Uchawi wa Wafaransa kwenye Ligi Kuu England

Thursday February 28 2019

 

KUTOKA Patrick Vieira hadi N’Golo Kante, wanasoka wa Kifaransa wanavyofurahia mafanikio makubwa kwenye Ligi Kuu England.

Ni hivyo, kama Liverpool watabeba ubingwa wa ligi hiyo msimu huu, basi itakuwa timu ya kwanza kufanya hivyo bila ya kuwa na mchezaji wa Kifaransa kwenye kikosi chao katika karne hii.

Kocha wa Liverpool, Jurgen Klopp si kwamba hapendi wachezaji wa Kifaransa. La, kwenye dirisha lililopita alijaribu kufanya usajili wa Nabil Fekir kutoka Lyon, kabla ya staa huyo kwenda kushinda ubingwa wa Kombe la Dunia 2018 akiwa na kikosi cha Ufaransa huko Russia. Dili hilo lilikwama.

Klopp alimkosa mchezaji huyo na hivyo wachezaji wake 22 waliopo kwenye kikosi ambacho anawatumia kwenye ligi msimu huu, saba ni Waingereza, watatu kutoka Brazil, wawili Uholanzi na mchezaji mmoja mmoja kutoka Ubelgiji, Cameroon, Misri, Guinea, Ureno, Senegal, Hispania, Uswisi na Scotland.

Msimu uliopita wakati Manchester City ilipochukua ubingwa kwenye kikosi chao kulikuwa na Wafaransa wawili, beki wa kati, Aymeric Laporte, aliyemnasa kutoka Athletic Bilbao na beki wa kushoto, Benjamin Mendy, waliyemsajili kutoka AS Monaco.

Mabingwa wa kwanza kwenye karne hii, Manchester United, wao walibeba ubingwa kwenye kikosi chao kukiwa na Wafaransa kibao. Timu zao za ubingwa kulikuwa na Wafaransa kama Mikael Silvestre, Eric Cantona na Fabien Barthez. Man United wakati inatamba kwenye ligi na kunyakua ubingwa, mara zote vikosi vyao vilikuwa na Wafaransa. Mfaransa mwingine aliyebeba Ligi Kuu England akiwa na Man United ni Patrice Evra, aliyebeba taji hilo mwaka 2007, 2008, 2009, 2011 na 2013 akiwa na wababe hao wa Old Trafford.

Arsenal ilinufaika sana na wachezaji wa Kifaransa walipokuja kuichezea timu hiyo iliyokuwa ikinolewa na Mfaransa, Arsene Wenger. Timu zao zilizobeba ubingwa mwaka 2002 na 2004, kwenye kikosi chao kulikuwa na wakali kama Thierry Henry, Patrick Vieira na Robert Pires.

Lakini, kulikuwa na Wafaransa wengine kwenye timu hiyo kama Gael Clichy, Pascal Cygan, Jeremie Aliadiere na Sylvain Wiltord.

Hilo limetokea pia Chelsea. Wakati bilionea Roman Abramovich alipoinunua timu hiyo na kumpa ajira kocha Jose Mourinho kushinda ubingwa mwaka 2005 na 2006, Claude Makelele alikuwa Mfaransa wa kwanza kwenye kikosi chao kubeba ubingwa huo, kabla ya kuwapo na Wafaransa wengine kwenye kikosi cha The Blues, William Gallas na Lassana Diarra katika taji lao la pili la ligi.

Mourinho aliondoka, akarudi akaondoka tena. Makocha wengine walipokuja Stamford Bridge nao walibeba taji hilo. Lakini, hakuna hata mmoja aliyeshinda taji bila ya kuwapo na mchezaji wa Ufaransa kwenye timu yao.

Carlo Ancelotti aliponyakua taji hilo akiwa na Chelsea, kwenye kikosi chake kulikuwa na Wafaransa, Florent Malouda na Nicolas Anelka. Mourinho aliporejea Chelsea na kubeba ubingwa mwaka 2015, wachezaji wa Wafaransa walikuwa Kurt Zouma na Loic Remy waliocheza mechi 34 kwa pamoja.

Kisha ikaja zamu ya Antonio Conte, aliyebeba ubingwa mwaka 2017 kwenye kikosi hicho cha Chelsea, ambapo katika timu yake kulikuwa na N’Golo Kante, ambaye mwaka mmoja kabla alikuwa huko Leicester City alikobeba taji hilo chini ya kocha Claudio Ranieri. Hata mara nyingine ambazo Man City ilibeba ubingwa, kikosi chao kilikuwa na Wafaransa kama Samir Nasri na Eliaquim Mangala. Imekuwa utamaduni, timu inayobeba ubingwa wa Ligi Kuu England kwenye kikosi chake lazima kuwa na mchezaji wa kutoka Ufaransa.

Liverpool msimu huu inapambana kuvunja rekodi hiyo, ikipambana kubeba taji lao la kwanza la ligi kwa kipindi cha miaka 29 huku kwenye kikosi chao kukiwa hakuna mchezaji yeyote Mfaransa na wala kocha si wa kutoka Ufaransa ni Mjerumani.