Faini zatawala Ligi Kuu Bara

Muktasari:

  •  Katika uamuzi uliotolewa timu ya Mashujaa imetozwa faini ya Sh1 milioni kwa kosa la kujihususha na imani za kishirikina.

KAMATI ya Uendeshaji na Usimamizi wa Ligi ya Bodi ya Ligi Kuu Bara (TPLB) katika kikao cha Aprili 30, mwaka huu imepitia matukio yaliyojitokeza katika mechi za Ligi Kuu, Championship na First League na kutoa adhabu mbalimbali kwa timu na wachezaji.

 Katika uamuzi uliotolewa timu ya Mashujaa imetozwa faini ya Sh1 milioni kwa kosa la kujihususha na imani za kishirikina.

Kwa mujiibu wa adhabu hiyo wachezaji na viongozi wa timu hiyo walionekana wakimwaga vitu vyenye asili ya unga kwenye viti na mabenchi ya ufundi na kuweka chupa yenye kimiminika ikiwa na karatasi nyeupe ndani yake wakati wa mchezo wao dhidi ya Azam FC ulioisha kwa suluhu.

Adhabu hiyo ni kwa kuzingatia kanuni ya 47:1 ya Ligi Kuu Bara kuhusu udhibiti wa klabu huku mchezaji wa Azam FC, Abdul Suleiman 'Sopu' akitozwa faini ya Sh500,000 kwa kosa la kuchukua taulo na maji ya kipa wa Mashujaa kisha kuvitupa mbali.

Adhabu hiyo kwa nyota huyo wa Azam, Sopu inazingatia kanuni ya 41:5(5.5) ya Ligi Kuu Bara kuhusu udhibiti wa wachezaji.

Nayo Tanzania Prisons imetozwa faini ya Sh500,000 kwa kosa la kukataa kutumia chumba maalumu cha kuvalia kuelekea mchezo baina ya timu hiyo dhidi ya Geita Gold uliomalizika kwa suluhu.

Viongozi wa timu hiyo walitoa maelekezo kuwa chumba chao kimewekwa vitu vinavyoashiria imani za kishirikina na kina harufu isiyo ya kawaida jambo ambalo lilishindwa kuthibitishwa na maofisa wa mchezo huo waliolifanya ukaguzi baada ya taarifa hiyo.

Hata hivyo, taarifa ya mchezo inaonyesha, Prisons ilikabidhiwa funguo za chumba chao kwa wakati na walifanya usafi wa chumba wenyewe kabla ya kuwasili kwa wachezaji na adhabu hiyo ni kutokana na kanuni ya 17:20 na 17:60 ya Ligi Kuu Bara.

Pia, Prisons imetozwa Sh1 milioni kwa kosa la baadhi ya viongozi wake na benchi la ufundi kujisaidia haja ndogo pembeni ya ukuta uliokuwa jirani na vyumba vya kuvalia nguo badala ya kutumia vyoo  vilivyoandaliwa.

Adhabu hiyo ni kwa kuzingatia kanuni ya 47:1 ya Ligi Kuu Bara kuhusu udhibiti wa klabu.

Naye beki wa Coastal Union, Lameck Lawi amefutiwa kadi nyekundu aliyoonyeshwa wakati wa mchezo dhidi ya Yanga baada ya kuthibitika mwamuzi wa mechi hiyo na mwamuzi msaidizi namba mbili walishindwa kutafsiri vyema sheria za mpira wa miguu.

Tukio hilo lilitokea baada ya Lawi kumvuta jezi nyota wa Yanga, Stephane Aziz Ki jambo ambalo kadi hiyo ilionekana  haikuwa sahihi kwani alipashwa kupewa ya njano kwa sababu hakuwa mchezaji wa mwisho wakati wa pambano hilo.

Uamuzi wa kufuta kadi hiyo unatokana na kuzingatia kanuni ya 12:8 ya Ligi Kuu Bara kuhusu usimamizi wa Ligi Kuu Bara.

Mwamuzi wa mchezo huo, Raphael Ikambi kutoka Morogoro na mwamuzi msaidizi namba mbili wamepewa onyo kali kwa kushindwa kutafsiri sheria,  uamuzi unatokana na kuzingatia kanuni ya 42:1(1.1) kuhusu udhibiti wa waamuzi.

Katika Ligi ya Championship, klabu ya TMA na Pamba zimetozwa faini ya Sh500,000 kila mmoja kwa kosa la kukataa kutumia vyumba maalumu vya kuvalia vilivyoandaliwa kwenye Uwanja wa Black Rhino, Arusha wakati wa mechi hiyo iliyopigwa Aprili 21, mwaka huu.

Adhabu hiyo ni kwa kuzingatia kanuni ya 17:20 na 17:60 ya Ligi ya Championship kuhusu taratibu za mchezo.

Kwenye Ligi Daraja la Pili (First League), klabu ya Moro Kids imepewa ushindi wa mabao matatu na pointi tatu baada ya timu ya Kurugenzi kushindwa kutokea uwanjani kwa ajili ya mchezo huo uliopaswa kufanyika Uwanja wa Jamhuri Morogoro.

Pia Kurugenzi imetozwa faini ya Sh3 milioni na kutakiwa kulipa gharama za maandalizi ya mchezo na kupokwa pointi 15 katika msimamo wa Ligi inayoshiriki huku adhabu hiyo ikitokana na kanuni ya 32:1(1.1,1.2 na 1.3) ya First League kuhusu kutofika uwanjani.