SHIKAMKONO: Niliiokoa Simba isishuke daraja, nikaidhiri Yanga

Muktasari:

  • Kila mtu uwanjani hapo alikuwa anamwangalia yeye. Ni watu wachache tu ambao hawamtambui mtu yule na wanabaki na maswali yao.

TUNAENDELEA na mfululizo wa makala haya yaliyofanyika Kisaki, kijijini Gomero mkoani Morogoro kati ya mfadhili wa zamani wa Simba, Jabir Ally Shikamkono na mwandishi wa gazeti hili, MOHAMMED KUYUNGA.

Jana Alhamisi, Shikamkono alisimulia jinsi alivyofilisika kutokana na kihudumia Simba. Msimu wa 1988 Simba ilikuwa katika hali mbaya sana. Klabu hiyo ilitakiwa kushuka kutoka Ligi Daraja la Kwanza (sasa Ligi Kuu Tanzania) kama ingepoteza michezo yake miwili dhidi ya Pamba ya Mwanza na Yanga jijini Dar es Salaam.

“Klabuni kulikuwa na mgogoro mkubwa sana kati ya Katibu Mkuu, Jimmy David Ngonya na wazee wa klabu hiyo anakumbuka Shikamkono.

“Kwa kuwa timu ilikuwa ikitakiwa kupata pointi moja tu ili kunusurika kushuka daraja, tulikubaliana kila upande uchukue mechi moja. Ngonya akachagua mechi dhidi ya Pamba ambayo ilikuwa inachezwa Mwanza na mimi sikuwa na uchaguzi zaidi ya kubaki na mechi ya Yanga,” anasema Shikamkono.

WAPIGWA MWANZA

Katika mechi ya kwanza dhidi ya Pamba kule Mwanza, Simba ilifungwa bao 1-0 na kubakiwa na mchezo mmoja tu dhidi ya Yanga.

“Timu ilichukuliwa na Saad Juma Mzee hadi Dodoma ambako nilituma basi langu na kuirejesha kambini, Kibaha pale Hoteli Njuweni ambako ndiko ilikokuwa kambi yetu.

“Hapo ndipo kazi ilipoanza, ilinibidi kuitisha kikao na wazee wakiongozwa na Sherrif Al Khatasi na kuwakabidhi timu. Niliwaambia nyie ndio wenye timu yenu, mmeshafanya mengi, miye sijui kitu naomba mnisaidie. Wazee walifurahi sana, Al Khatasi akaniambia watanisaidia. Aliambia atakuwa na vijana wadogo wa madrasa nje ya mji. Alinitaka niwapatie chakula na mahitaji muhimu kwa muda uliobakia ili waweze kuomba dua, nikalitimiza ombi hilo.”

Shikamkono anafichua msaada mwingine aliupata kutoka kwa wachezaji wa Pilsner iliyokuwa ikicheza na Tukuyu kule Mbeya.

“Jamhuri Kihwelo, alikuwa mmoja wapo, alinitaka nisiwe na wasiwasi kwani wangeifunga Tukuyu Stars kule Mbeya ili kuinusuru Simba na kweli waliifunga.”

AWAENDESHA WACHEZAJI

Mbali na kufanya kazi za kuifadhili Simba, kusajili na kulipa posho na mishara ya wachezaji, Shikamkono pia alikuwa akiendesha basi la wachezaji wa Simba kwenda mikoani na hata kwenye mechi za timu hiyo Uwanja wa Taifa (sasa Uhuru).

“Niliendesha basi mwenyewe, zaidi nilikuwa na madereva waliofuzu hasa wawili ambao ni wachezaji, Edward Chumila (marehemu) na John Makelele. Nilipochoka mmojawapo kati yao aliendesha basi la wachezaji,” anafafanua Shikamkono.

SIKU YA MECHI YA YANGA

“Siku ile ya mechi ya Jumamosi Julai 23, asubuhi nilihakikisha wachezaji wanafanya mazoezi ya mwisho. Kisha saa nne nikaenda kwenye mkutano wa mechi nikiwa na nahodha wangu.

“Kisha nikapeleka chakula cha wachezaji kule Kibaha. Kumbuka chakula cha siku ya mechi ya Simba na Yanga kilipikwa nyumbani kwangu. Mke wangu na familia yangu ndio waliopika kuogopa hujuma.

“Saa sita mchana chakula kilienda Kibaha ili wachezaji wale mapema. Saa tisa naondoka na wachezaji kuwahi mechi. Siku hii tena niliendesha basi langu binafsi, nilikuwa na mabasi mawili yaliyotumika kuisafirisha timu kila tulipoenda. Tukiwa tunaenda kucheza dhidi ya Yanga, nikiendesha basi la wachezaji. Nikiwa na eskoti ya polisi, tulipofika mahali, ghafla nilishindwa kuona mbele na mwili ukaishiwa nguvu. Nikapaki pembeni. Sikumbuki nani kati ya Chumila au Makelele mmoja kati yao ndiye aliyeendesha basi lile hadi uwanjani.”

KABILA KUMBE SIMBA

Shikamkono anakumbuka timu iliingia Uwanja wa Taifa akiwa amepata nafuu kubwa tu. Lakini uwanjani mashabiki wa Simba walikuwa wachache mno.

“Upande wa Simba ulikuwa mweupe ukilinganisha na ule wa Yanga, niliangaza juu ya jukwaa, nilimuona mtu ambaye huwa hakosi uwanjani pindi Simba inapocheza. Alikuwa na kiti chake katika sehemu maalumu pale uwanjani. Mtu huyu baadaye alikuwa Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Laurent-Désiré Kabila baba yake Rais aliyemaliza muda wake, Joseph kabila.

“Nilifarijika nilipomuona alikuwa akinipa maneno matamu ya kunifariji kila tulipokutana. Alikuwa anaipenda sana Simba ndio maana hata alipokwenda kwao na kuwa Rais aliibadili Timu ya Taifa ya Congo na kuiita Simba.”

KITUKO KINGINE

Katika hali isiyokuwa ya kawaida, Simba ilikuwa na wachezaji 13 tu siku hiyo, wawili wakiwa wa akiba na haikuwa na kipa wa akiba. Wachezaji 11 uwanjani na wawili wa akiba tu.

“Katika dakika 21 Chumila alifunga bao. Watu wachache tulipata matumaini lakini hali ilibadilika katika dakika ya 36 wakati Issa Athumani alipoisawazishia Yanga.

“Mchezo ulikuwa mkali kwelikweli ndipo kilipokuja kipindi cha kilio kwa Yanga na furaha kwetu pale Makelele alipofunga bao la ushindi katika dakika 58 kipindi cha pili,” anakumbuka Shikamkono.

“Nderemo zilitawala kila kona ya uwanja pale mchezo ulipoisha. Wakati tunarudi njiani tulikutana na makundi ya mashabiki ya Simba, gari letu halikuendeshwa tena bali lilisukumwa hadi Msimbazi.

Kutokana na matokeo hayo, Coastal Union ikawa bingwa licha ya kufungwa 2-0 na African Sports kule Tanga.

“Kkuna watu walisema kipa wa Yanga Sahau Kambi amenibeba kwa kuwa mimi ni wa Morogoro mwenzake. Hakuna ukweli hakupewa rushwa wala hakunibeba,” anafafanua.

Kesho Jumamosi Shikamkono atafichua alivyoporwa kimafia na Yanga wachezaji, Edibily Lunyamila na Sanifu Lazaro ‘Tingisha’ waliokuwa watue Simba. Usikose.