Mashabiki wamzomea Ten Hag

MANCHESTER, ENGLAND. MASHABIKI wa Manchester United walimzomea kocha wao Erik ten Hag baada ya kuamuru straika wa timu hiyo, Rasmus Hojlund atolewe nje katika mchezo dhidi ya Burnley.

Rasmus alitolewa kipindi cha pili dakika ya 65 wakati ubao ukiwa unasoma ni 0-0 na mbali ya yeye pia Kobbie Mainoo alitolewa na nafasi yake ikachukuliwa na Scott McTominay.

Kwa sasa Rasmus ndio mfungaji bora namba mbili wa Man United kwa msimu huu akiwa na mabao 14 nyuma ya Bruno Ferndandes mwenye mabao 15 na Mainoo anashika nafasi ya tatu kwa mabao yake 10.

Sauti kali za kuzomea zilisikika majukwaani wakati Hojlund anafanyiwa mabadiliko ikiwa ni ishara ya kwamba mashabiki hawakukubaliana na kutolewa na straika huyo wa Denmark.

Nafasi ya Hojlund ilichukuliwa na Amad Diallo ambaye kuingia kwake kuliongeza chachu ya mashambulizi kwenye eneo la ushambuliaji ambapo dakika 15 baadaye Man United ilipata bao kupitia Antony, ingawa Burnley ilisawazisha baadaye kwa penalti iliyopigwa na Zeki Amdouni.

Mbali ya mashabiki waliozomea uwanjani, wengine pia walitumia mitandao ya kijamii kumshambulia kocha huyo.
Kupitia Twitter mmoja kati ya mashabiki alisema: "Unahitaji goli halafu unamtoa straika, hii inaingia akilini? Kutolewa kwa Hojlund limekuwa ni janga."

Sare hiyo imezidi kufuta matumaini ya Man United kufuzu michuano ya Ulaya mwakani kwani inashika nafasi ya sita ikiwa na pointi 54 baada ya kucheza mechi 34.