Sanchez awatesa De Gea na Martial

Monday November 5 2018

 

MANCHESTER, ENGLAND.UWANJANI mambo yameanza kunyooka pale Old Trafford lakini nje ya uwanja mambo si shwari. Manchester United inateswa na kivuli cha staa wao wa kimataifa wa Chile, Alexis Sanchez ambaye mambo yake hayaendi sawa klabuni.

United inapata shida kubwa kuwabakisha mastaa wake wawili muhimu klabuni, mshambuliaji, Anthony Martial na kipa, David De Gea kutokana na mawakala wa mastaa hao kutaka wachezaji wao wapewe mikataba minono kama staa huyo.

Sanchez alipewa mkataba ambao unamfanya alipwe kiasi cha pauni 400,000 kwa wiki wakati United ilipokuwa inamshawishi kwa udi na uvumba kutua klabuni hapo dhidi ya wapinzani wao wa jadi Manchester City ambao pia walikuwa wanamtaka.

Sanchez pia anapokea kiasi cha pauni 75,000 kwa kila mechi ambayo anacheza Manchester United licha ya kiwango chake kudorora tangu alipotua klabuni hapo akitokea Sanchez katika dirisha la Januari kitu ambacho hakikutazamiwa.

Awali United ilionekana wamepata lakini sasa wanaonekana wamepatikana na mchezaji huyo amekuwa mtego mkubwa kwa mastaa wenzake ambao wanaamini wana mchango mkubwa ndani ya timu kuliko yeye na wanatumia nafasi ya hali ilivyo katika mikataba yao kupata pesa zaidi kutumia jina lake.

Na sasa kipa namba moja wa United, David de Gea,27 anaamini kwamba dili la mshahara la pauni 300,000 kwa wiki ambalo United wanataka kumlipa haoni kama linamstahili wakati huu akichukuliwa kama kipa bora zaidi duniani kwa sasa.

Kwa sasa De Gea ambaye pia ni kipa namba moja wa timu ya taifa ya Hispania analipwa mshahara wa pauni 175,000 kwa wiki na amegoma kusaini mkataba mpya klabuni hapo huku United wakipambana kujaribu kumuongezea mkataba mpya.

Tayari kocha wa United, Jose Mourinho amekiri kwamba ana wasiwasi kwamba huenda kipa huyo wa zamani wa Atletico Madrid asisaini mkataba mpya klabuni hao licha ya United kuwa na nafasi ya kumuongezea mkataba wa mwaka mmoja kwa mujibu wa vipengele vya mkataba wake wa sasa.

Wakifanya hivyo De Gea atalazimika kubakia mpaka katika dirisha kubwa la majira ya joto mwaka 2020 lakini watampoteza bure endapo ataendelea kushikilia msimamo wake wa sasa wa kutosaini mkataba mpya.

Matumaini ya United pia kumbakisha staa wao wa Ufaransa, Anthony Martial yanaonekana kuwa shakani baada ya staa huyo kukataa ofa yake ya karibuni huku ikidaiwa kwamba nyota huyo wa zamani wa Monaco anaweza masharti kama yale yale ya De Gea.

Martial kama ilivyo kwa De Gea na yeye mkataba wake unatarajiwa kumalizika katika dirisha kubwa lijalo la majira ya joto na kwa sasa anaingiza kiasi cha pauni 70,000 kwa wiki huku United wakiwa tayari kumuongezea mshahara huo mara mbili zaidi lakini mwenyewe amegoma.

Juventus na PSG wanamtaka staa huyo mwenye umri wa miaka 22 na United wanapambana kumbakisha licha ya kusuguana na kocha wake, Jose Mourinho mwanzoni mwa msimu lakini sasa amekuwa nyota klabuni hapo na amerudisha fomu yake.

Mourinho anaonekana kubadili msimamo wake na sasa anataka staa huyo aliyefunga mabao manne katika mechi tatu zilizopita za Ligi Kuu ya England ikiwemo bao dhidi ya Bournemouth juzi kubakia klabuni hapo.

“Sina kauli kauli katika mazungumzo ya mikataba. Sishiriki katika aina hizi za mikataba. Ni wazi kwamba matumaini yangu ni kuwa watakubaliana. Ni wazi kwamba ningependa abaki. Najua klabu inamtaka abaki. Ni matumaini yangu kwamba atabakia.” Alisema kocha huyo mtata.