RIDHIWANI:Tatizo la Yanga wala sio Manji

Friday November 16 2018

 

By CHARITY JAMES

HAKUNA ubishi, Yusuf Manji, Bilionea wa Yanga na Mwenyekiti aliyetangaza kujiuzulu na kisha kurejea hivi karibuni amewachanganya kabisa Wanayanga.

Kitendo cha kujiweka kando katika uongozi tangu alipojiuzulu Mei 20 mwaka jana kumeiyumbisha Yanga kwa vile ndiye aliyekuwa Mwenyekiti na Mfadhili Mkuu wa Yanga akiisaidia kifedha mwanzo mwisho.

Ndio maana wanachama waliamua kumgomea maamuzi yake. Baraza la Wadhamini nao walimpelekea msimamo wa wanachama. Yanga ilikuwa inamhitaji Manji zaidi kwa sababu kila kitu kilisimama Jangwani. Manji ndiye kila kitu kwa maana halisi.

Hata hivyo kukaa kwake kando na huku Yanga ikiwa haina kiongozi mkuu baada ya aliyekuwa Makamu Mwenyekiti na Kaimu Mwenyekiti, Clement Sanga kujiuzulu, kuliifanya klabu iyumbe zaidi.

Kwa mujibu wa Katiba, Yanga ilipaswa kufanya uchaguzi kuziba nafasi hizo za juu na zile za Kamati za Utendaji ili kukamilisha uongozi, ndio maana Serikali kupitia Baraza la Michezo Taifa (BMT) ikalielekeza Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kuitisha uchaguzi wa Yanga uliopangwa kufanyika Januari 13 mwakani.

Kutangazwa kwa uchaguzi huo hasa kwa nafasi ya Mwenyekiti kuliwachanganya zaidi Yanga waliokuwa na imani kwamba Manji bado ni kiongozi wao na ndio maana walilipuka kwa furaha waliposikia mwenyekiti huyo amekubali kurejea.

Hata hivyo, kurejea kwa Manji kulikotangazwa na Mwenyekiti wa Baraza la Wadhamini, Kapteni George Mkuchika kumewagawa wanachama wa klabu hiyo, baadhi wakiamini nafasi yake ichaguliwe tu, ili apatikane mtu mwingine kwa vile alishawaacha solemba kitambo na kurejea kwake ni kupita mlango wa nyuma.

Mwanaspoti limefanya mahojiano maalumu na Mwanachama na mmoja wa vigogo wa Yanga, Ridhiwani Kikwete ambaye ni Mbunge wa Chalinze na moja ya swali lilihusu juu ya sarakasi zinazoendelea klabuni kwao na yeye kufafanua kwa kina.

Ridhiwani, mmoja wa watoto wa Rais Mstaafu wa Awamu wa Nne, Dk. Jakaya Kikwete anasema hakuna ubishi Manji ni muhimu ndani ya Yanga, lakini kufanya Uchaguzi kwa sasa ni muhimu zaidi ili kuipeleka klabu mbele. Kivipi?

Ebu endelea na kigogo huyo ambaye amefafanua mambo kadhaa ndani ya Yanga na vitu vinavyopaswa kufanya ili kuikwamua klabu hiyo kongwe nchini.

MABADILIKO LAZIMA

Ridhiwani anasema Yanga kwa sasa inayumba kwa sababu mambo mengi yamesimama na kusisitiza dawa ya kutatua ishu hiyo ni kuhakikisha kunakuwa na mabadiliko kama waliyofanya watani wao, Simba waliochaguana hivi karibuni.

Anasema mabadiliko na mfumo madhubuti wa uendeshaji wa klabu ndio unaoweza kuifanya Yanga kuwa imara kiuchumi. Mfumo utakaifanya Yanga kutoyumba kiuchumi hata kama itatokea kiongozi fulani muhimu ataondoka kwenye nafasi yoyote ya uongozi.

“Wengi wanaamini labda kutokuwepo kwa Manji ndio sababu ya Yanga kuyumba, hapana. Tatizo la Yanga sio Manji ni mfumo uliopo klabu na njia ya kuweka mambo sawa ni lazima kufanyika mabadiliko kama ninavyosisitiza, kila kitu kitakuwa sawa awe yupo Manji ama kiongozi mwingine yeyote,” anasema.

MFUMO WA HISA

Ridhiwani anasema ili klabu iweze kufanya vizuri inahitaji kuendeshwa kisasa na si kumtegemea mtu mmoja kama ilivyo sasa jambo ambalo linakwamisha maendeleo.

“Yanga haiwezi kuendesha timu na ikafanya vizuri bila ya kuwa na mfumo bora wa uendeshaji. Na kuna baadhi ya wanachama wanakwamisha maendeleo kwa kupinga mfumo huo wa mabadiko na kung’ang’ania mtu,” anasema na kuongeza;

“Wapo wanachama wanamng’ang’ania kiongozi mmoja ambaye inafika wakati na yeye anaweza kuchoka na kushindwa kuisaidia timu mfano umeonekana baada ya Manji kujiweka pembeni kwa muda wa mwaka mmoja na kujikuta uongozi uliobaki kushindwa kulipa wachezaji na watu wa benchi la ufundi mishahara yao.”

Anasema jambo hilo linapaswa kuepukwa kama Yanga inahitaji kujikwamua na kuendana na kasi ya soka la dunia ya sasa ambalo linaendeshwa kisasa na kulipa vyema kwa vile kwa sasa soka ni biashara na sio kitu cha kupotezea muda tu.

KURUDI KWA MANJI

Kuhusu kurejea kwa Manji klabuni, Ridhiwani anasema ni faraja kwa wanachama na mashabiki wote, lakini hakuondoi maana ya kufanyika kwa uchaguzi kama ulivyotangazwa, kwani amekaa nje ya uongozi muda mrefu.

Anasema kukaa kwake nje ya uongozi kwa muda mrefu kwa mujibu wa katiba yao ya Yanga ni kukosa sifa ya uanachama.

“Manji ni mtu muhimu sana katika klabu ya Yanga kutokana na mambo aliyowahi kuifanyia, lakini uchaguzi kwa sasa ni muhimu zaidi kwani kwa mujibu wa katiba ya Yanga unatakiwa kufanya uchaguzi upya kama anahitaji nafasi hiyo ambayo ipo kwa ajili ya mpito kuelekea katika mabadiliko.”

kuhusu UCHAGUZI

Ridhiwani anasema kwa kuwa TFF na serikali imekomalia uchaguzi, wanayanga lazima wakubali kuufanya kwa nafasi zilizotangazwa ambazo zilikuwa wazi badala ya kupinga wakati klabu inazidi kuyumba.

“Wanayanga lazima wakubali kuwa, uchaguzi ni kwa afya ya klabu yao, nafasi zilizotangazwa zinapaswa kuchaguliwa watu, ili kuvuka kipindi hiki na chini ya

kipindi hicho uharakishwe mchakato wa mabadiliko kwani yapo ndani ya katiba ni utekelezaji wake tu, tofauti na watani zetu,” anasema.

Anasema kama wanachama wataendelea kupingana, wasishangae watani zao wakiwaacha mbali, kwani mfumo walioingia unawafanya watanue wigo wao na kuifanya klabu yao kuendeshwa kisasa, jambo lililopaswa kufanywa na Yanga mapema kwani ndio walioasisi suala ya klabu kugeuzwa kuwa kampuni.

VIPAUMBELE

Ridhiwani anaweka wazi, endapo angepata nafasi ya kuiongoza Yanga hasa kipindi kiki ambacho timu nyingi zimeanza kuingia katika mfumo wa uendeshaji wa hisa basi kwa upande wake kipaumbele chake cha kwanza kingekuwa ni kuubadilisha mfumo walionao sasa na kuingia katika mfumo mpya.

Angefanya hivyo kwa vile anaamini ni mfumo ambao unaweza kuisaidia Yanga kufika mbali kibiashara na kuweza kuwadhibiti wezi wengi wanaonufaika kupitia

klabu hiyo kwa kutokuwa na watu wa kuwabana.

“Mfano tukiwa na mfumo wa uwekezaji tunaweza kuingia katika udhibiti wa baadhi ya nembo ya klabu jinsi inavyotumika vibaya na watu wasio itakia mema klabu kwa kutengeneza jezi na kuziuza huku wakinufaika wao wenyewe.”

VIGOGO HAWAICHANGII YANGA

Yanga ina wanachama wengi wanaojiweza na walishawahi kujitoa sana hapo nyuma, lakini sasa wanaishia kuwaangalia tu watu wanaohangaika na hiyo timu bila ya mafanikio.

“Unajua kuna muda hadi Manji alishawahi kulalamika kuwa natumia fedha nyingi ila hakuna anachoingiza, hii inatokana na timu hiyo kukosa wasimamizi wazuri wa rasilimali za klabu mtu anaingiza hela yake katika usajili, lakini hawezi kuambulia chochote, ndio sababu ya wengi kujiweka pembeni,” anasema.

“Nina uhakika asilimia mia moja kama wanayanga kwa umoja wetu tutakubali kuingia katika muundo mpya kila mwanayanga atatamani kuingiza hisa zake kwa sababu atakuwa anaona fedha yake inatumiwaje na inaingiza vipi faida.”

Anasema kwa aina ya mfumo uliopo sasa unaoruhusu wapiga dili kujinufaisha badala ya wale wanaotoa fedha zao kuikwamua klabu ni ngumu mtu mwenye fedha zake kukubali kuiingiza Yanga, akiamini anatwanga maji katika kinu.

HANA MPANGO KABISA

Mitaani kumekuwa na taarifa nyingi juu ya Ridhiwani, akitajwa kuwa ni mmoja ya waliokuwa wakikitamani kiti cha Manji ili aiongoze Yanga, lakini anapoulizwa kigogo huyo anajibu kwa kujiamini;

“Nina majukumu mengi sina mipango wa kuwania nafasi yoyote katika uchaguzi unaotarajia kufanyika nitabaki kuwa mwanachama wa kawaida kama ilivyo kwa wanachama wengine ambao sio viongozi.”

“Ni mtumishi wa serikali na Mbunge, nategemewa na wananchi wangu wa Chalinze na nina familia, hivyo natakiwa kuiongoza, pia bado nina majukumu mengine ya kuongeza elimu yangu. Kwa sasa nasoma nikitaka kuiongoza Yanga nitakuwa najiongezea mzigo, siwezi na wala sifikirii kufanya hivyo,” anasema.

USAJILI DIRISHA DOGO

Dirisha la dogo la usajili limefunguliwa rasmi jana Alhamisi, Ridhwani anapoulizwa kama Yanga nayo inahitaji kulichangamkia anajibu kwa kusema klabu yao ina kikosi bora, ila ukata ndio unaowaangusha kwa sasa.

Hata hivyo anasema kama Yanga ingepata fedha na iwapo kuna umuhimu wakuongeza wachezaji wenye dirisha dogo, basi wanaotakiwa kuongezwani straika na winga mmoja kwani maeneo hayo ndiyo yanaonekana kupwaya.

“Tuna viungo bora na wazuri lakini wao ni wazuri zaidi kukaa na mipira suala ambalo ndilo linachangia timu kushindwa kutengeneza nafasi nyingi za kufunga na kujikuta ikipata matokeo kwa idadi ndogo ya mabao, hii sio nzuri kwa timu.”

“Tunatakiwa kuwa na wachezaji ambao kila mchezaji anaitendea haki nafasi anayocheza mfano beki anakuwa makini sana na nafasi yake kuhakikisha

anamlinda kipa asishambuliwe, sina maana kwamba akipata nafasi ya kufunga asifanye hivyo hapana, ila kikosi kinahitaji marekebisho kidogo sana,” anasema.

CHAGUENI VICHWA MAKINI

Ridhiwani (39), anatoa wito kwa wanachama wenzake kuelekea uchaguzi utakaofanyika Januari 13 mwaka ujao ambao mchakato wake kwa sasa upo hatua ya kuchukua na kurudisha fomu.

Anasema kuelekea uchaguzi mkuu wa klabu hiyo, wanachama wanatakiwa kuwa na machaguo sahihi ya watu watakao kuwa viongozi ambao watawavusha kwenda kwenye mabadiliko.

Kigogo huyo anasema wanachama wa Yanga wanatakiwa kuwa makini ili wasijiingize kwenye mtego ambao utawafanya washindwe kufikia mabadiliko ambao kimsingi yanaweza kuwakwamua kwenye ukata walionao kwa sasa.

“Vurugu haziwezi kuwasaidia kipindi hiki wanatakiwa kuwa watulivu kwa kuwa kitu kimoja ili wafanye uchaguzi wao mkuu kwa amani.

Lazima tuseme ukweli viongozi watakapewa dhamana na Wanayanga wanatakiwa waupiganie mchakato wa mabadiliko tunayoyataka kwa haraka kwa sababu mambo yamebadika.