Ugonjwa unaowatesa Martial na Lacazette

Muktasari:

  • Majeraha waliyopata ni katika eneo la kinena kwa kitabibu hujulikana kama groin na yanaweza kuwaweka nje ya mchezo kwa wiki mbili hadi sita.

TIMU ya Taifa ya Ufaransa imepata pigo baada ya wachezaji wake, Anthony Martial na Alexandre Lacazette kupata majeraha hivi karibuni.

Kocha wa Ufaransa, Didier Derchamps amethibitisha wachezaji hao hawatakuwepo leo Ijumaa usiku katika mchezo wa Kundi A wa Ligi ya Mataifa dhidi ya Uholanzi.

Masaa mawili baada ya kutangazwa kuitwa kuchukua nafasi ya Martial aliyejiondoa kikosi cha Ufaransa kutokana majeraha ya kinena, Lacazette naye alijiondoa kutokana na kupata majeraha kama hayo.

Kimekuwa ni kitu cha kushangaza kwani wote wanatoka taifa moja na wamepata majeraha ya aina moja. Wote wanacheza Ligi Kuu ya England na walipata majeraha siku moja na wote hawakuitwa kwenye kikosi cha Ufaransa kilichotwaa Kombe la Dunia mwaka huu.

Martial mshambuliaji wa Manchester United na na Lacazette wa Arsenal Lacazette waliumia Jumapili iliyopita katika mechi za ligi.

Washambuliaji hawa ambao miezi ya karibuni wameking’ara katika Ligi Kuu England na kutoa mchango katika ushindi wamemvutia kocha wa Ufaransa.

Majeraha waliyopata ni katika eneo la kinena kwa kitabibu hujulikana kama groin na yanaweza kuwaweka nje ya mchezo kwa wiki mbili hadi sita.

Majeraha ya Lacazette si makubwa ukilinganisha na Martial, lakini habari njema ni kuwa wote majeraha yao ni ya tishu laini ya misuli ya eneo, hapakua na uvunjikaji au kuteguka mfupa.

Kwanini majeraha

ya kinena?

Majeraha ya kinena hayakwepeki kwa mwanasoka, kutokana na mazingira ya kucheza mchezo huo. Hii ndio misuli ambayo inawezesha kupeleka mguu upande na sawa au kama vile kupiga msamba. Ukitazama ukabaji katika soka utaona unahusisha kutanua miguu kwenda pembeni.

Misuli hii pia ndiyo inayowezesha kugeuka ghafla wakati unapokuwa unakimbia. Tukio kama hilo ni lazima mwanasoka atalifanya ili kucheza, kupiga chenga na kukaba.

Wakati wa kucheza misuli mitano ya kinena itahitajika kukunjuka na kujikunja ili kujongesha mwili katika mitindo tofauti ikiwamo wakati wa kupiga mashuti, kupiga mashuti, kukaba, kukimbia kwa kasi na kuruka.

Wakati wa kucheza kwa ushindani mwili hufanya matendo ya namna hii na kupitiliza kiwango cha ufanyaji kazi kiasi cha kuivuta misuli hii kupita kiwango, hivyo kusababish majeraha kutokea.

Eneo lenyewe

la kinena sasa

Kinena ni sehemu ya makutano baina ya mapaja na kiuno. Eneo la ndani, ni eneo ambalo sehemu ya tumbo linapoishia na ndio eneo miguu inapoanzia. Eneo hili lina misuli mitano inayojulikana kitabibu kama Adductor Muscles ndiyo huijongesha miguu kwenda pembeni na ndani. Katika eneo hili kuna mpaka ambao una mfereji uitwao kitabibu Inguinal Canal, eneo ambalo ngiri (hernia) hutokea kwa wachezaji na watu wa kawaida na pia ni eneo mkabala na inapotokea mitoki.

Kupata vimichubuko vya ndani kwa ndani, kuchanika kwa misuli hii na kujivuta kulikopitiliza ni kusababisha majeraha yanayowapata wanamichezo wengi ikiwamo wanasoka.

Maumivu ya eneo hili yanaweza yakawa ni kujeruhiwa kwa nyuzi ndogo zinazounda bunda la misuli, tishu laini jirani na eneo hilo na nyuzi ngumu za tendoni na ligamenti. Ukiacha wanasoka hata wanamichezo wengine ikiwamo wanariadha, wacheza mpira wa kikapu na waruka vihunzi hupata sana majeraha ya kinena.

Dalili za majeraha ya kinena ni pamoja na maumivu, kuvimba, kuwa pekundu, misuli kukakamaa, kuhisi misuli kuvuta kwa ndani, kuchechemea na kushindwa kuutumia mguu.

Matibabu ya

majeraha ya kinena

Matibabu hutegemeana na uanishaji wa jeraha baada ya uchunguzi. Kuna aina tatu za majeraha ya nyonga kuvutika sana, kuchanika kiasi na kamili.

Baada huduma za awali hufuatiwa na uchunguzi maalumu katika hospitali maalumu za majeraha viungo na mifupa. Tiba ni kupumzishwa kwa wiki mbili hadi sita na hupona yenyewe au kufanyiwa upasuaji kama ni makubwa.

Majeruhi wanaweza kuwekewa kifaa tiba kulinda eneo hilo lisitonesheke au kujijeruhi zaidi. Dawa za maumivu na mazoezi tiba ya viungo hutolewa kusaidia uponaji.

Ni vigumu kwa mchezaji kujikinga na majeraha haya ila anaweza kufanya mambo yanayoweza kupunguza hatari ya majeraha ikiwamo kunyoosha viungo vya mwili na kupasha mwili moto kabla ya kuingia mchezoni.

Hii husaidia kuiandaa misuli, nyuzi laini za misuli, nyuzi ngumu za tendoni na ligamenti kulainika, hivyo kuwa rahisi kukunjuka bila kujijeruhi.

Mojawapo ya zoezi la kunyoosha misuli ya kinena ni kuwekewa mpira mkubwa katikati ya mapaja na kuubana na kuachia. Hii husaidia kunyoosha misuli hiyo na kuiwezesha kuimarika kila siku.

Kwa mwanamichezo ambaye amejeruhiwa kinena aepuke kurudi mapema uwanjani kabla ya muda uliopangiwa na azingatie lishe bora hasa protini.

Kama uponaji utaenda sawa Lacazette anarajiwa kucheza mchezo wa ligi Novemba 25 dhidi ya Bournemouth wakati Martial bado haijatabirika lini anaweza kurudi.

Mbali na mechi ya leo Ijumaa dhidi Uholanzi, pia Ufarasana itawakosa wachezaji hawa katika mchezo wa kirafiki wa Novemba 20 dhidi ya Uruguay.