Mwarabu yupo siriazi anaitaka Man United

Muktasari:

  • Ikiwa dili hilo la kuiuza Man United kwa Bilionea huyo kutoka Saudi Arabia litakamilika, maana yake klabu mbili kubwa za soka jijini Manchester zitakuwa mikononi mwa Matajiri kutoka Uarabuni kwani tayari wapinzani wao Manchester City kwa sasa wapo chini ya umiliki wa  Abu Dhabi United Group ya Bilionea wa Falme za Kiarabu, Sheikh Mansour bin Zayed Al Nahyan.

MANCHESTER, ENGLAND.KUMBE hii ishu ipo siriazi aisee. Ishu ya kuhusu mwana wa mfalme wa Saudi Arabia kutaka kuinunua Klabu ya Manchester United.

Unaambiwa hivi, Prince Mohammad bin Salman sasa ameweka sawa mipango na mikakati yote katika kuhakikisha anapata fursa ya kuwa mmiliki wa klabu yenye hadhi kubwa zaidi ya kibiashara duniani.

Kwenye mpango huo, mwarabu ametenga mkwanja kiasi cha Pauni 4 bilioni ili kuwashawishi wamiliki wa Man United waweze kumuuzia klabu hiyo.

Bilionea huyo tajiri wa mafuta, anatajwa kuwa na utajiri unaofikia Pauni 850 bilioni, amepanga kukutana na wamiliki wa Man United, wanafamilia, Joel na Avram Glazer huko Mashariki ya Kati wiki chache zijazo. Avram Glazer alipanga kwenda mjini Riyadh kwenye kongamano la kimataifa la wafanyabiashara wakubwa. Avram ni mmiliki mwenza wa Man United na ndugu yake, Joel kwa sasa wameamua kukaa nyumanyuma kufanya biashara hiyo kutoakana na mwana huyo wa mfalme kuwa na matatizo yake binafsi ya kidiplomasia kuhusiana na kifo cha mwaandishi wa habari, Jamal Khashoggi. Hata hivyo, Bin Salman jambo hilo haliwezi kumfanya afute mpango wake wa kuwa mmiliki wa klabu hiyo ya Man United yenye maskani yake Old Trafford, licha ya kwamba familia ya Glazers wanatak amalizane na mambo yake binafsi kwanza kabla ya kuketi mezani kuzungumza biashara.

Familia ya Glazer waliinunua Man United 2005, watapata faida ya Pauni 2.2 bilioni kama dili hilo la kumuuzia timu mwarabu litakamilika.