Ndio hivyo, vijana ni muhimu timu za taifa

Monday March 12 2018Ramadhani Awam Kabwili

Ramadhani Awam Kabwili 

By THOMAS NG’ITU

ASIKUAMBIE mtu mafanikio yoyote ya timu za taifa hujengwa na maandalizi mazuri ya wachezaji tangu wakiwa vijana wadogo.

Ndio maana si ajabu makocha wa timu za Taifa za Vijana popote pale huwa wana kazi kubwa ya kujenga wachezaji wao ili waisaidie nchi na maisha yao ya baadaye ya soka.

Wamekuwa wakiwatengeneza vijana na baadaye huchukuliwa na baadhi ya klabu baada ya kuonekana, lakini wengine wakienda huko wanakuwa hawapati nafasi ya kutosha.

Mwanaspoti limeziangalia klabu tatu Simba, Yanga na Azam kwa jinsi ambavyo zinawatumia vijana katika timu zao, pia limemulika baadhi ya klabu zilizowasajili vijana wa Serengeti Boys na jinsi zinavyowatumia.

YANGA

Licha ya Yanga kwa sasa kuwa katika harakati za kutetea taji lao la Ligi Kuu, klabu hii imekuwa ikiwapa nafasi vijana wao chipukizi ambao wanakipiga katika klabu hiyo. Hata kama imelazimika kuwapa kwa sababu ya tatizo la majeruhi walio nao kwa nyota wake, lakini angalau msimu huu vijana waliopo Yanga wamenufaika.

Kipa Ramadhan Kabwili mpaka sasa katika mechi nne, amedaka mara mbili, moja dhidi ya St Louis na Township Rollers katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika iliyochezwa Uwanja wa Taifa.

Vile vile, Yohana Mkomola naye anaingia katika orodha hii, baada ya kusajiliwa wengi walihoji juu ya uwezo wake, lakini alivyopewa nafasi amekuwa akionyesha ni mchezaji ambaye alistahili kucheza katika kikosi hicho.

Majeraha ambayo aliyapata katika mchezo dhidi ya Ruvu Shooting, ndiyo yanamfanya ashindwe kucheza, lakini alivyokuwa mzima alikuwa akipata nafasi ya kucheza mara kwa mara.

Yanga pia licha ya nafasi ya kuwapa vijana wote wacheze ni finyu, lakini wamekuwa wakimtumia Said Mussa katika baadhi ya michezo, pia kiungo chipukizi Edward Maka anayevaa jezi namba nane ya Haruna Niyonzima, naye alikuwa akipata nafasi na amefanya vizuri katika michezo ambayo amecheza.

AZAM

Inawezekana ndio ikawa timu yenye vijana wengi kuliko timu yoyote ligi hivi sasa na hii ni kutokana na wachezaji wake nyota waliokuwepo awali kuondoka katika kikosi hicho.

Azam iliondokewa na Shomari Kapombe, John Bocco, Erasto Nyoni na nyota wengine kibao, lakini jamaa bila wasiwasi wao waliongeza spidi katika vijana.

Yahya Zaid hivi sasa anasimama mbele akiwa kama ndio mshambuliaji namba mbili, huku pia wakiwa wamemsajili Mbaraka Yusuph na Wazir Junior.

Wachezaji hawa wote wamekuwa wakipata nafasi kila wanapokuwa wapo sawa, Wazir Junior licha ya kwamba alikuwa akisumbuliwa na majeraha, lakini katika mechi za kirafiki walipokuwa Uganda, aliweza kuifungia timu hiyo mabao takribani manane.

Mbaraka na Zaid wote wameonekana katika Ligi Kuu kwamba wana kitu ambacho wanakitafuta, sawa na Iddy Kipagwile ambaye amekuwa akipewa nafasi na kuonyesha kiwango kikubwa.

SIMBA

Hawa jamaa wao hivi sasa hawana masihara hata kidogo, hawataki kabisa kujaribisha mchezaji katika kikosi chao kutokana na mahitaji yao waliyoyapanga msimu huu.

Simba imeonekana kabisa wanalihitaji kombe la ligi msimu huu, hivyo katika kikosi chao ni ngumu kuona kijana yeyote, kwani hata wale ambao wamepandishwa kutoka katika timu yao ya vijana, wamejikuta wakisugua benchi.

WENGINEO

Klabu ya Njombe Mji, walimchukua kinda kutoka Serengeti Boys, Nickson Kibabage na amekuwa akipata nafasi mara kwa mara tangu aondoke Lewis Harerimana katika kikosi hiko baada ya kudai pesa zake za usajili na mishahara.

Kibabage katika michezo aliyocheza, ameonyesha katika miguu yake ana vitu vya ziada ambavyo mchezaji aliyepitia misingi bora anatakiwa kuwa nayo.

Upande wa Singida United, ilimchukua aliyewahi kuwa nahodha wa Serengeti Boys, Issa Makamba na kuzua mjadala mkubwa kuhusu matibabu yake baada ya kurejeshwa nchini akitokea Gabon kulipokuwa na mashindano hayo.

Issa anayecheza nafasi ya kiungo mshambuliaji amekuwa na wakati mgumu katika kikosi hicho, baada ya Singida nao kuwa katika presha kubwa ya kuhitaji matokeo katika kila mechi.

Mtibwa wao walimpa nafasi kubwa dogo Dickson Job, ambaye ndiye alikuwa akicheza beki wa kati katika kikosi cha Serengeti Boys kilichoshiriki michuano ya vijana nchini Gabon, pia alivyorudi akaingia moja kwa moja katika kikosi cha wakubwa cha Mtibwa Sugar na amekuwa akipata nafasi ya kucheza.

Ndanda wao walimsajili kinda Abdul Suleiman aliyekuwa anavalia jezi namba 9 katika kikosi cha Serengeti, hata hivyo amekuwa katika wakati mgumu baada ya kukosa nafasi ya kucheza mara kwa mara.