Yanga ya Makambo hadi Masau anaijua

ACHANA na lile tukio lililowachanganya watu pale Taifa, baada ya Msemaji wa Maafande wa Ruvu Shooting, Masau Bwire kutoa bastola yake kwa mashabiki wa Yanga waliomzonga kutokana na tambo zake kabla ya mchezo.

Bila shaka, Bwire atakuwa ameufyata kutokana na bao la usiku la Heritier Makambo lililoipa Yanga pointi tatu muhimu katika ushindi wa mabao 3-2 pale Taifa. Hadi dakika 90 zinatimia kuacha zile za nyongeza za mwamuzi zinazotokana na mpira kusimama mara kwa mara, Ruvu walikuwa wakiamini tayari wameibana Yanga na kujisahau kabisa wakidhani mpira umekwisha na kuondoka na pointi moja.

Hata hivyo, jeuri hiyo ilikuwa kuzimwa na Makambo baada ya kuwapiga bao lililowashtua na kuwamaliza nguvu kabla ya mwamuzi kupuliza kipyenga cha mwisho na Yanga kuvuna pointi tatu.

Ushindi huo unaifanya Yanga kuendeleza rekodi ya kucheza mechi mfululizo bila ya kupoteza ikiwa ni mchezo wa 16 sasa msimu huu sawa na Azam FC.

Yanga wenyewe wako kileleni na pointi zao 44 huku Azam wanaowafuatia nafasi ya pili wakiwa na 40.

TAMBWE KAWA MTAMU

Mrundi Amiss Tambwe sio wa mchezo. Kadir siku zinavyopsonga ndivyo anarudi kwenye makali yake ya ufungaji baada ya kutoka kuwa majeruhi. Kasi ya Makambo iliwafanya mashabiki na wanachama wa Yanga kuanza kuamini kuwa ufalme wa Tambwe Jangwani umefikia mwisho.

Hata hivyo, katika michezo ya hivi karibuni ukiachana na ile aliyokuwa akiingia dakika za mwisho, amekuwa na wastani wa kufunga karibu kila mchezo aliyocheza zaidi ya dakika 30.

Tambwe ana mabao matano aliyoyafunga kwenye michezo mitatu, dhidi ya Singida United (2), Tanzania Prisons (2) na moja juzi pale Taifa dhidi ya Ruvu Shooting ya Masau Bwire.

MAKAMBO NDIO HATARI ZAIDI

Wakati Tambwe anarejea kwa kasi kwenye kiwango chake cha ufungaji, huku kwa Makambo ndio kama anazidi kukimbiza kutokana na kasi yake ya kutupia kambani. Mkongomani huyo ambaye amekuwa kipenzi cha mashabiki wa Yanga, bao lake dhidi ya Ruvu Shooting ‘wazee wa kupapasa’ juzi Jumapili limemfanya afikishe mabao tisa sawa na Said Dilunga wa Ruvu na Eliud Ambokile wa Mbeya City na kuingia kwenye orodha ya mastaa wanaowania kiatu cha dhahabu cha mfungaji bora wa Ligi Kuu.

YANGA KILA MECHI BAO

Chini ya kocha wao, Mwinyi Zahera, Yanga ya sasa utaipenda. Haiachi kitu. Unaweza kusema imedhamiria kufanya kweli msimu huu kutokana na kasi yao licha ya kukabiliwa na ukata kiuchumi.

Katika michezo 16 ya ligi ambayo imecheza hadi sasa imeshinda 14, dhidi ya Stand United kwa mabao 4-3, Coastal Union (1-0), Singida United (2-0), Mbao FC (2-0), Alliance (3-0), KMC (1-0), Lipuli (1-0), Mwadui (2-1), Kagera Sugar (2-1) na JKT Tanzania wakaifunga kwa mabao 3-0.

Nyingine ni dhidi ya Tanzania Prisons kwa mabao 3-1, Biashara United (2-1), Mtibwa Sugar (2-1) na ule wa juzi wa mabao 3-2, michezo ambayo wametoka sare ni ule wa Simba (0-0) na Ndanda ya Mtwara kwa bao 1-1.

KABWILI MECHI SITA BAO SITA

Ramadhani Kabwili ambaye amekuwa akitegemewa na Yanga kwa sasa baada ya kipa namba moja wa timu hiyo, Beno Kakolanya kuwa na mvutano na Zahera, amecheza michezo sita na kuruhusu bao sita. Kabwili ana wastani wa kuruhusu bao moja kila mchezo na mechi pekee ambayo hakuruhusu bao ni dhidi ya JKT Tanzania ambayo Yanga ilishinda kwa mabao 3-0.

Mechi ambazo Kabwili ameidakia Yanga ukiondoa mchezo dhidi ya JKT Tanzania ni dhidi ya Mwadui, Kagera Sugar, Tanzania Prisons, Biashara United na Ruvu Shooting ambao aliruhusu bao mbili.

FEI TOTO AIBUKA

Hakuna namna. Linapotokea suala la kuchagua viungo, jina la Feisal Salum ‘Fei Toto’ halikosekani.

Licha ya kuwa na mfupi wa kujumuika na wenzake kwenye maandalizi ya mchezo dhidi ya Ruvu Shooting, Zahera ilibidi amtumie Fei Toto kwa kumwanzisha kwenye mchezo huo.

Fei Toto alipata matatizo na kusafiri hadi visiwani Zanzibar kwa ajili ya msiba, hivyo hakuwa na muda mwingi wa kufanya mazoezi na wenzake.

Kiungo huyo ambaye ni miongoni mwa wachezaji wa Yanga waliofiti vizuri kwenye mfumo wa Zahera, alikuwa katika kiwango bora na kufunga moja ya mabao mazuri lililoifanya Yanga kuwa mbele kwa 2-1 kabla ya muda mfupi baadaye Said Dilunga kusawazisha kwa Penalti.

Fei Toto alifunga mara ya mwisho kwenye mchezo dhidi ya KMC Uwanja wa Taifa, ikiwa imepita michezo sita tangu afunge bao hilo pekee la usiku lililoipa Yanga pointi tatu.

MATOKEO YA NYUMA

Ushindi wa Ruvu Shooting kwa Yanga msimu uliopita wa 2017/18 ilikuwa ni sare ya 2-2, Mei 25 mwaka huu, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Katika mchezo wa kwanza baina yao msimu huo, Ruvu Shooting ya Pwani, ikiwa nyumbani kwenye Uwanja wa Uhuru Januari 21, mwaka huu, walikutana na kipigo cha bao 1-0.

YANGA YA COMEBACK

Mchezo ni dakika 90. Kufunga bao la kutangulia kwa Yanga kwa sasa ni sawa na kuichokoza. Utaombea mchezo uishe kwani ni lazima warudishe bao na ikiwezekana wakufunge tena. Suala la ‘Comeback’ kwao ni kitu cha kawaida.

Desemba 3, mwaka huu kwenye Uwanja wa Sokoine, Yanga walitanguliwa kwa bao 1-0 na wenjeji wao, Tanzania Prisons, hata hivyo, mbinu za Zahera na mabadiliko yake, hadi dakika 90 za mchezo Prisons akakalishwa kwa mabao 3-1.

Pia Desemba 9, Yanga wakiwa nyumbani, walitanguliwa na Biashara United kwa bao 1-0, lakini walikomboa na kushinda kwa mabao 2-1.

Mbali na Yanga mwishoni mwa wiki iliyoisha pia kulikuwa na michezo mingine na Alliance ilikutana na Biashara, huku Ndanda FC alikuwa mwenyeji wa African Lyon.

Alliance alikuwa ni mwenyeji wa mchezo huo ambao hadi dakika 45 za kwanza hakuna timu iliyoona lango la mwenzake, mara baada ya mapumziko timu zote zilianza kushambuliana kwa zamu hadi dakika 90 zinakamilika Alliance ilishinda mabao 2-0.

Mtwara, Ndanda aliambulia pointi tatu nyumbani baada ya kufanikiwa kupachika bao kwa mkwaju wa penalti katika dakika ya 30 uliofungwa na Vitalis Mayanga.