Pembe: Simba wasipofunga mlango, zile 5 zinarudi

Wachekeshaji Pembe (kulia) akiwa na mwenzake Senga (kushoto) wakiwa katika moja ya majukumu yao. Wasanii hao ni miongoni mwa mashabiki wa Yanga

Muktasari:

  • Nyota wa vichekesho, Pembe na mwenzake Senga ni miongoni mwa wasanii waliodumu kwa muda mrefu katika kundi moja la uchekeshaji wakiwa wakereketwa wa Yanga.

MSANII wa vichekesho nchini, Yusuph Kaimu 'Pembe' amesema pamoja na matumaini waliyonayo mashabiki wa Yanga kushinda, lakini mastaa wanapaswa kuiheshimu Simba kwani mechi ya watani siyo kujihakikishia pointi tatu, japo akaonya: "Simba wasipofunga mlango vizuri zile tano zinarudi.".

Kauli ya msanii huyo inakuja ikiwa imebaki siku moja kushuhuhudia mchezo wa watani wa jadi kati ya Yanga na Simba, utakaopigwa Jumamosi hii kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa Dar es Salaam.

Hadi sasa mashabiki wa Yanga wanaonyesha matumaini ya timu hiyo kuweza kushinda mpambano huo kutokana na matokeo mazuri waliyonayo kwa sasa wakiwa kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu kwa pointi 55.

Pia mchezo wa mwisho kuwakutanisha vigogo hao Simba walikumbana na kisago cha mabao 5-1 huku wakiwa wametoka kuondoshwa kwenye Kombe la Shirikisho dhidi ya Mashujaa kwa penalti 6-5 siku chache zilizopita.

Pembe ambaye ni shabiki kindakindaki wa Yanga amesema wanayo matumaini ya ushindi, lakini kwa mchezo wa 'dabi' hawawezi kujipa asilimia zote kuondoka na alama tatu.

Amesema mashabiki wa Yanga wanapaswa kuiombea timu hiyo iendeleze ushindi ili kufikia malengo ya kutetea ubingwa, lakini wakati huo wachezaji wasiwabeze wapinzani.

"Sisi Yanga hadi sasa tuna asilimia 80 za ushindi, 20 zinabaki kwenye dakika 90, ile ni 'dabi' wachezaji wasibweteke kuwadharau Simba hata kama tunawazidi kila kitu."

"Yanga haimtegemei mchezaji mmoja uwanjani, isipokuwa yeyote anaweza kumaliza mchezo muda wowote, zile 5 tulizowapiga tunaona zinaweza kujirudia wasipofunga mlango vizuri," amesema mvunja mbavu huyo.

Mchekeshaji huyo maarufu nchini, ameongeza kuwa mechi hiyo wanatarajia ushindi wake utawaweka katika njia nzuri za kutetea taji lao kwa msimu wa tatu mfululizo akiwaomba mashabiki kujitokeza kwa wingi kuishangilia timu hiyo.