Mahakama yamuamuru Harmonize kuilipa CRDB Sh113 milioni

Msanii wa muziki wa Bongofleva, Rajab Abdukahali Ibrahim, maarufu Harmonize
Muktasari:
- Benki ya CRDB ilimfungulia kesi ya madai Harmonize baada ya kushindwa kurejesha kwa ukamilifu deni la mkopo wa Sh300 milioni. Mahakama Kuu imemuamuru Harmonize kulipa deni lililokuwa limesalia pamoja na fidia na riba baada ya CRDB kushinda kesi hiyo.
Dar es Salaam. Mahakama Kuu Divisheni ya Biashara imemuamuru msanii wa muziki wa Bongofleva, Rajab Abdukahali Ibrahim, maarufu Harmonize kuilipa Benki ya CRDB Sh113 milioni, zikiwa ni sehemu ya deni la mkopo anaodaiwa pamoja fidia.
Mahakama hiyo imetoa amri hiyo katika hukumu yake ya kesi ya madai iliyofunguliwa na benki hiyo baada ya msanii huyo kushindwa kurejesha deni la mkopo wa Sh300 milioni aliouchukua mwaka 2019.
Hukumu hiyo imetolewa Agosti 2, 2024 na Jaji Cleophas Morris aliyeisikiliza kesi hiyo baada ya benki hiyo kushinda.
Katika hukumu hiyo Mahakama imemuamuru Harmonize kuilipa benki hiyo Sh103.18 milioni ambazo ni sehemu ya deni la mkopo lililosalia na Sh10 milioni zikiwa ni fidia ya hasara ya jumla iliyoipata benki hiyo, kwa kitendo cha Harmonize kushindwa kumaliza kulipa deni hilo.
Pia Mahakama hiyo imemuamuru Harmonize kulipa riba ya asilimia 18 ya kiasi hicho cha deni lililosalia kwa mwaka kuanzia tarehe aliyoshindwa kuilipa (kwa mujibu wa makubaliano) mpaka tarehe ya hukumu hiyo.
Vilevile Mahakama hiyo imemuamuru kulipa riba ya asilimia saba kwa mwaka, ya jumla ya kiasi alichoamuriwa kulipa, kuanzia tarehe ya hukumu hiyo mpaka tarehe ya kukamilisha malipo yote pamoja na gharama za kesi hiyo.
Kesi hiyo ya kibiashara namba 151 ya mwaka 2023 ilisikilizwa na kuamuriwa upande mmoja baada ya Harmonize kupuuza wito wa mahakama kuwasilisha utetezi wake wa maandishi wala kufika mahakamani kujitetea kwa mdomo wakati wa usikilizwaji wa kesi hiyo, licha ya kupelekwa hati za wito mara nne kwa nyakati tofauti.
Kwa mujibu wa hukumu hiyo, kesi hiyo ilifunguliwa Desemba 6, 2023 na Desemba 8, 2023 na Desemba 14, 2023 Mahakama hiyo ilitoa hati ya wito kwa Harmonize kuwasilisha maelezo yake ya utetezi na nyaraka ambazo angezitumia katika utetezi wake, lakini hakutekeleza.
Kufuatia maombi ya Wakili wa mdai (CRDB) Februari 28, 2024, Mahakama hiyo ilitoa amri ya kupelekwa wito mwingine kwa Harmonize na Machi 4, 2024 Mahakama hiyo ilitoa hati nyingine ya wito.
Hata hivyo, hati hiyo ya wito ilirejeshwa mahakamani bila kusainiwa baada ya msanii huyo kukataa kuipokea alipopelekewa Machi 6, 2024.
Kwa mara nyingine Mahakama hiyo ikielekeza benki hiyo imfikishie msanii huyo wito mwingine kwa njia ya tangazo la gazetini kupitia gazeti la Mwananchi na ingawa tangazo hilo lilitoka toleo la Mwananchi la Aprili 19 bado msanii huyo alipuuza wito.
Hivyo Wakili wa CRDB, Fredrick Mpanju aliiomba Mahakama nayo iridhie kuendelea na usikilizwaji wa kesi hiyo upande mmoja bila mdaiwa kuwepo, kwa mujibu wa Amri ya VIII Kanuni ya 14 ya Kanuni za Mwenendo wa Mashauri ya Madai.
Kwa mujibu wa hukumu hiyo, CRDB ilimpatia Harmonize mkopo huo wa Sh300 milioni Oktoba 10, 2019, kwa ajili ya msanii huyo kununulia vifaa vya muziki, kuanzisha studio ya uzalishaji muziki, uzalishaji na utangazaji wa muziki wake.
Mkopo huo ulipaswa kurejesha pamoja na riba yake ya asilimia 18 kwa mwaka, ndani ya miezi 36 (miaka mitatu) na mkopaji, Harmonize alitakiwa kufungua akaunti ya benki katika benki hiyo ambayo pia angezitumia kwa mapato yatokanayo na shughuli zake za muziki.
Hata hivyo, benki hiyo ilidai msanii huyo licha ya kwamba hakutekeleza masharti hayo ya mkopo pia alishindwa kurejesha mkopo huo kikamilifu.
Katika ushahidi wake benki hiyo pamoja na mambo mengine ilieleza baada ya kumwandikia taarifa ya kumkumbusha msanii huyo aliandika barua kwa meneja wa tawi huku akiomba kiasi cha marejesho ya mkopo huo kwa mwezi kipunguzwe kutoka zaidi ya Sh10.8 milioni mpaka Sh3.3 milioni.
Hata hivyo, lisha ya kumkubalia ombi hilo hakuweza kulipa mkopo wote kwa muda waliokubaliana na kwamba mpaka wanafungua kesi alikuwa anadaiwa Sh103.185 milioni kama deni la msingi.
Mahakama baada ya kusikiliza ushahidi wa mdai pamoja na vielelezo mbalimbali vilivyowasilishwa mahakamani, katika uamuzi wake iliridhika kuwa mdai ameweza kuthibitisha madai yake kwa kiwango kinachotakiwa kisheria katika kesi ya madai.
"Kwa hiyo kutokana na uchunguzi na uchambuzi hapo juu ni mtizamo wa Mahakama hii kwamba kiapo cha mdai kimethibitisha madai kwa kiwango kilichoelezwa hapo juu," amesema Jaji Morris katika hukumu hiyo baada ya kuchambua ushahidi wa mdai na kisha kutoa amri hizo dhidi ya mdaiwa.