Staili za ushangiliaji za mastaa hawa na maana zao

Muktasari:

  • Gareth Bale  anatambulika kwa Staili yake ya ushangiliaji, anaitumia kama alama ya kutambulisha biashara zake. Winga huyu wa kimataifa wa Wales aliyevunja rekodi ya uhamisho wa dunia mwaka 2013 wakati alipotoka Tottenham kwenda Real Madrid.

KILA siku unapokaa mbele ya runinga yako huwa unashuhudia mastaa mbalimbali wa soka wakirudia staili za aina moja za ushangiliaji pindi wanapofunga mabao. Imekuwa mazoea kwa mashabiki ingawa wengi huwa hawaelewi chanzo cha aina hizo za ushangiliaji. Siri za nyuma ya ushangiliaji wao ni hizi hapa.

Mesut Ozil

Kiungo mchezeshaji wa Ujerumani na Klabu ya Arsenal, Mesut Ozil. Anajulikana kwa staili yake moja tu ya ushangiliaji. Anaviinamisha vidole vyake vitatu chini ambavyo vinatengeneza herufi ya M na kisha mkono mwingine ananyonya kidole gumba. Staili yake hii ni mahususi kwa ajili ya mtoto wa dada yake anayeitwa Mira. Ozil na mtoto huyo ni marafiki wa karibu na mara zote anapofunga anashangilia kwa staili ya kumkumbuka mtoto huyo.

Antoine Griezmann

Ilianza katika michuano ya Euro pale kwao Ufaransa ambapo Griezmann alionekana akishangilia kwa kucheza dansi. Bahati nzuri alifunga mara nyingi na kuibuka kuwa mfungaji bora huku staili yake ikiwa maarufu kila alipofunga. Alipohojiwa kuhusu staili hii ya ushangiliaji, staa huyu wa Atletico Madrid alidai alikuwa ameitoa katika wimbo wa Hotline Bling ambao umeimbwa na mwanamuziki maarufu wa Marekani, Drake. Mpaka leo akiwa na Aletico amekuwa akikumbusha kuhusu jambo hilo.

Gareth Bale

Huyu ameenda mbali zaidi. Staili yake ya ushangiliaji, anaitumia kama alama ya kutambulisha biashara zake. Winga huyu wa kimataifa wa Wales aliyevunja rekodi ya uhamisho wa dunia mwaka 2013 wakati alipotoka Tottenham kwenda Real Madrid. Amezoeleka kwa kushangilia katika staili ya kuviweka vidole vyake katika umbo la moyo ikiwa ni ishara ya penzi. Bale anafanya hivyo kwa ajili ya heshima la penzi lake kwa mke wake, Emma Rhys-Jones ambaye ni mpenzi wake tangu wakiwa watoto.

Mastaa wengine ambao wamewahi kutumia staili hiyo ni pamoja na nyota wa PSG, Angel Di Maria na nyota wa zamani wa Brazil, Alexander Pato ambaye naye alikuwa anatuma ujumbe kwa mpenzi wake, Sthefany Brito.

Luis Suarez

Staa wa kimataifa wa Uruguay ambaye ni mmoja kati ya washambuliaji wenye urafiki mkubwa na nyavu. Pamoja na kusifika kwa vurugu za hapa na pale akiwa na Liverpool kisha Barcelona kwa sasa lakini Suarez ni mtu wa familia hasa.

Kila anapofunga bao staa huyu wa kimataifa wa Uruguay huwa anabusu mkono wake eneo la ndani karibu na kiganja chake. Hii ni kwa ajili ya familia yake akiwa katika eneo hilo ameandika majina ya watoto wake watatu pamoja na mkewe.

Fabio Borini

Nyota wa Italia ambaye soka lilimkataa akiwa na Liverpool baadaye akaenda Sunderland lakini mambo hayakwenda sawa. Borini anakumbukwa kwa staili yake ya kushangilia kwa kuweka upande wa kiganja chake mdomoni. Mwenyewe aliwahi kufafanua staili hiyo inatoka kwao Italia ambapo mtu akiweka kiganja mdomoni ni ishahara ya mtu aliyeweka kisu mdomoni kuashiria kuna kitu anakisaka kwa udi na uvumba.

Bafetimbi Gomis

Staa wa zamani wa Swansea ambaye aliliteka soka la England kwa staili yake ya kushangilia ambayo ilikuwa ya kipekee sana. Mara nyingi anapofunga mabao huwa anakimbilia katika kibendera cha kona na kuanza kutambaa kwa magoti huku akiunguruma. Staili hii inajulikana kama ‘Panther Celebration’, ambayo aliiga kutoka kwa gwiji wa klabu yake ya zamani Ufaransa, Saint-Etienne, Salif Keita ambaye ni mfungaji wao bora wa kihistoria. Panther ni mnyama dubu ambaye huwa anatembea kwa staili ambayo Gomis amekuwa akiitumia.

Daniel Sturridge

Ukiacha uwezo mkubwa wa kufumania nyavu, Daniel Sturridge (27), pia anajua kucheza dansi. Staili yake imekuwa maarufu kuanzia msimu wa msimu wa 2013/14, ambao alitengeneza kombinesheni ya kuvutia ya nyota wa Uruguay, Luis Suarez. Mwenyewe anadai staili hiyo ya kushangilia ilitokana na jinsi ambavyo yeye alikuwa anacheza na binadamu yake siku za utotoni. Kabla ya hapo staa huyo wa zamani wa Chelsea na Manchester City alikuwa anapenda kushangilia kwa kupandisha jezi yake na kuziba sura lakini kitendo hicho kilikuwa kinampatia kadi za njano mara kwa mara akaamua kuachana na staili hiyo.

Lionel Messi

Mchezaji hatari zaidi wa zama hizi lakini staili yake ya kushangilia haina makeke sana. Akimaliza kushangilia na wenzake huwa ananyanyua vidole viwili juu kutoka katika kila mkono na kuangalia mbinguni.

Mwenyewe amefafanua anafanya hivyo kwa ajili ya kumkumbuka bibi yake ambaye ndiye aliyemuingiza zaidi katika kucheza soka lakini akafariki kabla ya Messi kuwa jina kubwa Catalunya.

“Nafanya hivi kwa sababu mabao yangu ni shukrani kwake. Alinipeleka katika soka lakini kwa sasa hajui nimefika mbali kiasi gani. Hata hivyo, nina imani anaendelea kunisaidia mimi na familia yangu,” aliwahi kusema Messi.

Kwa mujibu wa Luca Caioli, mtu aliyeandika kitabu cha maisha ya Messi anadai kocha mmoja nyumbani kwao Messi Rosario aliogopa kumchezesha Messi kwa madai alikuwa ana umbo dogo sana.

Hata hivyo, bibi yake Messi alimwambia kocha huyo “Muweke uwanjani utaona jinsi ambavyo atakavyopiga soka la uhakika,” kocha wake alijibu. “Sawa namuweka lakini kaa karibu na mstari ili akilia umchukue.”

Cristiano Ronaldo

Staili ya Cristiano Ronaldo ya ushangiliaji inawashangaza wengi. Staili hii inaitwa Siii ikiwa ni lugha ya ‘yes’ kwa Kiingereza au ‘ndiyo’ kwa Kiswahili.

Inadaiwa staili hii iligunduliwa na wachezaji wa Madrid wakiwa mazoezini lakini Ronaldo akaigeuza kuwa yake binafsi. Katika staili hii, Ronaldo huwa anazungusha kiganja chake cha mkono na kuruka juu huku akijigeuza hewani.

Imekuwa staili maarufu kwake ingawa bado haijathibitisha kama ni kweli ilianzishwa na wachezaji wote wa Madrid wakiwa mazoezini.