaniuliza.
“Ndio. Kesho jioni.”
Kesho yake sikwenda kwa Mustafa kwa sababu Musa alikuwa hajaondoka. Nikamdanganya tena Mustafa kuwa watoto wa yule mama aliyekufa wameniomba nilale nao hadi kesho yake tena. Mustafa akakubali.
Kama nilivyokuwa nimepanga, kesho yake Musa akapata safari ya kwenda Burundi.
Aliondoka asubuhi akiwa hana habari ya safari, baadaye mchana alirudi akaniambia kuwa atakuwa na safari.
“Utaondoka saa ngapi? Nikamuuliza haraka.
“Nitaondoka usiku. Hivi sasa gari iko bandarini inapakia mzigo.”
“Hapa nyumbani utaondoka saa ngapi?”
“Nimekuja kuchukua begi langu, nikitoka ndio nimeondoka jumla. Sitarudi tena.”

“Poa,” nikajisemea.
Hivyo ndivyo nilivyokuwa nataka.
“Hutawahi kula chakula?” Nikajidai kumuuliza.
“Kwani umeshapika?”
“Ndio ninapika.”
“Sitakisubiri, acha niende. Nitakula huko huko.”
“Hao matajiri zenu wanapenda kuwapa taarifa za ghafla sana. Ilitakiwa wakwambie mapema kuwa utakuwa na safari.”
“Ndio kazi zetu zilivyo. Tumeshazoea.”
“Poa. Safari njema.”
Musa alichukua begi lake akatia vitu alivyovitaka kisha akaniaga. Wakati anatoka nikamuuliza.
“Kondomu zako huzihitaji tena?’
Musa aligeuka mara moja akanitazama.
“We acha mzaha wako,” akaniambia kisha akageuka na kutoka.
Nilisimama kunako mlango nikamtazama alivyokuwa akitembea kuelekea kwenye kituo cha daladala. Wakati namtazama mawazo ya Mustafa yakaanza kunijia.
Nikarudi ndani na kufunga mlango. Niliketi kwenye sebule nikajiambia kuwa sitapika tena. Nitakwenda kupika kwa Mustafa.
Nilisubiri zipite saa mbili nikatia baadhi ya vitu vyangu kwenye mkoba wangu kisha nikatoka. Sikuchukua nguo. Nilikwishahamishia kwa Mustafa baadhi ya nguo zangu na viatu. Nilichukua vitu vidogo vidogo tu ambavyo Mustafa asingeweza kuvizingatia.
Kabla ya kwenda Mbezi nilipitia sokoni nikanunua vitu ambavyo nilihitaji kupika. Nilipofika Mbezi Mustafa alikuwa hayupo. Kwa vile nilikuwa na funguo zangu nikafungua mlango na kuingia ndani.
Niliingia chumbani nikabadili nguo kisha nikazima simu yangu na kuiweka kwenye chaji ili Mustafa akija aone simu iko kwenye chaji. Sikutaka anipigie wala sikutaka Musa anipigie.
Baadaye nikatoka chumbani na kuelekea jikoni na kuanza kupika.
Yalikuwa mida ya saa kumi na moja Mustafa aliporudi nyumbani na kunikuta nimeketi sebuleni nikiangalia filamu ya Kihindi.
“Mbona hukunifahamisha kama umeshakuja?” Akaniuliza.
“Kwani ulitaka kuleta msichana wako?”
“Mishi acha mzaha wako, una ‘surprise’ za ajabu sana. Halafu nilikupigia ukawa hupatikani.”
“Simu ilikuwa kwenye chaji. Mimi mwenyewe nilikuwa jikoni napika.”
“Kwani ulikuja saa ngapi?”
“Tangu saa sita niko hapa.”
Nilimdanganya. Muda niliofika, saa sita ilikuwa imeshapita.
“Umepika nini?”
“Nimepika wali na nyama.”
Nilipomwambia hivyo Mustafa aliinuka na kuelekea chumbani. Baadaye alirudi tena sebuleni akiwa amevaa saruni. Alionekana alikuwa anatoka kuoga.
Tukaendelea na mazungumzo.
Kabla ya mwezi mmoja kukamilika Mustafa akaenda India. Alipoondoka tu nikarudi kwa Musa. Musa aliporudi kutoka Burundi alinikuta nipo nyumbani.
Kwa vile safari zake nyingi zilikuwa za Burundi, alipoondoka tena kwenda Burundi nikahamia Mbezi kwa Mustafa. Mustafa alikaa India kwa wiki nzima. Aliporudi alinikuta nipo nyumbani kwake.
Baada ya mwezi mmoja nikajikuta nina mimba. Sikujua ile mimba ilikuwa ni ya nani lakini nilikisia kuwa ilikuwa ya Mustafa. Nikaitambulisha mimba yangu kwa waume wote wawili. Kila mmoja akajua nina mimba na mimba ni yake.
Kwa vile waume wangu wote wawili walikuwa wakisafiri nje ya nchi na wakiwa huko hukaa kwa zaidi ya wiki. Niliendelea kutumia mtindo uleule wa kuhamia kwa mwanaume mmoja pindi mwenzake anaposafiri.
Kwa bahati njema walikuwa wakisafiri kwa nyakati tofauti hivyo kuniwezesha mimi kuweza kuwa kwa mwanaume mmoja pale mwenzake anapokuwa hayupo.
Ile mimba iliendelea hadi ikatimiza miezi tisa. Hakukuwa na mwanaume wangu yeyote aliyegundua kuwa mimba hiyo ilikuwa ya watu wawili.
Kuna siku Mustafa alikuwa amekwenda China kununua bidhaa. Lakini Musa alikuwapo na nilikuwa nyumbani kwake. Musa akaniambia kwamba anataka asafiri lakini anasita kwa sababu naweza kuumwa na uchungu wakati wowote na nitakuwa peke yangu.
Wakati akiniambia hivyo Mustafa alishanipigia simu kunijulisha kuwa anarudi kesho yake.
Nikamwambia Musa kuwa anaweza kwenda safari.
“Mimi nitakwenda kwa shangazi.”
“Shangazi ataweza kukuhudumia?” Akaniuliza.
“Kwanini asiweze. Yeye mwenyewe ameniambia niende.”
“Kama ameshakwambia basi unaweza kwenda, acha mimi niende safari.”
Siku ile Musa akaondoka. Sikwenda kwa shangazi. Musa alipoondoka nikaenda Mbezi kwa Mustafa.
Mustafa alirudi siku iliyofuata na siku hiyo hiyo nikaumwa na uchungu. Mustafa akaniwahisha hospitalini kwa gari lake. Nikajifungua usiku mtoto wa kiume. Alikuwa amefanana sana na Mustafa.
Mustafa alikuja hospitalini asubuhi akamkuta mtoto ameshazaliwa. Akampa jina hapo hapo.
“Mwanangu ataitwa Amani,” akaniambia.
Nikatabasamu na kumuuliza.
“Umempa jina la nani wako?”
“Ni jina la babu yangu mzaa mama yangu,” akaniambia.
Kwa vile nilikuwa na afya njema na mwanangu alikuwa na afya njema nikaruhusiwa kutoka hospitalii asubuhi ile ile. Nikarudi Mbezi.
Shangazi yangu alikuwa hajui kama nilikuwa nimejifungua na sikutaka ajue haraka. Pia sikumfahamisha lolote Musa ingawa namba aliyokuwa anaitumia Burundi nilikuwa nayo.
Mustafa aliniletea mfanyakazi wa kunisaidia kazi ili mimi niweze kumlea yule mtoto. Nikajiambia ili niweze kutekeleza mambo yangu vizuri nijenge uhusiano wa kirafiki na yule msichana ili anapogundua siri zangu asimueleze Mustafa.
Nilimpa baadhi ya nguo zangu za thamani. Pia nikawa nampa siri zangu ndogo ndogo na kumsisitiza kwamba asiwe anamueleza Mustafa maneno yetu.
Yule dada wa kazi ingawa hakutambua dhamiri yangu kiundani alinielewa. Tukawa marafiki sana.
Mustafa alipohakikisha kuwa nilikuwa na mtumishi wa kunisaidia akaanzisha tena safari zake za nje ya nchi ambazo alikuwa amezisimisha kwa muda.
Siku ile alipoondoka na mimi niliondoka kwenda kwa shangazi lakini mtumishi nilimuacha nyumbani kwa Mustafa. Nilimdanganya kwamba mama yangu aliyekuwa akiishi Ilala alikuwa mgonjwa hivyo nilikuwa nakwenda kumjulia hali na kwamba nitakuwa huko kwa wiki nzima.
Inaendelea...