Bayern, Madrid ni sare ya piga nikupige

Muktasari:

  • Ilikuwa mechi ya kikubwa kwelikweli, ambapo Real Madrid ikiwa ugenini ilitangulia kwa bao la winga wa Kibrazili, Vinicius Junior.

MUNICH, UJERUMANI: Noma droo. Ndicho unachoweza kusema juu ya mchezo wa mkono wa kwanza wa hatua ya nusu fainali baina ya Bayern Munich na Real Madrid uliopigwa uwanjani Allianz Arena usiku wa Jumanne na mwamba hiyo kufungana mabao 2-2.

Ilikuwa mechi ya kikubwa kwelikweli, ambapo Real Madrid ikiwa ugenini ilitangulia kwa bao la winga wa Kibrazili, Vinicius Junior.

Hata hivyo, wenyeji Bayern hawajataka kuonyesha unyonge na kusawazisha bao hilo kupitia kwa winga wa Kijerumani, Leroy Sane.

Makocha wa timu zote walionyesha ufundi mkubwa, ambapo Thomas Tuchel wa Bayern alitumia mfumo wa 4-2-3-1, wakati Carlo Ancelotti wa Real Madrid alitumia fomesheni ya 4-3-1-2. Mambo yalikuwa moto si mchezo.

Mchezo huo ulishuhudia penalti mbili, moja kwa kila upande, ambapo straika, Harry Kane alitangulia kwa kuifungia bao la pili Bayern kwa mkwaju wa penalti, lakini Los Blancos nao wakasawazisha kwa staili hiyohiyo kupitia Vinicius Junior.

Katika mchezo huo, Bayern ilipiga mashuti 11, matano yakilenga goli, wakati Madrid yenyewe imepiga mashuti manne, yaliyoleng golini yote, huku kikosi cha Tuchel kikimiliki mpira kwa asilimia 54 dhidi ya asilimia 46 za chama la Mtaliano, Ancelotti.

Kwa kuwa ilikuwa mechi ya ufundi, timu zote zilishambuliana kwa kuviziana, ambapo Bayern ilifanya mashambulizi matano ya kushtukiza, wakati Madrid imefanya mashambulizi sita ya aina hiyo.

Bayern ilipiga krosi nane, dhidi ya 11 zilizopigwa na Madrid, huku wenyeji wa kipute hicho cha Allianz Arena, Bayern ilipiga kona sita dhidi ya kona tano za Madrid, huku makipa kwenye mechi hiyo wakilazimika kufanya sevu kadhaa, ambapo Bayern kipa wao alifanya sevu mbili, huku yule wa Madrid alisevu tatu.

Miamba hiyo itarudiana Jumatano ijayo huko Santiago Bernabeu katika kupata mshindi wa kutinga fainali, ambaye atakutana na mshindi wa nusu fainali nyingine baina ya Borussia Dortmund na Paris Saint-Germain, ambapo mechi yao ya kwanza itapigwa Jumatano hii huko Ujerumani.