Kajala hataki kabisa mambo ya Harmonize

Muktasari:
- Kajala alivunja ukimya huo aliponaswa na Mwanaspoti na kuchomokewa swali juu ya uvumi wa kurudisha majeshi kwa Harmonize na kusema kama kuna kitu asichokipenda kusikia kwa sasa anapohojiwa ni kuuliza ishu za staa huyo wa muziki wa kizazi kipya nchini.
MWIGIZAJI Kajala Masanja ameweka wazi hisia alizonazo kwa kusema hapendi kufanyiwa mahojiano na kuulizwa ishu za mpenzi wake wa zamani, Harmonize anayedaiwa kwa sasa wamerudiana kimyakimya.
Kajala alivunja ukimya huo aliponaswa na Mwanaspoti na kuchomokewa swali juu ya uvumi wa kurudisha majeshi kwa Harmonize na kusema kama kuna kitu asichokipenda kusikia kwa sasa anapohojiwa ni kuuliza ishu za staa huyo wa muziki wa kizazi kipya nchini.
Bibie huyo alisema huwa anakwazika kumzungumzia mtu ambaye hayupo pamoja kwa sasa na kusema hajui ni kwanini kila anayemhoji ni lazima amchomekee swali hilo, ilihali wao kwa sasa ni zilipendwa baada ya kutemana muda mrefu uliopita.
"Jamani, jamani...kuna mambo mengi sana ya kuzungumza katika mahojiano au kwa watu ambayo yatakuza kazi zake zangu za sanaa, na sio kila kukicha ni habari tu za mambo yaliyopita, sipendi kweli, yaani utakuta ukiamka asubuhi unakutana na simu nyingi za watu mbalimbali au meseji nyingi kuhusu swali hilo hilo," alisema Kajala na kuongeza; "Itoshe kusema haya mambo nisiulizwe tena jamani, hii naongea kwa watu wangu wote wa karibu na media zote huu ujumbe uwafikie, kwamba mimi na Harmonize ni zilipendwa na kila mtu ana ishu zake kwa sasa, hii habari ya kuulizwa kila uchao ni kupotezeana muda na kutibuliana mudi tu."
Hivi karibuni kulikuwa na tetesi kwamba, Kajala na Harmonize wamerudiana kimapenzi na kuishi pamoja kama zamani, ikidaiwa ni baada ya Konde Boy kuwekewa masharti makubwa na Kajala na kuyakubali. Hata hivyo, wiki iliyoisha Harmonize alifanya mkutano na waandishi na kuruka kimanga jambo hilo, japo alikiri wanapiga stori tu kwa sasa.