Waamuzi wetu bongo wanafeli wapi AFCON

KATIKA kundi la waamuzi wa soka 56 walioteuliwa kuchezesha mechi za Fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON) mwaka huu kule Misri, hakuna jina la mwamuzi kutoka Tanzania.

Inashtua kidogo lakini ndiyo uhalisia uliopo na jambo la kusikitisha zaidi ni kwamba, wakati Tanzania ikikosa mwamuzi kwenye mashindano hayo, majirani zetu karibia wote wamefanikiwa kupeleka marefa AFCON.

Refa mmoja ameteuliwa kutoka Burundi, Kenya inapeleka waamuzi wawili, mmoja atatokea Rwanda, RD Congo wamepata bahati kwa waamuzi wao wawili kuteuliwa huku Zambia nao refa wao mmoja akipata fursa hiyo.

Kwenye orodha ya waamuzi wenye beji za kimataifa za Shirikisho la Mpira wa Miguu Duniani (FIFA) kuna waamuzi 15 kutoka Tanzania lakini inashangaza kuona hatujapata nafasi hata moja ya uteuzi kwenda kuchezesha mashindano hayo makubwa barani Afrika. Tatizo liko wapi?

Kuna Hery Sasii, Jonesia Rukyaa, Nassoro Mfaume, Flerentina Zabron, Frank Komba, Emmanuel Mwandembwa, Kinduli Mgaza, Soud Lila, Mohammed Mkono, Mtwana Dalila, Grace Wamara, Hellen Mduma, Chacha Ferdinand, Janet Balama na Haule Mbaraka, wanashindwaje kuwemo kwenye orodha ya waamuzi wa kuchezesha AFCON?

Kuna siri gani iliyopo nyuma ya pazia ambayo inakwamisha waamuzi wetu hadi wanashindwa kufikia mafanikio waliyopata baba zao kina Omar Abdulkadir na marehemu Hafidh Ally Tahir ambao, walipata nafasi adhimu ya kuchezesha Fainali za Mataifa ya Afrika kwa nyakati tofauti kipindi walichokuwa wanachezesha?

Je, wanaangushwa na suala la lugha rasmi ambazo zinatambulika na kutumika kwenye mechi za mashindano yanayosimamiwa na CAF pamoja na FIFA ambazo ni Kifaransa na Kiingereza tofauti na wenzao wanaopata nafasi hizo?

Au huwa wanapata alama za chini kwenye mechi kadhaa za kimataifa ambazo wanapata fursa ya kuchezesha ziwe zile za ngazi ya klabu Afrika au zinazohusu timu za taifa, ambazo hutolewa na watathmini wa waamuzi ambao huenda kwenye mechi hizo?

Nani anajua, pengine wanaangushwa na muonekano wao ambao labda unawafanya wanaopanga na kuteua majina ya waamuzi wa kuchezesha AFCON wasiwaamini kuwa, wanaweza kumudu kuleta ushawishi ndani ya uwanja dhidi ya wachezaji wa timu mbalimbali?

Maendeleo ya mpira wa miguu kwenye nchi hayawezi kupatikana kwa timu za taifa au klabu zake kushiriki mashindano ya kimataifa huku waamuzi wakishindwa kupata nafasi kama hiyo.

Unapokuwa na waamuzi bora ambao wanapata nafasi ya kuchezesha mashindano makubwa kama AFCON, ni wazi kuwa soka la nchi litaimarika kwani, utapata wachezaji wenye nidhamu na wanaoheshimu misingi na sheria 17 za mpira wa miguu lakini pia itasaidia kuleta ushindani kwenye ligi na kupata timu bora zitakazoiwakilisha vyema nchi kimataifa.

Tusijidanganye kuwa soka letu linapiga hatua wakati huo huo waamuzi wetu wanakosa nafasi ya kujitambulisha na kujiweka kwenye soko la kimataifa huku wakiishia kuchezesha mechi za ligi ya ndani na zile za kawaida za mashindano ya Afrika.

Baada ya kukosa waamuzi wa kushika filimbi kwenye AFCON 2019 itakayofanyika kule Misri, miezi miwili ijayo, ni vyema tukajitazama upya na kutafuta dawa ya tatizo na kutoka na mikakati mipya kwa ajili ya kujitathimini na kuwapa mbinu waamuzi wetu.