Hiyo UEFA ni uongo mtupu, mwamuzi aomba radhi

Muktasari:

  • Mbali ya mashabiki hao, Kocha wa Bayern Thomas Tuchel naye pia alisema uamuzi wa mechi yao ilikuwa ni janga na tofauti kabisa na sheria za soka.

MADRID, HISPANIA: Mashabiki wa soka Ulaya wamekasirishwa na waamuzi wa mechi za nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa barani humo na kudai mechi zote zimepangwa baada ya Bayern Munich kukataliwa bao lao la kusawazisha dhidi ya Real Madrid.

Mbali ya mashabiki hao, Kocha wa Bayern Thomas Tuchel naye pia alisema uamuzi wa mechi yao ilikuwa ni janga na tofauti kabisa na sheria za soka.

Katika mchezo huo wa jana Bayern ndio ilikuwa ya kwanza kufunga bao kupitia kwa Alphonso Davies dakika ya 68 na kufanya ubao usome 3-2 kwa matokeo ya jumla baada ya ule mchezo wa mkondo wa kwanza kumalizika kwa sare ya mabao 2-2.

Madrid ilisawazisha na kuongeza lingine kupitia kwa staa wao Joselu dakika ya 88 na 90+1 ambapo ubao ukawa ni 4-3 kwa matokeo ya jumla, lakini Bayern wakapata bao la pili na la nne kwa matokeo ya jumla kupitia beki wao wa kati  Matthijs de Ligt lakini lilikataliwa na kuambiwa kwamba kuna mchezaji aliotea.

Mastaa wa Bayern waliokuwa uwanjani wakaanza kuwafuata waamuzi wa mchezo kuanzia yule wa kati Szymon Marciniak na mshika kibendera namba moja wakitaka wapitie katika VAR kabla ya mchezo kuendelea lakini hilo halikufanyika.

Mmoja kati ya wachezaji hao alikuwa ni Harry Kane  ambaye alionekana kujibizana na waamuzi akiamini hakukuwa na tukio la kuotea.

Baada ya mechi hiyo kocha wa Bayern, Tuchel alisema: "Tumefunga bao moja lakini kulikuwa na makosa makubwa katika maamuzi ya mwamuzi wa kati na mshika kibendera ni kama kulikuwa na usaliti mwishoni.

"Mshika kibendera alisema samahani lakini hiyo haiwezi kusaidia chochote, sijui ilikuwaje akanyanyua kibendera kwa mazingira yale, mwamuzi naye aliona nafikiria ni moja kati ya maamuzi mabovu sana kuwahi kutokea, ni kinyume na sheria ni ngumu sana kulimezea mate lakini ndio limeshatokea."

Kwa upande wake staa aliyefunga bao hilo, beki De Ligt aliiambia tovuti ya Movistar: "Sitaki kusema kwamba Real Madrid huwa wanabebwa na mwamuzi kila siku lakini hicho ndio kimeamua mchezo, Real unapoona wamekufa ujue watapindua tena ndio maana wana makombe 14 ya Ligi ya Mabingwa, mshika kibendera alikuja akaniambia samahani kwamba amefanya kosa kukataa bao langu."

Wakati tukio hili likitokea huko mitandaoni mashabiki nao walitoa yao ya moyoni ambapo mmoja kupitia Twitter ama X, alisema michuano hii tayari imeshapangwa, mchezaji hakuotea pale, kwanini mwamuzi anyanyue kibendera haraka wakati kuna VAR, hii ni michuano mingine ya Ligi ya Mabingwa ambayo Madrid imepangwa ichukue.

Mbali ya mashabiki, mchezaji wa zamani wa Manchester United Paul Scholes ambaye kwa sasa ni mchambuzi alisema hana uhakika kama kulikuwa na tukio la kuotea lakini mwamuzi alikuwa na haraka sana, alitakiwa atulie na kusubiri ajiridhishe, hiyo ndio sheria ilivyo.