Chama afungiwa michezo mitatu, Simba, Yanga zapigwa faini

Muktasari:

  • Taarifa iliyotolewa na Bodi ya Ligi (TPLB) ilieleza adhabu hiyo ni kutokana na kuzingatia kanuni ya 41:5(5.2) ya Ligi Kuu Bara kuhusu udhibiti wa wachezaji.

KIUNGO wa Simba, Clatous Chama amefungiwa michezo mitatu na kutozwa faini ya Sh1 milioni kwa kosa la kumkanyaga kwa makusudi beki wa Yanga, Nickson Kibabage katika mchezo wa Ligi Kuu Bara baina ya timu hizo uliopigwa Aprili 20 mwaka huu.

Taarifa iliyotolewa na Bodi ya Ligi (TPLB) ilieleza adhabu hiyo ni kutokana na kuzingatia kanuni ya 41:5(5.2) ya Ligi Kuu Bara kuhusu udhibiti wa wachezaji.

Katika mchezo huo, Simba ilifungwa mabao 2-1 ikiwa ni kichapo cha pili baada ya mechi yao ya kwanza iliyopigwa Novemba 5, mwaka jana kupoteza pia kwa mabao 5-1 na kufukuzwa aliyekuwa kocha mkuu wa timu hiyo, Roberto Oliveira 'Robertinho'

Hiyo sio mara ya kwanza kwa nyota huyo kufungiwa kwani Mei 21, mwaka jana alifungiwa pia kutocheza michezo mitatu na kutozwa faini ya Sh 500,000 baada ya kumkanyaga kwa makusudi aliyekuwa nyota wa Ruvu Shooting, Abalkassim Suleiman.

Katika hatua nyingine klabu ya Simba imetozwa faini ya Sh1 milioni huku Yanga ikitozwa Sh5 milioni kwa kosa la kuingia kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa kupitia milango isiyokuwa rasmi wakati wa mchezo wa Ligi Kuu Bara baina ya timu hizo.

Yanga imekumbana na adhabu hiyo kutokana na kufanya makosa yanayojirudia kwani ni mara ya nne ndani ya misimu mitatu baada ya msimu wa 2021/2022, 2022/2023 na 2023/2024 huku ikitokana na kanuni ya 17:21 na 17:60 ya Ligi Kuu Bara kuhusu taratibu za michezo.

Baada ya timu hizo kufika ndani, klabu ya Yanga haikuingia kwenye chumba maalumu cha kuvalia badala yake ilitumia eneo la wazi kwa ajili ya maandalizi yao kwa maelekezo kuwa chumba hicho kilikuwa na harufu isiyokuwa ya kawaida.

Kwa upande wa Simba ilitumia chumba maalumu cha kuvalia kabla ya kuanza mchezo lakini hawakurejea kutumia chumba hicho wakati wa mapumziko.

Kamati ya uendeshaji na usimamizi wa ligi inasubiri taarifa ya daktari wa mchezo huo ambaye alichukua sampuli ya hewa kutoka vyumba vyote viwili kwa ajili ya kuzifanyia uchunguzi.