MTAJUTA: Wanasoka waliopigwa chini utotoni wakionekana vimeo

Saturday April 11 2020
Vimeo pic

LONDON, ENGLAND. KWA taarifa yako tu, Kylian Mbappe aliwahi kufanya majaribio kwenye klabu ya Chelsea ya Ligi Kuu England kabla ya kwenda kujiunga na timu ya vijana ya AS Monaco ya Ufaransa.

Mbappe aliamua kurudi kwao Ufaransa na kwenda kujiunga na Monaco badala ya Chelsea ambayo ilikuwa na nafasi nzuri zaidi ya kuendeleza kipaji chake cha soka.

“Nilikuwa mdogo sana, miaka 10 au 11 hivi. Nilikwenda London na kukaa kule kwa wiki kama mbili hivi. Nilifanya mazoezi Chelsea na tulikuwa na mechi ya kirafiki dhidi ya Charlton,” alisema Mbappe.

“Tulishinda 6-0 au 7-0. Nilicheza mbele, lakini sikufunga bao. Ilikuwa safi na ilikuwa mara yangu ya kwanza kucheza nje ya Ufaransa na hapo niliona nafasi ya kwenda kucheza England ilivyo.”

Lakini, Mbappe hata miaka 20 hajafika, alipata dili la kwenda kujiunga na Paris Saint-Germain kutokea Monaco kwa ada ya Pauni 166 milioni baada ya kuonyesha soka la kiwango cha juu sana sambamba na timu ya taifa ya Ufaransa. Hii ina maana kwamba Chelsea wangembeba Mbappe, angekuwa mchezaji wao na pengine isingekuwa inammezea mate kwa sasa.

Hata hivyo, Mbappe hakuwa mchezaji pekee ambaye alikataliwa na timu fulani alipokuwa mdogo kabla ya kwenda kuwa supastaa mkubwa kwingineko na kumezewa mate.

Advertisement

11. Mario Balotelli

(Barcelona)

Familia ya Balotelli ilimchukua Mario akiwa mdogo na kumpeleka kwenye akademia ya Barcelona, Juni 2006. Lakini, klabu hiyo ya Nou Camp, ambayo akademia yake ni maarufu kwa jina la La Masia, ilipata shaka juu ya nidhamu ya mchezaji huyo na hivyo kuamua kufuta mpango wa kumchukua moja kwa moja licha ya kufunga mabao matano katika mechi zake za majaribio katika akademia hiyo. Kutokana na tabia za Balotelli, Barca iliamua isimchukue mchezaji huyo, ambaye baadaye alikuja kuwa maarufu, akicheza Inter, Milan, Man City na Liverpool.

10. Marcus Rashford

(Man City)

Akiwa na umri wa miaka tisa, Marcus Rashford alikuwa kwenye rada za Manchester City. Klabu hiyo ilikuwa umbali wa kutembelea tu kwa miguu kutoka kwao Rashford, lakini alionekana kuwa mdogo sana na Manchester United wakaamua kumchukua wao. Kipindi hicho, Rashford alikuwa kwenye timu ya Fletcher Moss Rangers na bosi kwenye timu hiyo, Ron Jamieson aliwapa Man City ofa ya kumchukua kinda huyo kabla ya kumkataa na kumfanya fowadi huyo kutimkia zake kwa mahasimu wao, Man United.

9. Diego Costa

(Corinthians)

Straika Diego Costa, alishindwa kujiunga na akademia yoyote ya klabu maarufu huko kwao alipokuwa mdogo kwa sababu alikataliwa. Klabu kibao ikiwamo Corinthians, Palmeiras na Santos, zote zilimkataa straika huyo mzaliwa na Brazil kwa sababu alionekana kwamba hana kipaji cha mpira. Baadaye, Costa alionekana na wakala Jorge Mendes kipindi akiwa na umri wa miaka 15 na baada ya hapo akampeleka kwenye klabu ya Braga. Huo ndio ulikuwa mwanzo wa Costa kutamba kwenye soka la Ulaya, akicheza klabu kubwa kama Atletico Madrid na Chelsea na kuichezea timu ya taifa ya Hispania.

8. Roy Keane

(Brighton)

Akiwa na mzuka wa kufanya majaribio kwenye klabu yoyote kipindi hicho akiwa na umri wa miaka 15, Roy Keane akatua Brighton akiamini hapo atatimiza ndoto zake za kujaribiwa na kupewa nafasi. Lakini, Brighton walifuta nafasi ya kwenda kujaribiwa siku moja kabla ya kwenda kwenye klabu hiyo kwasababu tu alikuwa na umbo dogo. Huyu ni Keane yuleyule aliyekwenda kuwa moyo wa kiungo cha Manchester United na kupata mafanikio makubwa katika miaka ya tisini. Alianza kwa kusajiliwa na Nottingham Forest mwaka 1990 kabla ya kwenda kujiunga na Man United miaka mitatu baadaye.

7. Antoine Griezmann

(Lyon)

Kijana mdogo, Antoine Griezmann alikataliwa na klabu nyingi sana utotoni ikiamo Olympique Lyon, Auxerre, Saint-Etienne na Sochaux. Klabu hizo zote ziligoma kumchukua Griezmann wakati huo kwa sababu ya kimo chake, kwamba alikuwa mfupi. Lakini, baada ya hapo, amekuwa staa mkubwa akicheza kwa mafanikio katika kikosi cha Atletico Madrid na kunaswa na Barcelona kwa pesa nyingi. Sasa akitamba Nou Camp, amekuwa mtu muhimu pia katika timu ya taifa ya Ufaransa, akitwaa nayo Kombe la Dunia.

6. Luke Shaw

(Chelsea)

Akiwa shabiki wa Chelsea tangu utoto wake, beki wa pembeni, Luke Shaw alikwenda kuichezea timu ya watoto ya klabu hiyo huko Guildford, lakini hakupata nafasi ya kunaswa na akademia ya timu hiyo. Badala yake, Shaw aliamua kwenda zake kujiunga na akademia ya klabu ya Southampton kipindi hicho akiwa na umri wa miaka minane na aliichezea timu hiyo hadi hapo aliponaswa na Manchester United, mwaka 2014. Pengine kwa sasa Shaw angekuwa kwenye kikosi cha wababe hao wa Stamford Bridge.

5. Harry Kane

(Arsenal)

Kane alitumikia kwa mwaka mmoja kwenye akademia ya klabu ya Arsenal kabla ya kuachwa kutokana na kuonekana mfupi na hakuwa na kasi. Mwaka 2015, kocha wa Arsene Wenger alisema kwamba anajutia uamuzi wa Arsenal kuachana na mshambuliaji huyo, ambaye amekuwa akifanya mambo makubwa huko kwa mahasimu wao, Tottenham Hotspur. Kane ni moja ya washambuliaji moto zaidi kuwahi kutokea kwenye Ligi Kuu England na sasa anasakwa na klabu kibao ikiwamo Manchester United, Manchester City na Real Madrid.

4. Javier Zanetti

(Independiente)

Akiwa mdogo, Zanetti aliambiwa kwenye kikosi cha watoto cha Independiente kwamba hataweza kupata mafanikio yoyote kwenye mchezo a soka. Lakini, Muargentina huyo ameonyesha kiwango bora kwenye kikosi cha Inter Milan, alikwenda kucheza mechi 868 na kushinda mataji kibao kwenye kikosi hicho na kutajwa kuwa gwiji katika kikosi hicho cha Serie A. Kwa sasa wakitajwa wachezaji mahiri waliopata kutokea kwenye kikosi cha Inter, basi huwezi kuliweka kando jina la Zanetti.

3. Ruud Gullit

(Arsenal)

Wakati alipokuwa na umri wa miaka 19, Gullit alikwenda kufanya majaribio kwenye kikosi cha Arsenal, lakini alikataliwa na kocha Terry Neill kwa sababu hakuwa tayari kulipa Pauni 300,000 kunasa saini yake. Kutokana na jambo hilo, Gullit alishindwa kujiunga na Arsenal na kuichezea timu hiyo kutokana na Neill, ambaye alikuwa kwenye timu hiyo kati ya 1976 na 1983. Mambo yangekuwa tofauti, Gullit angeingia kwenye rekodi ya kuwa mmoja wa wachezaji waliowahi kukipiga kweye kikosi cha Arsenal.

2. Franco Baresi

(Inter Milan)

Kama mambo yangekuwa tofauti, basi gwiji wa AC Milan, angekuwa mchezaji wa mahasimu wa wababe hao huko San Siro, Inter Milan mahali ambako kaka yake alikuwa akicheza. Baresi alisema alitaka kufuata nyayo za kaka yake, alikwenda kufanya majaribio Inter, lakini ikashindikana kumchukua na kupelekwa AC Milan, mahali ambako alikubalika na kuanza kukipiga. Timu nyingi zilipatwa wasiwasi juu ya umbo la mchezaji huyo, kipindi hicho alikuwa na umri wa miaka 14 tu. Baresi alichezea mechi 719 AC Milan na kuchaguliwa Mchezaji Bora wa Karne kwenye timu hiyo.

1. Ronaldo

(Flamengo)

Wakati alipokuwa mdogo, Ronaldo wa Brazil, alikataliwa Flamengo, timu ambayo alikuwa akiipenda na kuishabikia. Badala yake alikwenda kujiunga na Cruzeiro, mahali ambako alifunga mabao 44 katika mechi 47 na kwenda kuwa mmoja wa wachezaji wakubwa kabisa duniani. Baada ya hapo alikwenda kutamba na timu za Inter, Barcelona na Real Madrid na kushinda Kombe la Dunia akiwa na Brazil huku akifunga mabao 15 katika michuano hiyo mikubwa.

Advertisement