Lusajo: Profesa shabiki wa Simba alinikazia nisijiunge Yanga

Muktasari:

  • Katika mahojiano na Mwanaspoti, straika huyo ambaye anasema hupenda kuzurura pindi Ligi Kuu Bara inaposimama na siyo mtu anayepania kusoma isipokuwa ana akili za kuzaliwa akiamua kuweka mkazo katika kitabu, basi hakuna kinachoshindikana.

Mshambuliaji Reliants Lusajo anajipambanua kuandaa maisha baada ya kustaafu soka, jambo linalomfanya aipe elimu kipaumbele ili kumwezesha kufanya shughuli nyingine kwa urahisi.

Katika mahojiano na Mwanaspoti, straika huyo ambaye anasema hupenda kuzurura pindi Ligi Kuu Bara inaposimama na siyo mtu anayepania kusoma isipokuwa ana akili za kuzaliwa akiamua kuweka mkazo katika kitabu, basi hakuna kinachoshindikana.

“Usinione hivi kama mpole ligi inaposimama napenda kuingiza vitu vipya kichwani. Nina marafiki wengi utanikuta Arusha, Moshi ili mradi tu nimezurura huku na kule, hivyo siyo mtu wa kupanga ama kupania kusoma. Nikielewa tu ninachotaka kukifanya, basi mambo yanakwenda sawa,” anasema.

KISA YANGA PROFESA AMKAZIA

Yanga ilimsainisha Lusajo akisoma Chuo cha Ushirika Moshi, lakini mmoja wa maprofesa wa chuo hicho ambaye hamtaji alikuwa shabiki wa Simba, hivyo wakati aliotakiwa ajiunge na timu alimtaka kusalia chuoni kwa miezi mitatu.

Anasema aliiomba Yanga ruhusa ya wiki mbili kwa ajili ya kufanya utafiti (research) na baada ya kumpelekea matokeo profesa huyo ayakague, akakataa na kumtaka afanye mwingine uliofanya abaki peke yake chuoni.

“Yanga ilikuwa inajiandaa na msimu mpya wa 2012/13 niliwaomba ruhusa viongozi wanipe wiki mbili za kufanya utafiti  (reseach), ila mambo yakaenda sivyo licha ya kocha kuzikubali wiki mbili za mwanzo, maana alikuwa anaelewa mambo ya elimu. Mwisho wa siku nikajikuta namkwaza,” anasema Lusajo.

“Kabla ya kusaini Yanga timu ya kwanza kunihitaji ilikuwa  ni JKT Oljoro ya Arusha ambayo iliniahidi kazi baada ya mambo kushindikana nikasaini kwa Wanajangwani, Simba nayo ilihitaji saini yangu, ila niliangalia maslahi, jambo ambalo lilimkwaza profesa, akaamua kunikalisha chuo kama kunikomoa.

“Nikajiunga na Yanga wakati wenzangu walishaanza kucheza Ligi Kuu Bara kwa muda mrefu, hicho kitu sijawahi kukisahau  na huyo profesa yupo hadi leo kwenye chuo hicho na nikienda tunawasiliana vizuri tu, maisha yalishaendelea.”

Lusajo mwenye shahada ya ugavi na manunuzi anasisitiza, umuhimu wa elimu kwa mchezaji au mtu anayepata nafasi ya kusoma akiamini inarahisisha vitu vingi.

“Elimu inatafsiri mambo mengi sana, ndio maana kunaweza kukawekwa kitu hapo kila mtu atakiongelea kwa maana yake, kwa namna anavyojaliwa kufikiria na dunia ya sasa inakwenda kasi inahitaji kuvielewa vitu kwa kina, vinginevyo kuna ugumu unaweza ukawa unakutana nao katika kutatua mambo,” anasema.

Anaongeza kuwa elimu inamsaidia katika taaluma yake. “Mfano kwenye kutafsiri mikataba yangu ya kazi, kujua thamani yangu, hivyo hadi nakwenda kwenye timu nakuwa nimeelewa nilichokisaini kina maana gani kwangu.”

Anapoulizwa kuna kipindi kulikuwa na taarifa za kujiunga na Azam FC, hiyo ilikuaje? Anajibu: “Ni kweli kabisa dili likafa dakika za mwisho, ila siwezi kusema ilikuaje, huko kutakuwa ni kuchimbua vitu ambavyo vimepita.”

VIUNGO NA MABAO

Lusajo anasema anaona viungo ndio wanaoongoza kufunga, jambo linalowapa changamoto ya kupambana washambuliaji, ili kurejesha heshima, ingawa kwa mpira wa kisasa haimshangazi kuona mabadiliko hayo.

“Ni kweli washambuliaji tunatakiwa kupambana kufunga, ila wakati mwingine hao wanaofunga pengine ndio wanaotengenezewa uwanjani kufunga zaidi. Inategemeana wakati mwingine na mifumo ya makocha, pia mashabiki wanapaswa kuelewa mchezaji hawezi kuwa juu wakati wote, kwani ni binadamu kuna wakati atashuka chini na kujipanga,” anasema mchezaji huyo.

“Kuna wakati huwa naona navyosemwa nikifunga mabao 10 kwamba ndio mwisho wangu, basi wanapaswa kuliheshimu hilo. Kuna washambuliaji ambao hawawezi kufikia idadi hiyo na asili ya uchezaji wangu ni kiungo,nilibadilishwa nafasi kwenda ushambuliaji nikiwa Yanga na naendelea kupambana.”

DILI ZIKITIKI  HACHEZI TENA

Lusajo anajipanga kusoma masuala ya utawala katika michezo na kuna chuo anafuatilia ambapo anasema mambo yakikaa sawa muda wake mwingi atautumia huko na siyo soka.

Mwanaspoti lilipomuuliza kauli yake hiyo ni kwamba ana mpango wa kutundika daruga siku za hivi karibuni? Anajibu: “Nina mishe zangu nyingi naziseti zikikaa sawa  nitaachana na soka, hivyo siwezi kusema ni lini, ila kwa sasa ijulikane ni mchezaji wa Mashujaa.”

Kuna jambo analijutia? Lusajo anasema wakati wanapambana ili kuipandisha Dodoma Jiji kabla ya kupanda Ligi Kuu alipewa apige penalti dhidi ya Stand United, lakini alijikuta anapiga mpira bila malengo akasababisha wasipande daraja.

“Nilitoka kufiwa na mtu wangu wa karibu bado moyo ulikuwa na machungu. Penalti ambayo niliipiga ilikuwa ya kuamua kupanda kabla ya kupiga niliwaambia wenzangu siwezi kwa sababu nina msongo wa mawazo, wakanilazimisha, nikapiga ilimradi tumalize nikashangaa timu pinzani wanaingia uwanjani wanashangilia, hiyo inanifanya nijute hadi leo,” anasema.

SOKA BONGO LIKOJE?

Mchezaji huyo anasema kadri muda unavyokwenda soka nchini linaongeza ushindani unaomfanya mchezaji azingatie miiko ili kuhakikisha anafanya vizuri kwani kiwango kikiwa juu ni biashara inayolipa.

“Kuna ushindani wetu wazawa na wageni, hivyo hatuna budi kutunza viwango kwa ajili ya timu ya taifa,” anasema.

Lusajo anawataja baadhi ya  mastaa aliokuwa anawakubali na kuwaona kuwatumia kama kioo chake kuwa ni  Haruna Moshi ‘Boban’, John Bocco, Idd Athuman ‘Chuji’ akisisitiza wakiwa kwenye viwanho vya juu, miguu yao ilikuwa ya dhahabu.

“Mfano Boban ni mnyoofu, moyo wake mkunjufu kama kuna kitu alikosea kwenye soka hataki wadogo zake tupite njia hizo. Amekuwa akinishauri mambo mengi ya kunijenga, jamaa ni tofauti kabisa na picha ambayo jamii inamchukulia,” anasema Lusajo. Mbali na hilo, anasema timu ambayo anaiona ni kama nyumbani ni Namungo FC aliyoitumikia muda mrefu, “niliondoka kwa amani ili kusaka changamoto mpya ya ushindani, ila ni kama timu yangu ya nyumbani.”