Simba walisahau bao la Bocco Kitwe, mpira umebadilika

NILISHANGAA wachezaji wa Simba na baadhi ya mabosi wao walikuwa wanashangilia matokeo ya Kitwe dhidi ya Nkana Red Devils.

Nadhani ni baada ya bao la penalti la John Bocco. Soka la kisasa limekwenda mbali kiasi kwamba bao la ugenini si mali kitu.

Nkana wanaweza kupata bao Dar es salaam. Kwanza ni kwa sababu ya ubora wao katika safu ya ushambuliaji.

Pili, bao linaweza kuja kwa namba yoyote ile. Linaweza kuja kwa mipango, linaweza kuja kwa makosa ya wachezaji wa timu pinzani, linaweza kuja kwa penalti kama aliyofunga Bocco.

Litazame pambano la Mbabane Swallows dhidi ya Simba Uwanja wa Taifa. Mbabane walipata bao bila ya matarajio ya wengi. Ndivyo inavyokuwa. Lakini hapo hapo Simba walipokwenda Swaziland Mbabane Swallows walishindwa kupata bao katika ardhi ya nyumbani, halafu Simba ikafunga mabao manne tena.

Hili linaweza kuwatokea Simba na linaweza kuitokea timu yoyote katika soka la Afrika kwa sasa kama mpo katika kiwango kimoja. Unaweza kushangaa mpaka mapumziko Uwanja wa Taifa Nkana ikaongoza mabao mawili. Watu wakatazamana sura.

Kinachotakiwa Simba ni kutojali sana kama ina bao la ugenini mkononi. Ni kama ambavyo haipaswi kujali sana hata kama Nkana wakipata bao la kuongoza Uwanja wa Taifa. Mara nyingi wachezaji wetu wananyong’onyea. Mashabiki nao wanaweka ngoma chini wanaanza lawama kuanzia kwa kocha mpaka wachezaji wao.

Soka la bao la ugenini sio dili sana katika soka la kiwango cha juu. Imegundulika kwamba sio kinga kubwa sana kwa sababu timu zote zinafunga ugenini hasa zile zilizoanzia nyumbani. Wanakwenda ugenini na mgeni anajikuta katika wakati mgumu wa kujigawanya kati ya kujihami na kushambulia, hasa kama anacheza na timu ngumu.

Kinachotakiwa kwa Simba ni kufanya kile walichokifanya dhidi ya Mbabane. Kucheza soka la mgandamizo na kuwa timu bora uwanjani. Kusaka mabao mengi na kutocheza na akili sana ya bao la ugenini. Wachezaji wakiamini wana faida ya bao la ugenini wanaweza kujikuta katika wakati mgumu kisaikolojia kama Nkana wakitangulia kupata bao.

Kama wakipata nafasi SImba inabidi wawakandamize Nkana mabao mengi kama walivyofanya Mbabane.

Wakati mwingine katika hali kama hii wachezaji wanakuwa wanaamini wanahitaji bao moja kupita. Ikitokea Nkana ikapata mabao mawili wanapoteza akili zao uwanjani.

Mara nyingi tunafanya makosa kuwasisitizia zaidi eti ‘Mgeni asiruhusu bao’. Hapana, kitu cha muhimu zaidi ni kumkandamiza adui kila unapopata nafasi. Nkana wanaweza kupata bao lakini vipi Simba wakipata mabao manne itawasaidia nini Nkana?

Nawafahamu wachezaji wetu, hasa wale wazawa. Siamini sana kama wanaweza kuwa na umakini kwa muda wote wa mchezo. Nimetazama mechi za kimataifa za Simba, Yanga, Azam, Taifa Stars na nyinginezo. Wachezaji wetu hawawezi kucheza dakika zote tisini bila ya kupoteza umakini.

Kama tunahitaji kuambiana ukweli basi ni wazi timu kutoka Uganda, Zambia na Afrika Magharibi zinaweza kufunga bao katika muda wowote Uwanja wa Taifa. Ndio maana sioni umuhimu sana wa kushangilia sana bao la ugenini Kitwe wakati sisi wenyewe ni mabingwa wa kutoa zawadi kwa mabao ya ugenini kwa wageni.

Kuhusu mengineyo, tunachosahau pia, katika hali ya kawaida Nkana wamewasoma Simba. Ingawa walishinda 2-1 kwao lakini wanaweza kuja Tanzania wakiwa watu tofauti zaidi. Inategemea wana kocha wa aina gani anayejua kusoma mapungufu au nguvu za adui.

Siamini kama Nkana watakuja Dar es salam kwa ajili ya kusaka sare. Watakuja Dar es salaam kwa ajili ya kujaribu kushinda mechi.

Watatazama tena na tena mkanda wao wa mechi yao nyumbani na kuchunguza makosa ya Simba.

Mara nyingi mechi za pili Afrika huwa zinaleta matokeo ya kushangaza. Ni kama yale ya SImba na Mbabane. Kocha wa Simba inaonekana aliwasoma vizuri Mbabane na kupata ushindi mkubwa zaidi akiwa ugenini wakati nyumbani mechi ilishakuwa ya tabu mpaka kipa wa Mbabane alipoteleza. Ndivyo mpira ulivyo.

Nawasihi Simba, bao la Bocco Kitwe sio dili sana. Simba wangeweza kufungwa 2-0 Kitwe na bado wakashinda Dar es salam au kufungwa. Timu nyingi siku hizi zipo makini katika mashambulizi ya kushtukiza (Counter attack) kuliko wakati mwingine wowote ule.

Februari ikiwadia unaweza kutazama mechi nyingi za mtoano za Ligi ya Mabingwa wa Ulaya. Timu nyingine zinapata mabao ugenini. Katikati ya wiki iliyopita nusura Liverpool itolewe katika dakika ya mwisho ya mchezo na Napoli kama sio uhodari binafsi wa kipa Alisson Becker.

Kinachotakiwa kwa Simba ni kujaribu kufunga kadri inavyoweza. Siamini kama pambano la Dar es salaam linaweza kumalizika kwa ushindi wa 1-0 kwa Simba. Ninachohisi kinaweza kutokea ni Simba kushinda 3-1. Sio lazima sana Nkana isipate bao la ugenini. Hii ndio hali halisi.