Mama Bacca: Bacca kanilazimisha kuifuatilia Yanga SC

WIKI iliyopita katika makala ya mahojiano na baba mzazi wa beki wa Yanga, Ibrahim Hamad ‘Bacca’ alizungumza vitu vingi ikiwemo msimamo wake wazi kuwa hapendi mwanawe aende Simba kwa sasa.

Leo tunamalizia na Mwajina Makame, mama mzazi wa beki huyo wa kati wa Yanga na Taifa Stars ambaye ni shabiki kindakindaki wa Simba anayeeleza jinsi anavyolazimika kushabikia mechi za Yanga shingo upande.

Katika mahojiano hayo yaliyofanyika nyumbani kwa kina Bacca eneo la Bubu Skuli, Zanzibar anaweka wazi kwamba ana watoto wa tatu, Bacca akiwa wa kwanza na jinsi biashara ya chipsi ilivyomtoa.

KUMBE MJEDA

Mwajina na mumewe, Abdallah Hamad ambao ni askari wa Magereza, anasema Bacca kiasili ni mtundu na mkimya na wakati wote akiwa mdogo  alikuwa anawaza kucheza soka.

“Sisi wote ni askari Magereza hatukuwa tunakaa sehemu moja wakati wa makuzi ya Bacca, hivyo tulikaa Pemba miaka 12 hapo ndipo tuligundua mwanetu anapenda nini,” anasema.

“Ndani ya muda huo Ibra alimaliza shule darasa la 10 na hakutaka tena kuendelea  jambo ambalo liliniumiza kama mzazi kwani nilitaka awe daktari.”


KARITHI KWA BABA

Mwajina anasema Bacca ameridhi kucheza soka kutoka kwa baba yake ndio maana hakuwa mkali anapokwenda viwanjani.

“Baba yake ameajiriwa kupitia mpira, hivyo anauheshimu sana na mara zote alikuwa anasema tumwache Bacca acheze tu labda huko ndipo ilipo hatima (mafanikio) yake,” anasema.

“Mwisho nikakubaliana naye na kutaka kuona watafika wapi na kama ni kweli ndio kazi waliyoandikiwa basi Mungu amsaidie.”

BAADA YA KUGOMA

Mama huyo anasema mtoto wake aliendelea na soka na kuwa huru baada ya kuachana na masuala ya elimu, ndipo alipoanza kuchezea timu tofauti.

“Alianza kucheza Mapembeani, Taifa ya Jang’ombe, Zanzibar Heroes wakaenda Kenya wakapata nafasi ya pili na kupewa zawadi ya viwanja, wakamtaka Malindi miaka miwili na baada ya hapo KMKM wakamtaka nikagoma,” anasema


KWANINI ALIGOMA

Mwajina anasema, “wakati Bacca anawaza kucheza tu mimi nilikuwa nawaza maisha yake ya baadaye kwani tayari hana elimu ya kutosha.

“Nilikataa asicheze bure tu KMKM kawa hawatampa ajira ili hata kama akiachana na soka basi awe na pa kukimbilia maana mpira ni mchezo wa muda mfupi tu. Hivyo wakamkubalia na kumsaini hapo na mpaka anakwenda Yanga alitokea pale kwenda huko.”


SAFARI YA BARA

Mzazi huyo anasema baada ya Bacca kucheza KMKM siku moja akaamua zake kwenda Bara na rafiki yake kusaini timu nyingine.

“Ibrahim alikwenda kusaini Polisi Tanzania wakati yuko KMKM, jambo lililozua utata mkubwa kwani hakufanikiwa kwa sababu e alikuwa ni askari tayari,” anasema Mwajina.

Hivyo alirudishwa haraka Zanzibar na kupewa masharti ya kuondoka na kuambiwa kama atataka kucheza nje na KMKM, basi anatakiwa aende timu tatu kubwa ambazo ni Simba, Yanga na Azam FC.


ALIVYOENDA YANGA

Mama anaeleza jinsi Mapinduzi ilivyompa shavu Bacca mpaka kufikia hatua ya kusajiliwa Yanga bila hata wao kama wazazi kutegemea.

“Michuano ya Mapunduzi Cup ilipowadia KMKM walikuwa washiriki na walicheza na Yanga ndipo hapo viongozi wake walipoongea na Yanga kuwauliza kama atawafaa,” anasema Mwajina.

“Basi Yanga wakasema anafaa na akasajiliwa huko japo haikuwa pesa nyingi ila sio sawa na huku (zanzibar).”

YANGA PAGUMU

Mwajina anasema katika maisha ya soka ya Bacca yaliyomuumiza ni kipindi cha mwanzoni aliposajiliwa na Yanga.

“Alipofika Yanga mabeki walikuwa Dickson Job na Bakari Mwamnyeto hivyo mwanangu hakuwa anapata nafasi alikaa nje kwa takribani msimu mzima kama sio nusu msimu,” anaeleza mzazi huyo.

“Nilikata tamaa na nikashindwa kumfariji ila yeye alikuwa imara wala hakujali hali anayoipitia na kunitia moyo kuwa wakati bado haujafika.”


MANENO YA WATU

Anaeleza kwamba wakati alipokuwa hachezi Yanga, alikumbuka maneno aliyosikia yakisemwa na watu juu ya mwanawe.

“Niliwahi kusikia mtu anasema mwanangu amesajiliwa kwa pesa ndogo sana, lakini hana kiwango cha kuichezea Yanga na msimu ukiisha tu ataondoka jambo lililoniumiza zaidi na wakati huo hakuwa anapata nafasi.”


GARI LIKAWAKA

Mwajina anakitaja kipindi ambacho mwanawe alianza kuonyesha makali chini ya kocha Nasreddine Nabi.

“Michuano ya Kombe la Shirikisho ilimpa nafasi Bacca kuonekana zaidi na kumfanya kupewa nafasi kubwa zaidi ya hapo awali jambo lililotupa faraja (familia) kwani alikuwa akicheza vizuri sana na kupambania timu,” anasema.


MKATABA WA PILI NOMA

Mama anasema Yanga imembadilisha Bacca katika mambo mengi.

“Sasa amekuwa kimpira na kiakili pia. Bila kusahau mkataba mzito wa raundi ya pili ulivyomuongezea pesa zaidi na mafanikio.”


SIANGALIGI MPIRA

Anasema mara zote Bacca anapokuwa uwanjani huwa hawezi kuangalia mpira kwani anapata hofu kubwa.

“Naogopa mtoto wangu akiumia kuna mechi moja nilimuona ameruka juu na akaumia madkatari wakamuwahi na baadaye akainuka tena.

“Zipo mechi zingine anaumia pia, lakini wananiambia tu ila mimi sitaki kumuona akiumia mbele ya macho yangu napata shida sana nikiona vitu kama hivyo,” anasema.


SIMBA DAMU

Anasema ujana wake alikuwa Simba mpaka alipoolewa hakutaka kabisa kuhamia timu nyingine japokuwa familia nzima ni Yanga.

“Namshabikia Bacca sio Yanga kwa sababu mimi ni Simba na anajua hilo, hata nikimuomba jezi hataki kunipa kwa sababu anajua siwezi kuvaa,” anasema mama huyo.

“Mashabiki wenzangu (Simba huwa) wananiona kama msaliti vile kwa sababu tu nawaombea Yanga washinde kwa sababu ya mwanangu.”


MAFANIKIO BALAA

Mwajina anasema Bacca amekuwa na mafanikio makubwa ikiwemo kuisadia familia yake katika mambo mbalimbali.

“Amejenga mwenyewe ana nyumba zake na mambo mengine ukizingatia pia ni baba bora kwa watoto wake wawili japokuwa wako Pemba,” anasema.


USICHOKIJUA

Mzazi huyo anasema Bacca ana tabia flani hivi tofauti na wachezaji wengi wa soka.  “Mwanangu sio mtu wa starehe kabisa na ni mtulivu, hanywi pombe wala hana mambo mengi hadi chakula chake hataki kiwe na vitu vingi.

“Anapenda kula wali wa nazi na mchuzi wa samaki chukuchuku, juisi ya matunda na kumtembelea bibi yake.”


‘ASIPENDE MABIBI’

Mama Bacca anasema jambo analomshauri kila wakati mwanawe ni kuhusu mahusiano na wanawake.

“Huwa namwambia asipende wanawake ili azidi kuwa vizuri  kwa ajili ya heshima yake binafsi.”


ALIVYOMPATA MKEWE

Kuhusu ndoa, Mwajina anasema Bacca ambaye alioa kwa siri.

“Bacca alimpata mke wake huku Zanzibar kwani wote walikuwa wanafanya kazi KMKM.

Lakini pia tunaishi naye hapa nyumbani wakati Bacca akiwa Dar es Salaam kule kambini.”


SABABU KUUZA CHIPSI

Kama ulikuwa hujui, basi elewa kwamba yule beki kitasa pale Yanga, Bacca aliwahi kukaanga na kuuza chipsi wakati akiwa bado hajatoka kimpira.

“Alikuwa na rafiki yake ambaye alikuwa anauza chipsi, hivyo muda mwingi alikuwa akienda pale kumenya viazi ili apate pesa kidogo za kujikimu,” anasema mama huyo.

“Lakini hakuwa amefungua kibanda cha chipsi kabisa kwamba hiyo ndio biashara aliyokuwa akiifanya, yeye akili yake yote ilikuwa ni mpira tu siku zote hajawahi kubadilika.”


ACHEZE AZAM

Mwajina anasema kuwa mdogo wake Bacca anayefahamika kwa jina la Mudhihir ambaye ndiye wa mwisho kuzaliwa matamanio yake ni kumuona anacheza kama mshambuliaji namba tisa.

“Nataka acheze Azam huyu sitaki aende Simba wala Yanga japo yeye anapenda timu aliyopo kaka yake, ila mimi sikubaliani naye kabisa. Azam kuna pesa ndio maana nataka akacheze ili apate pesa haraka awe tajiri akiwa kijana asiwe kama sisi wazazi wake,” anasema mama huyo.