Ndo’hivyo: Kumbe kanda za video zinambeba Msuva

Muktasari:

 

  • Mshambuliaji Msuva amekuwa katika kiwango bora tangu alipotua katika klabu ya Diffa Jadida na msimu amefunga mabao sita katika Ligi ya Mabingwa Afrika.

KUMBE ubora wa kiwango cha mshambuliaji wa Kitanzania, Simon Msuva umechangiwa na tabia ya kuomba kwake kanda za video za michezo ambayo amekuwa akicheza kwa lengo la kujitathimini ili afanyie kazi udhaifu wake. Msuva aliyezaliwa Oktoba 2, 1993, amebainisha kuwa kurejea kwake kwa kutizama kanda za kila mchezo unaopita ni moja ya nguzo zake kubwa ambazo amekuwa akizitegemea kwenye uchezaji wake soka ili kuimarisha kiwango chake.

“Napenda kuwa bora kwa hiyo mbali na mazoezi ambayo nimekuwa nikifanya niliwaza kuwa nawezaje kugundua makosa yangu ili niwe nayafanyia kazi taratibu.

“Kocha huwa ananieleza lakini baada ya mechi kwa wenzetu kuna wepesi wa kupata video ya mchezo mzima, kitu ambacho huwa nafanya ni kuoga na kutumia muda wangu kutizama mechi kabla ya kupumzika,” alisema Msuva.

Mshambuliaji huyo wa Difaa El Jadida ya Morocco, alisema kufanya hivyo kulimfanya kuwa mtulivu pindi anapoingia kwenye eneo la hatari la wapinzani. Msuva alisema miongoni mwa tatizo kubwa ambalo lilikuwa likimsumbua kwenye uchezaji wake ni utulivu akiwa kwenye eneo hilo ambalo kama mchezaji anafanyiwa madhabi huwa ni adhabu kubwa ya mkwaju wa penalti.

MSUVA ASHINDWA KUINUSURU DIFAA

Msuva ambaye Wamorocco wanamfananisha na Sadio Mane wa Liverpool, bao lake alilofunga juzi kwenye mchezo wa Ligi Kuu Morocco ‘Batola Pro’ lilishindwa kuifanya walau Difaa kuambulia sare mbele ya Kawkab Marrakech.

Difaa imekumbana na kipigo cha kwanza msimu huu wa 2018/19 kwenye Batola Pro cha mabao 2-1 ugenini kwenye Uwanja wa Marrakech na kujikuta wanang’olewa kwenye kilele cha msimamo wa Ligi hiyo.