MAONI: Wachezaji Twiga Stars, Watanzania wanasubiri kushangilia ushindi wenu

Friday April 5 2019

 

Timu ya Taifa ya Tanzania kwa wanawake, Twiga Stars inashuka kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam leo kwa mchezo wa kwanza dhidi ya wenzao wa DR Congo ikiwa ni mfululizo wa mechi za kuwania kufuzu Michezo ya Olimpiki itakayofanyika Japan 2020.

Mchezo wa leo ni muhimu kwa Twiga Stars kushinda kwa kuwa kila mpenda soka anataka kuona mafanikio yake na kuona Twiga Stars ikisonga mbele kuelekea kwenye Michezo hiyo ya Olimpiki.

Ushindi wa mabao mengi tunaamini utakuwa kichocheo cha kusonga mbele, kwani mechi ya marudiano itakuwa nyepesi ikilindwa na mabao yatakayofungwa leo.

Hata hivyo, pamoja na kwamba Twiga Stars ina nafasi kubwa ya kushinda kwa kuwa DR Congo si timu ya kutisha sana, lakini si timu ya kubeza kwa kuwa na yenyewe inataka nafasi hiyo ya kwenda Japan.

Hadi kuja Tanzania, ni dhahiri DR Congo wamejipanga na kuja na mbinu mbalimbali kutaka kupata matokeo kwenye mchezo, lakini hatudhani kwamba wachezaji wa Twiga Stars watakuwa wanahofu ya kuwavaa, lakini ushindi utapatikana tu, lije jua, ije mvua.

Twiga Stars inaingia uwanjani ikiwa na rekodi za watangulizi wao, kaka zao, Taifa Stars ambayo imefuzu fainali za Afrika, Afcon 2019 zitakazofanyika nchini Misri.

Kufuzu kwa timu hiyo kumekuja wakati mwafaka, sasa Twiga Stars kupoteza mchezo huo hatutarajii.

Kauli mbiu itaendelea kubakia kuwa hata Wacongo hao wajue kuwa Olimpiki ni zamu ya Tanzania safari hii.

Hatutarajii kama Twiga Stars watapoteza kirahisi mchezo huo kwa kuwa wamepata maandalizi ya maana, maandalizi ya kutosha kuhakikisha ushindi unapatikana.

Pamoja na hayo yote, kuna mambo manne tunataka kuwaambia wachezaji wa Twiga Stars kwa mchezo wao wa leo, kwanza; wanatakiwa kucheza kwa tahadhari kubwa kuepuka kadi zisizo za lazima, ambazo zinaweza kuwatoa mchezoni na baadaye kuanza kumlalamikia mwamuzi, kitu ambacho tayari itakuwa wamechelewa.

Pili; Ushindi wa Twiga Stars leo ni muhimu kwa kuwa wachezaji watakuwa wakicheza kwenye uwanja waliouzoea mbele ya mashabiki wao watakaokuwa wakiwapa nguvu ya mchezo huo na hatimaye kuwachakaza Wacongo hao kwa mabao ya kutosha. Leo wanafungwa Wacongo wanawake na kesho wanapigwa kaka zao wa TP Mazembe.

Mashabiki siku zote ni mchezaji wa 12 uwanjani, kwani hamasa, mashamsham na kila aina ya ushabiki utakuwa kichocheo cha ushindi wa Twiga Stars kwa mchezo wa leo.

Tuna imani kutokana na kiingilio kuwa cha kirafiki zaidi, ni dhahiri mashabiki wa kutosha watajitokeza kwenye mchezo wa leo kwa ajili ya kuwapa nguvu tangu filimbi ya kwanza hadi ya mwisho.

Tatu; Twiga Stars itakuwa ikicheza kwenye hali ya hewa waliyoizoea, kwani kama alivyoeleza kocha Edna Lema, kuwa wameiandaa timu kwa mazingira yoyote, lakini tunawaambia kwa kuwatahadharisha kuwa na viatu maalumu endapo itatokeo mvua kunyesha na uwanja kujaa maji.

Hali ya hewa ya Tanzania hasa Dar es Salaam, wachezaji wameizoea vizuri na haitawapa shida kwa mchezo huo.

Nne; Watanzania watakuwa wakisali, wakiomba dua, lakini kikubwa na wachezaji nao wanatakiwa kucheza kwa nguvu, ari na kujitoa kwa hali na mali kwamba hata timu inapofungwa, ionekane kweli imefungwa lakini wachezaji walijituma kwa asilimia hata zaidi ya 100.

Kwa hayo manne, tunaamini yatakuwa yametoa msukumo wa wachezaji wetu kushinda mchezo huo, na sisi tukiwataka mashabiki wa soka, kuangalia namna ya kushangilia bila kuleta madhara kwa upande mwingine ikiwemo kurusha vitu uwanjani.

Mashabiki mara nyingi hugeuka na kuanza kushangilia wageni, hata ikitokea wametangulia kufungwa, tuwape nguvu wachezaji, tuwashangilie kwa kuwa mpira ni dakika 90, tuone tumepoteza kweli.

Tunafahamu muunganiko wa wac hezaji wetu, Asha Rashid ‘Mwalala’, Mwanahamisi Omari ‘Gaucho’ na Fatuma Mustafa pamoja na wengine watatengeneza muunganiko wa kuleta furaha kwa Watanzania.

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda ameshasema kuwa kila timu itakayoingia Uwanja wa Taifa lazima ikae, sasa hakuna kuogopa, hakuna hofu kinachotakiwa ni ushindi.

Ifike hatua sasa Tanzania iwe inaogopwa katika ukanda wa soka kwa kuwa Simba imeonyesha inaweza, Taifa Stars ina tiketi ya Misri mkononi na Serengeti Boys tunataraji na yenyewe itafanya vizuri mechi zake.

Tunawatakia kila la kheri wachezaji, benchi ya ufundi na wote waliokuwemo kwenye timu hiyo na lengo liwe moja kuhakikisha ushindi unapatikana leo.

Wachezaji wa Twiga Stars watambue kuwa hakuna kingine kinachosubiriwa na Watanzania zaidi ya ushindi wa timu yetu ya Twiga Stars. Mungu Ibariki Tanzania. Mungu ibariki Twiga Stars.