Taifa Stars wala haikuwa kazi rahisi

Muktasari:

  • Safari nzima ya Tanzania kuelekea Cameroon katika Afcon 2019 zilianza Juni 10 ilipokata utepe wa kusaka tiketi hiyo kwa kuikaribisha Lesotho kwenye Uwanja wa Azam Complex, Chamazi jijini Dar es Salaam.

BILA kujali na matokeo ya jana Jumpaili wakati Taifa Stars ilikuwa uwanjani mjini Maseru, Lesotho kusaka tiketi ya kwenda katika Fainali za Afrika (Afcon) 2019, ushindi wa bao 1-0 iliyopata juzi Uganda The Cranes umeisafishia njia Tanzania.

Uganda ikiwa Uwanja wa Namboole, ilipata ushindi huo dhidi ya Cape Verde na kukata tiketi kwa mara ya pili mfululizo kushiriki Afcon, lakini ikiisafishia njia Tanzania kuvunja rekodi iliyowekwa miaka 38 iliyopita iliposhiriki mara ya kwanza michuano hiyo ilipofanyika mwaka 1980 kule Nigeria.

Kwa hakika haikuwa kazi rahisi kwa Tanzania kujiweka pazuri katika kuvunja rekodi yake, kama sio juhudi zakekatika mechi za Kundi L lililo na timu za Lesotho, Cape Verde, Uganda na yenyewe Tanzania.

Safari nzima ya Tanzania kuelekea Cameroon katika Afcon 2019 zilianza Juni 10 ilipokata utepe wa kusaka tiketi hiyo kwa kuikaribisha Lesotho kwenye Uwanja wa Azam Complex, Chamazi jijini Dar es Salaam.

Ikiwa chini na Kocha Mzawa, Salum Mayanga, Stars ilianza safari kwa matokeo ya sare ya bao 1-1 dhidi ya Lesotho mchezo uliochezeshwa na refarii Djamal Aden kutoka Djibouti.

Nahodha Mbwana Samatta aliitanguliza Stars kwa bao la dakika ya 28 kabla ya wageni kuchomoa dakika 10 baadaye kupitia Thapelo Tale, huku nahodha huyo wa Stars akiulalamikia Uwanja wa Azam kuwa mdogo na uliwabeba wageni wao.

AMUNIKE MDOGOMDOGO

Baada ya Mayanga kumaliza mkataba, Stars ilitafutiwa kocha mpya, Mnigeria, Emmanuel Amunike, Stars iliendelea kuambulia sare, lakini kibabe zaidi mbele ya Uganda ilipovaana nayo Septemba 8, mwaka huu.

Pambano hilo lilipigwa Namboole au Uwanja wa Taifa wa Mandela, ukiwa mchezo wa kwanza wa Mnigeria na kupata sare hiyo iliyofufua matumaini kwa Stars kabla ya kukutana na kipigo cha paka mwizi Mjini Praia, Cape Verde.

Stars ikiamini mambo yamenyooka, ilikumbana na kipigo cha mabao 3-0 dhidi ya wenyeji wao na kuwachanganya mashabiki, lakini Amunike aliwatuliza kiaina kwa kuambiwa lazima alipe kisasi nyumbani watakaporudiana na Cape Verde.

Siku nne tu baada ya kipigo hicho kweli Stars iliikaribisha Cape Verde na kuinyuka mabao 2-0 na kufufua matumaini ya kufuzu fainali za Afcon 2019.

MZUKA WA JPM

Ushindi huo ulimfanya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, John Magufuli kuamua kuwaalika vijana hao Ikulu na kuwatia hamasa akitaka waende kumaliza kazi Lesotho na jana Jumapili walikuwa uwanjani kutimiza ahadi hiyo.

Rais Magufuli alikula nao chakula cha mchana ikiwa muda mchache baada ya kuwamwagia Sh 50 milioni za kuwatia nguvu na midadi kuwa, lazima washinde ili kumalize ukame wa miaka 38 tangu nchi ishiriki Afcon 1980.

Licha ya jana kuwa uwanjani ugenini, lakini Stars bado ina mchezo mmoja mkononi dhidi ya Uganda utakaopigwa Machi 22, mwakani ili kuhitimisha mechi za makundi na kutangazwa timu zitakazofuzu fainali hizo za 32 tangu kuasisiwa kwake miaka 61 iliyopita kwani ilianzishwa rasmi mwaka 1957.

WALIOIBEBA STARS

Ukiachana na mafanikio ya timu kwa ujumla, kwenye matokeo ya mechi nne kuacha ile ya jana, Stars imetoka sare mara mbili, imefungwa mara moja na kushinda mara moja, huku mabao matatu yaliyoipa nafasi Stars yakifungwa na nyota wa kimataifa, Mbwana Samatta na Simon Msuva.

Samatta ndiye alifungulia pazia la mabao Stars akipachika bao la kuongoza kwa Stars dakika ya 28 kwenye mchezo dhidi ya Lesotho uliokwisha kwa sare ya bao 1 -1 kwenye Uwanja wa Taifa.

Samatta tena aliifungia Stars bao dakika ya 57 katika ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Cape Verde huku akitoa pasi ya bao kwenye mchezo huo lililofungwa na Msuva dakika ya 29 ingawa pia siku hiyo alikosa penati iliyosababishwa na Msuva baada ya kuchezewa faulo na mabeki wa Cape Verde kwenye eneo la hatari.

MASTAA WA LAGOS

Miaka 38 imepita tangu Stars ilipoonja fainali za mwaka 1980 baada ya sare ya 1-1 pale Ndola, Zambia kwa bao la Peter Tino.

Waliocheza katika mechi hizo zilizoivusha Stars wanasema ilikuwa ni mechi ya presha, sio tu kwa Stars bali Watanzania, baada ya ushindi wa bao 1-0 wa nyumbania, Stars ilihitaji sare Zambia ili ifuzu kucheza fainali hizo.

Mfungaji wa bao lililoipeleka Stars, Nigeria, Peter Tino anakumbuka kwa kusema tangu walipokuwa wanatua Uwanja wa Ndege wa Zambia, wenyeji waliwakebehi wakiwambia safari yao ya Afcon ndiyo itaishia hapo.

“Tulipokelewa na balozi wetu kule, tuliambiwa wachezaji wa Zambia kila mmoja ameahidiwa gari na rais wao endapo wangetufunga na kufuzu.

Kocha Bendera (Joel sasa ni marehemu) alituambia nendeni mkapambane, hata kama hatujapewa motisha wowote na nchi yetu, ila ushindi ndiyo motisha wenu,” anakumbuka.

Naye Mohammed Rishard ‘Adolph’ aliyefunga bao la mchezo wa kwanza jijini Dar es Salaam anakumbuka kwa kusema namna wachezaji wa Zambia (KK Eleven) walivyojaribu kuwatoa mchezoni siku ya mechi, ila mbinu yao ikagonga mwamba.

“Tulikuwa na upendo, umoja na tulihamasishana wachezaji wenyewe kwa wenyewe, pia tuliweza kumshauri kocha akatusikiliza, hata tulipokuwa Zambia, kocha wetu Mpoland alipigwa bumbuwazi wakati Wazambia walipotuvamia hotelini ili kutuvuruga kisaikolojia.

“Kocha alikuwa anatetemeka, lakini wachezaji tulimfuata tukamwambia, wala vitisho vya Wazambia visimkatishe, hao sisi hawatufungi,” anasimulia Adolph.

Anasema KK Eleven iliandaliwa meza ya chakula kwenye hoteli ambayo Stars ilifikia, wao Stars walipokuwa vyumbani walisikia kelele na vitisho vya wachezaji hao na Mpolandi akapagawa jambo walilofanikiwa kumtuliza.

“Tulimwambia, hivyo ni vitisho tu vya kutaka kutumaliza kisaikolojia, lakini wafanye wafanyavyo hawatufungi na kweli tuliwanyamazisha mbele ya rais wao.

Kipa Juma Pondamali anakumbuka namna alivyoupanchi mpira wa kona ambao Zambia iliamini kona ile ingezaa bao la pili ambalo litawavusha kufuzu kucheza Afcon.

“Mashabiki karibu uwanja wote walikuwa wakiishangilia Zambia, Tanzania tulikuwa na mashabiki wachache sana, wakati kona inakwenda kupigwa Rais Kaunda aliwaongoza mashabiki kusimama wakiimba ‘We need another goal’ huku wakipeperusha vitambaa vyeupe hewani.”

Anasema sio mashabiki tu, hata wachezaji walijua hilo ni bao, hivyo karibu wote walipanda kwenda kuongeza mashambulizi langoni mwa Stars.

“Niliupanchi ule mpira, ikapigwa kaunta ikamkuta Tino ambaye aliwazidi kasi mabeki, tukafunga bao la kusawazisha lililowatoa machozi wachezaji Zambia na mechi ikaisha kwa sare ya 1-1 iliyotupa nafasi ya kufuzu wakati ule. Kitendo cha kusawazisha kiliwamaliza kabisa wachezaji wa Zambia na hawakuamini kuona wakitoa sare mchezo huo.