Van Dijk ajibakiza Anfield

Muktasari:

  • Beki huyo Mdachi amebakiza mwaka mmoja kwenye mkataba wake jambo lililoibua hofu kubwa huenda akaungana na Kocha Jurgen Klopp katika kuelekea mlango uliondikwa ‘exit’ huko Anfield mwisho wa msimu.

LIVERPOOL, ENGLAND: Beki ghali, Virgil van Dijk amesema bado hajafahamu hatima ya mkataba wake huko Anfield, lakini anaamini atakuwa sehemu ya Liverpool mpya inayokwenda kujengwa msimu ujao.

Beki huyo Mdachi amebakiza mwaka mmoja kwenye mkataba wake jambo lililoibua hofu kubwa huenda akaungana na Kocha Jurgen Klopp katika kuelekea mlango uliondikwa ‘exit’ huko Anfield mwisho wa msimu.

Van Dijk, 32, alisema kwa msisitizo anavutiwa mabadiliko ya kumleta Mdachi mwenzake, Arne Slot kuja kurithi mikoba ya Klopp.

Michael Edwards amarejea pia kwenye klabu hiyo sambamba na Richard Hughes, ambaye amekuja kuwa mkurugenzi wa michezo kuanzia msimu ujao.

Van Dijk alisema: “Hatupo kimya kwa sababu tunafahamu mambo yanatokea, lakini kwa kipindi uamuzi bado haujafikiwa juu ya kocha mpya. Tunajua mambo mengine, Michael Edwards amerudi, Richard Hughes atakuja kuwa mkurugenzi wa michezo, hao ndio uamuzi uliofanyika hadi sasa. Zaidi ya hicho, tusubiri tuone.

“Lakini, nina imani na klabu inakwenda kwenye njia sahihi. Kuna mabadiliko makubwa yanakwenda kutokea na hakika navutiwa na kinachotokea kwa sasa. Ngoja tusubiri na kuona.”

Van Dijk aliulizwa kama ameshapewa ofa ya mkataba mpya baada ya Liverpool kuichapa Tottenham Hotspur mabao 4-2 kwenye mchezo wa Ligi Kuu England, Jumapili iliyopita.

Alisema: “Nadhani hakuna kitu cha kujadili kuhusu mimi, nadhani klabu iko bize sana kupambana na kocha mpya na hicho ndicho kipaumbele. Kama nilivyosema, nina furaha kuwa hapa, naipenda hii klabu na hilo linaonekana wazi.”