El Clasico imembakiza Xavi kazini, moto unawaka

Muktasari:

  • Hilo limepita, lakini madhara ya kichapo kwa Barcelona yaliwafanya waachwe pointi 11 kuwania ubingwa wa La Liga.

MADRID HISPANIA: Ile El Classico haijachosha watu. Kiungo wa England, Jude Bellingham alikuwa steringi iliyopigwa Bernabeu, ambapo Los Blancos ilishinda 3-2, huku Barcelona ikilalamikia bao lao kukataliwa.

Hilo limepita, lakini madhara ya kichapo kwa Barcelona yaliwafanya waachwe pointi 11 kuwania ubingwa wa La Liga.

Wikiendi hii mchakamchaka uliendelea, ambapo jana Ijumaa vinara Real Madrid ilikuwa ugenini kukabiliana na Real Sociedad.

Ushindi wa Real Madrid kwenye mechi hiyo utawafanya kuweka pengo la pointi kufikia 14 na kujisogeza karibu na ubingwa unaoshikwa na Barcelona. Baada ya mchezo wa jana, Real Madrid imebakiza mechi tano kukamilisha msimu huu huku pengo la pointi likiwafanya kuishi bila ya presha. Barcelona, ambayo yenyewe inafurahia taarifa kuhusu kocha Xavi kutangaza atabaki kwenye kikosi hicho, kitashuka uwanjani Jumatatu kitakapokuwa nyumbani kucheza na Valencia. Kikosi cha Xavi kilionyesha kiwango bora kwenye El Clasico na bila shaka kitakuwa kwenye ubora ili kukusanya pointi zitakazozidi kuipa presha Real Madrid kwenye mbio za kufukuzia ubingwa wa La Liga. Xavi alitangaza kubaki akidai kuna mambo hajayakamilisha kwenye kikosi hicho. Mchakamchaka huo wa La Liga utaendelea leo Jumamosi, ambapo Las Palmas itakuwa nyumbani kucheza na Girona inayosaka nafasi ya kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao. Girona inapambana kwamba haitoki kwenye timu nne za juu ili kukamatia tiketi ya kucheza michuano ya Ulaya msimu ujao.

Almeria itaonyeshana kazi na Getafe. Ikiwa imeshinda mechi moja kati ya tano za mwisho, Getafe ilijikuta ikiporomoka na kujiweka kwenye kundi la timu zinaweza kushuka daraja, hivyo itahitaji nguvu zote ili kuweka hai matumaini ya kubaki kwenye ligi.

Kasheshe jingine litahusu kipute cha Alaves na Celta Vigo. Kwenye mchezo uliopita, Celta Vigo ilitoka nyuma na kuichapa Las Palmas 4-1 ili kujiweka mbali na shimo la kushuka daraja. Mchezo wa mwisho kwa leo Jumamosi, utakuwa huko Wanda Metropolitano, ambako Atletico Madrid itakipiga na Athletic Club. Hilo ni bonge la mechi kutokana na timu hizo kupambana kuwania nafasi ya kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya, ambapo timu moja ipo kwenye nafasi ya nne, Atletico na nyingine ipo kwenye namba tano.

Kecho Jumapili kazi itakuwa huko Cadiz wakati itakapokuwa nyumbani kucheza na Mallorca. Katika mchezo huo timu zote zinahitaji pointi, huku Mallorca ikiwa na safu bora ya mabeki tangu mwaka huu ulipoanza jambo ambalo litaiweka Cadiz kwenye wakati mgumu.

Granada itakuwa na kazi nzito mbele ya Osasuna. Granada mambo yao yalikuwa hovyo kabla ya kuambulia pointi kwenye mechi dhidi ya Bilbao na sasa wanaamini watakuwa kwenye kiwango hicho kizuri wakikabiliana na Osasuna.

Villarreal itaulizana maswali na Rayo Vallecano. Katika mechi tano zilizopita, Villarreal imepoteza moja tu jambo linalowafanya kuwa kwenye wakati mzuri na huenda wakatumia fursa ya kuwa nyumbani kupata ushindi dhidi ya Rayo, huku Real Betis yenyewe ikiwa na shughuli pevu mbele ya Sevilla.