Simba imefunika, Yanga bado

Muktasari:

  • Dirisha hilo litakuwa wazi hadi Agosti 6. Kabla ya TFF kulifungua rasmi pazia la dirisha hilo, tayari baadhi ya klabu zilikuwa zilishaanza mbio hizo. Ya kwanza kabisa ilikuwa Singida United ambayo imepanda Ligu Kuu. Ilianza na wachezaji wa kigeni, imefanya vurugu Zimbabwe, Rwanda na Uganda.

DIRISHA la usajili kwa Tanzania Bara limefunguliwa jana Alhamisi, klabu za Ligi Kuu, Ligi Daraja la Kwanza na Daraja la Pili, sasa zinaruhusiwa kufanya usajili wa wachezaji kwa kadiri zinavy oona inafaa. Cha muh imu vigezo na mash arti vizing atiwe.

Dirisha hilo litakuwa wazi hadi Agosti 6. Kabla ya TFF kulifungua rasmi pazia la dirisha hilo, tayari baadhi ya klabu zilikuwa zilishaanza mbio hizo. Ya kwanza kabisa ilikuwa Singida United ambayo imepanda Ligu Kuu. Ilianza na wachezaji wa kigeni, imefanya vurugu Zimbabwe, Rwanda na Uganda.

Nyingine ambazo zilionekana kusubiri hadi jana ndio zianze usajili ni kuchelewa, ni Simba, Azam na Yanga. Usajili ulioanza kufanywa na klabu umeonekana kulenga zaidi safu za ushambuliaji, japo nafasi nyingine pia zimezingatiwa.

Yanga bado kasi yao ya usajili haaijarudi, kisa cha yote ni kujiweka kando kwa bilionea Yusuf Manji, aliyekuwa Mwenyekiti na pia mfadhili wao. Ingawa habari za uhakika zinasema kwamba muda wowote atabatilisha uamuzi wake na kurejea Jangwani baada ya kufuatwa na wakubwa wa klabu hiyo.

Simba imefunika

Mabingwa hawa wa Kombe la FA wao wametangaza usajili wa wachezaji wawili Jamal Mwambeleko na Yusuph Mlipili kutoka Kanda ya Ziwa na nyota watatu wa Azam FC ambao ni John Bocco, Aishi Manula na Shomary Kapombe.

Kocha wa makipa wa Mtibwa Sugar na Taifa Stars, Patrick Mwangata anaelezea juu ya usajili wa Manula kwenda Simba akisema: “Manula kwa sasa amekomaa, ana uwezo wa kucheza popote na kukabiliana na presha ya timu kubwa kama Simba.

Naye kocha wa zamani wa Taifa Stars, Professa Mshindo Msolla, anasema usajili wa Simba unakwenda vizuri, ijapokuwa anaamini wanaofanya usajili huo hawazingatii mahitaji ya timu na kwa wakati gani wanapaswa kuwatumia wachezaji wao.

“Kwa mfano wamemsajili John Bocco, ni sawa lakini atawasaidia kwenye mashindano ya ndani si ya kimataifa. Bocco umri wake umeanza kwenda, ana majeraha ya mara kwa mara ambayo yanamshusha kiwango. Kama kweli lengo ni kusajili wachezaji watakaoisaidia Simba kimataifa, basi isingekuwa kwa Bocco,” alisema kocha huyo msomi.

“Usajili wa Manula hapo Simba wamelamba dume, Manula ni mchezaji mzuri, kiwango chake kinapanda siku hadi siku, umri wake ni mdogo hivyo watamtumia kwa muda mrefu. Anaweza kucheza mechi zote za ndani na nje, hiyo inaaminisha kwamba Manula siyo mchezaji wa wasiwasi.

“Kwa hakika Kapombe anakaribia kumalizika kabisa kisoka, ana miaka miwili tu mbele ya kucheza vizuri pamoja na umri wake kuwa mdogo. Inawezekana kabisa miaka miwili aliyosaini Simba ndiyo miaka yake ya mwisho kucheza kiushindani, hilo si chaguo sahihi kwa Simba kwani hawatamtumia kipindi kirefu.”

Azam FC si haba

Kwa upande wa Azam wao wamesajili wachezaji wanne hadi sasa ambao ni Mbaraka Yusuph, Waziri Junior, Benedict Haule na Salmin Hoza. Professa Msolla ametoa neno pia juu ya usajili huo.

“Azam imepoteza miaka 10 sasa, ili irudi kwenye mstari ni lazima ichukuwe miaka minne mingine mbele. Azam haikuwa na malengo ya mafanikio hasa ilipoacha kuwatumia vijana kutoka kwenye kituo chao, ilipoanza kusajili watu wazima. Ilinishangaza kuona Azam ambayo tuliamini kuwa ndiyo tegemeo la soka nchini ikishindwa hata kupeleka timu ya vijana michuano ya kimataifa.

Yanga bado

Juzi Jumatano, Yanga ilifungua pazia lake la usajili kwa kumchukua beki wa Jang’ombe ya Zanzibar, Abdallah Swaibu ‘Ninja’ lakini ilionekana kama ni usajili wa kawaida.

Professa Msolla amewapongeza Yanga kwa kipindi chote ambacho walikuwa wanafanya vizuri mpaka sasa. “Sijajua usajili wa Yanga utakuwaje msimu huu, maana wapo kimya tofauti na watani zao Simba. Ila Yanga wanajua jinsi ya kuwatumia wachezaji vizuri kwani wanakaa nao kwa kipindi kirefu, ndio maana wanafanya vizuri,” anasema Msolla.

“Mfumo huo ndio unaotakiwa katika soka sio kusajili kila dirisha la usajili, sio kuwaacha nyota wanaosaidia timu kwa kiasi kikubwa. Hicho ndicho kitu pekee kilichowabeba kutetea ubingwa wao.”