Nani atavunja rekodi ya kina kibadeni?

MIAKA 42 imepita tangu Abdallah Kibaden ‘King Mputa’ afunge mabao matatu kwenye mchezo mmoja ‘hat trick katika mechi inayowakutanisha Watani wa Jadi, Simba na Yanga kwenye Ligi Kuu.

Tangu mechi hiyo iliyochezwa mwaka 1977 hadi sasa, hakuna mchezaji yeyote aliyeweza kuifikia rekodi ya Kibaden ingawa wapo baadhi walikaribia kufanya hivyo kama kina Emmanuel Okwi, Hamis Kiiza, Jerry Tegete na Mark Silengo.

Na kadiri miaka inavyozidi kusogea mbele, hakuonekani dalili za kufikiwa kwa rekodi hiyo kutokana na idadi ndogo ya mabao ambayo imekuwa ikifungwa pindi timu hizo mbili kongwe zinapokutana kwenye ligi.

Miaka 22 baada ya hat trick hiyo ya Kibadeni, mwanaume mwingine anayeitwa Mohammed Hussein ‘Mmachinga’ aliweka rekodi nyingine ya kibabe ambayo nayo imeonekana kuwa mwiba kwa wachezaji wa kizazi cha sasa hasa wale wanaocheza nafasi ya ushambuliaji.

Mmachinga akiwa na kikosi cha Yanga, aliibuka Mfungaji Bora wa Ligi Kuu Tanzania Bara mwaka 1999 baada ya kufumania nyavu mara 26, idadi ya mabao ambayo ni kubwa zaidi kuwahi kufungwa ndani ya msimu mmoja wa Ligi Kuu ambayo kabla na baada ya hapo hakuna aliyewahi kuifikia.

Kuanzia 1999 hadi sasa, kundi kubwa la washambuliaji wazawa na wale wa kigeni kutoka mataifa mbalimbali limecheza katika ligi yetu lakini hakuna hata mmoja aliyeweza kufunga idadi sawa au zaidi ya mabao yaliyofungwa na Mmachinga miaka 20 iliyopita.

Mwaka 2006, straika mmoja matata, Abdallah Juma aliyekuwa akichezea Mtibwa Sugar alikaribia kuifikia rekodi ya Mmachinga lakini kwa bahati mbaya akaishia kufunga mabao 25 ambayo hata nayo yamekuwa yakiwapa wakati mgumu washambuliaji wa kisasa kuyafikia.

Kimsingi rekodi za Kibadeni na Mmachinga zimekuwa mfupa mgumu kwa wachezaji wa kisasa kuutafuna na inawezekana zikachukua muda mrefu kuvunjwa.

Kwa nini inakuwa ni vigumu kwa wachezaji wa kisasa kuzifikia au kuvunja rekodi za wanaume hawa wawili waliowahi kutamba kwenye soka la Tanzania kwa muda mrefu?

Ni swali ambalo unaweza kujiuliza na ukashindwa kupata majibu sahihi kutoka kwa wachezaji wetu wa kizazi cha sasa.

Je, ni kwa sababu ya ushindani kutoka kwa mabeki au udhaifu wa washambuliaji wenyewe au kuna changamoto nyingine?

Tofauti na miaka ya nyuma, wachezaji wa kisasa wanapata huduma nzuri na wanalipwa mafungu makubwa ya fedha za ada ya usajili. Mishahara pamoja na posho ingawa pia wamekuwa wakilala mahali pazuri na kupatiwa matibabu ya kisasa.

Ilipaswa watumie fursa hiyo kuwajibu kwa vitendo wakongwe ambao walishastaafu soka miaka ya nyuma kuwa hisia zao za kuwa kiwango cha soka kwenye miaka ya sasa kimeporoka sio sahihi lakini hali imekuwa kinyume chake na badala yake, wanazidi kutengeneza mazingira ya kuonekana wachezaji wa miaka ya sasa wanaachwa mbali na wale wa zamani.

Kina Heritier Makambo, Okwi, Meddie Kagere, Donald Ngoma na John Bocco ambao wanalala katika hoteli za hadhi ya juu kama Serena, Seascape, Nefaland na Verde walipaswa kuwa wameshafikia na kuvunja zamani rekodi ambazo nyota wa zamani wanajivunia nazo hadi sasa.

Ukitazama namna nyota wa soka wanavyoishi kwa raha na starehe katika miaka ya sasa huku wakipata kila wanachotaka, ni wazi wanakosa jibu la kutuambia kwa nini rekodi za Mmachinga na Kibadeni zimekuwa na ugumu kwao.