Simba yaipiga Azam, Fei akosa penalti

Muktasari:

  • Mgunda ameingoza Simba kuvuna pointi 10 katika michezo minne iliyopita kwa kutoa sare moja dhidi ya Namungo na kushinda tatu mfululizo bila ya kuruhusu bao mbele  ya Mtibwa Sugar, Tabora United na Azam

WEKUNDU wa Msimbazi, Simba SC wameendeleza moto wao wakiwa chini ya Kaimu Kocha Mkuu, Juma Mgunda kufuatia kuibuka na ushindi wa tatu mfululizo katika mchezo wa vita ya nafasi dhidi ya Azam ambapo imeshinda kwa mabao 3-0 mchezo uliochezwa kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa.

Mabao ya Sadio Kanoute dakika ya 63,  Fabrice Ngoma dakika ya 77 na David Kameta 'Duchu' dakika ya 89, yametosha kwa vijana hao wa Mgunda kuvuna ponti tatu muhimu ambazo zimewafanya kuweka hai matumaini yao ya kumaliza msimu katika nafasi mbili za juu.

Kabla ya mchezo huo, Simba ambayo ipo nafasi ya tatu ilikuwa nyuma ya Azam FC kwa tofauti ya pointi nne hivyo ushindi huo umewafanya kuwa na pointi 56 na sasa wapo nyuma kwa pointi moja tu huku wakiwa na mchezo mmoja mkononi.

Simba na Azam ni kama waligawana vipindi katika mchezo huo. Azam ilikuwa bora sana katika kipindi cha kwanza kwa kufanya mashambulizi mfululizo kupitia maeneo yake ya pembeni ambako walicheza Gibril Sillah na Idd Seleman 'Nado'.

Dakika ya 35, Azam ilipata penalti baada ya Sillah kuangushwa na Che Malone Fondoh katika eneo la hatari hata hivyo walishindwa kuitumia.

Mkwaju wa Feisal Salum uligonga nguzo na mpira kurejea uwanjani huku ikizifanya timu hizo kwenda mapumziko zikiwa suluhu kabla ya kibao kugeuka katika kipindi cha pili kwa vijana wa Mgunda kutandaza kandanda la kuvutia zaidi.

Katika kipindi hicho cha pili ubora wa eneo la kati la Simba uliibeba timu hiyo, Ngoma, Kanoute na Mzamiru walifanya kazi kubwa ya kuzuia na kushambulia na matunda yake yakaonekana.

Kipigo cha Azam kinamaana kuwa Yanga imerahisishiwa kazi na Simba katika mbio za ubingwa kwani kwa sasa wanahitaji pointi nne tu badala ya tano kutwaa ubingwa huo.

Yanga yenye pointi 68, katika mechi nne zilizobaki ikifikisha 72 basi itatangaza ubingwa kwani Azam hata ikishinda mechi zote nne itaishia pointi 69, huku Simba katika mechi sita zilizobaki ikipata ushindi zote itamaliza na pointi 71.


VIKOSI

Azam FC; Mohammed Mustafa, Nathaniel Chilambo, Pascal Msindo, Yannick Bangala, Yeison Fuentes, James Akaminko, Gibril Sillah, Yahya Zayd, Kipre Junior, Feisal Salum 'Fei Toto', Idd Seleman 'Nado'.

Simba; Ayoub Lakred, Israel Mwenda, Mohammed Hussein 'Tshabalala', Che Malone, Kennedy Juma, Fabrice Ngoma, Ladack Chasambi, Sadio Kanoute, Freddy Michael, Mzamiru Yassin na Edwin Balua.