Waamuzi nao watazamwe kwa umakini

NILIUTAZAMA vizuri kupitia luninga, mpambano wa Ligi Kuu baina ya Prisons na Yanga kwenye Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya, Jumatatu iliyopita.

Yanga waliibuka na ushindi wa mabao 3-1, shukrani kwa mabao mawili ya Amissi Tambwe na lile la Ibrahim Ajibu huku bao la Prisons likifungwa na Jumanne Elfadhil.

Mchezo ulitawaliwa na matukio mengi ya utovu wa nidhamu ambayo yalipelekea mwamuzi, Meshack Suda kutoka Singida kuwaonyesha kadi nyekundu, Mrisho Ngassa wa Yanga na nahodha wa Prisons, Laurian Mpalile.

Hata hivyo pamoja na kuwaonyesha kadi nyekundu Ngassa na Mpalile, Mwamuzi Suda alionekana kushindwa kulimudu pambano lile hasa kwenye kipindi cha kwanza.

Alishindwa kuchukua hatua kwenye matukio mengi na mbaya zaidi alionekana kushindwa kuhimili presha ya wachezaji wa pande zote mbili.

Kwa jinsi Suda alivyochezesha mchezo ule, ni vigumu kwake kupona rungu la kamati ya waamuzi, labda itokee bahati tu kukwepa rungu.

Kiwango kisichoridhisha cha Suda ni mwendelezo wa rekodi ovyo ya marefa kutoka mikoani kuchemsha kwenye mechi za Ligi Kuu msimu huu.

Kabla yake tayari marefa Haji Mwarukuta, Athuman Lazi, Jimmy Fanuel, Nicholas Makaranga na Jamada Ahmada ambao wote wanatoka nje ya Dar es Salaam walikumbana na rungu la kamati ya waamuzi.

Katika hali ya kushangaza, waamuzi kutoka mikoa tofauti na Dar es Salaam ndio wamekuwa wakisumbuliwa na jinamizi la kuchezesha vibaya na kuadhibiwa huku wale wa hapa jijini wakipeta.

Kuna mambo kadhaa ambayo yanaweza kuwa siri iliyojificha nyuma ya kufanya vibaya kwa marefa kutoka mikoani.

Kuna sababu nyingi pengine ndizo zinazochangia utofauti mkubwa baina ya waamuzi wa soka kutoka Dar es Salaam na wale wa mikoani.

Kwanza inawezekana uwepo wa Makao Makuu ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) unawapa hofu na kuwaongezea umakini marefa wa soka kutoka hapa jijini tofauti na wenzao.

Ufuatiliaji wa marefa Dar es Salaam bila shaka unakuwa wa karibu na wa mara kwa mara kwa sababu asilimia kubwa ya maofisa wa TFF, Bodi ya Ligi Kuu pamoja na wale wa Chama cha Marefa wa soka Tanzania (FRAT) wako hapa.

Ni vigumu kwa refa kutofanya mazoezi ya kujiweka sawa au kushiriki shughuli za hapa na pale kama semina rasmi na zisizo rasmi za waamuzi kwa sababu anafahamu fika atajiweka kwenye wakati mgumu mbele ya mabosi wake.

Inaonekana hakuna ufuatiliaji wa karibu kwa waamuzi wa mikoani hasa katika ufanyaji wa mazoezi jambo ambalo linawafanya washindwe kuwa fiti na kupelekea wachemshe.

Lakini kingine ambacho kinawatofautisha ni ufanyaji wa mazoezi ya mara kwa mara kwa waamuzi wa Dar es Salaam hasa pale kwenye Uwanja wa Karume uliopo yalipo makao makuu ya TFF. Ni katika mazoezi hayo ambayo mara kwa mara wamekuwa wakisimamiwa na refa mkongwe na mzoefu mwenye beji ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Duniani (Fifa), Israel Nkongo amekuwa wakifanya mapitio ya mara kwa mara ya sheria 17 za mpira wa miguu.

Wamekuwa wakiyafanya kwa nadharia na vitendo hivyo inawapa urahisi wao kufahamu na kufanyia kazi mabadiliko ya mara kwa mara yanayotokea kwenye sheria za soka. Inakuwa ni vigumu kwa mwamuzi asiyefanya mazoezi kufahamu mabadiliko yanayotokea kwenye mchezo wa mpira wa miguu na ndio maana marefa wetu wengi kutoka mikoani hujikuta wanaachwa nyuma na kuchemsha kwenye idadi kubwa ya michezo.

Na sheria ambayo imeonekana kuwa tatizo zaidi kwao ni ile ya kuotea ambapo mara kwa mara hutokana na refa kushindwa kuendana na kasi ya mchezo pamoja na unyumbulifu jambo ambalo linatoa ishara ya wazi kuwa mwamuzi husika hasa mshika kibendera kutokuwa fiti.

Wakati mwingine makosa ya waamuzi wetu hayaji kwa bahati mbaya bali ni matokeo ya maandalizi duni ambayo wamekuwa wakifanya kuelekea kwenye michezo husika. Muda umefika kwa wahusika kuchukua hatua za kulitatua tatizo hilo ili lisiendendelee kutokea.