20 Percent-Ninajua ninachokifanya

20 Percent-Ninajua ninachokifanya

Muktasari:

  • Msanii wa muziki wa kizazi kipya, 20 Percent amesema utendaji kazi wake unazingatia ni ujumbe gani anaupeleka kwenye mioyo ya jamii anayoilenga na si kutengeneza bora kazi ili mradi  tu azungumziwe midomoni mwa mashabiki wake. 

Msanii wa muziki wa kizazi kipya, 20 Percent amesema utendaji kazi wake unazingatia ni ujumbe gani anaupeleka kwenye mioyo ya jamii anayoilenga na si kutengeneza bora kazi ili mradi  tu azungumziwe midomoni mwa mashabiki wake. 
Msanii huyo anatamba na kibao cha Nipeleke kwa Mama  kinachozungumzia baba anayepambana kumuuguza mtoto wake, huku akiwa hana kazi na mama mwenye nyumba anamsumbua kodi ya nyumba, kisha mwanae anaaga dunia.  
20 Percent Ameliambia Mwanaspoti online, leo Jumatano ya Aprili 7, 2021 kwamba anatamani nyimbo zake ziguse jamii na sio kusikiliza mzuka wa mdundo kisha baada ya wiki zinasahaulika, badala yake anapenda ziishi muda mrefu kwenye jamii, zikiwa na mafunzo.
Amesema hana wasiwasi wa kupitwa sokoni kutokana na kutoachia nyimbo zake mara kwa mara kwani anachokizingatia zaidi ni uimbaji wake utakaoacha alama ya mafunzo kwa vizazi na vizazi vitakavyokuja baadae.
"Aina ya muziki ninaoufanya ni ule wenye ujumbe unaoihusu jamii, nazingatia kutatua, kuonyesha kero, kukosoa na kuburudisha, lengo mtu yoyote atakayesikiliza anakuwa anapata kitu kinachomstahili na ndio maana nyimbo zangu zinaishi,"  
"Nyimbo zangu zingelenga kuburudisha tu, zingekuwa zimeishasahaulika, lakini hadi sasa zikipigwa ama mimi mwenyewe nikiziimba mikoani naona jinsi ambavyo zinapata kibali kikubwa kutoka kwa mashabiki wangu,"amesema  20 Percent