Mourinho: Hivi huyu Dean zile dakika sita kazitoa wapi?

Muktasari:

  • Mara kwa mara Mourinho amekuwa akiingia matatani kutokana na kauli zake ambazo amekuwa akizitoa dhidi ya waamuzi au waandishi wa habari jambo ambalo limekuwa likipelekea kukutana na adhabu za kutozwa faini na kufungiwa wakati mwingine.

LONDON, ENGLAND . KOCHA wa Manchester United, Jose Mourinho amemshambulia kwa maneno mwamuzi, Mike Dean kuhusu utunzani wa muda wake kwenye mechi ya sare ya 2-2 dhidi ya Chelsea Uwanjani Stamford Bridge.

Man United walipokoswa ushindi wao maarufu nyumbani kwa Chelsea baada ya bao la kusawazisha la dakika 97 lililofungwa na Ross Barkley kuwafanya wenyeji wa mechi hiyo ya Ligi Kuu England kupata pointi moja na kushikilia rekodi yao ya kutopoteza mechi hadi sasa.

Mourinho alisema: “Tulikuwa timu bora uwanjani. Kama unasema kabla ya mechi kwamba pointi moja itatosha Stamford Bridge, utaeleweka kwa sababu ni mahali pagumu, lakini kwa mchezo tuliocheza na matokeo haya tuliyopata, ni mabaya sana kwetu na mazuri kwao.

“Tulikuwa mchezoni hasa, tulimiliki kila kitu, tuliwamiliki wakali wao Hazard na Jorginho wote walifichwa. Baada ya kuwa 2-1 tulikuwa na nafasi ya kufunga bao la tatu, ukweli tulikuwa timu bora ndani ya uwanja na tulitulia.

“Lakini, nadhani kila mwamuzi anapaswa kufanya kama Mike Dean kwa kuongeza dakika sita, sijui zile dakika kazitoa wapi, maana muda wote mechi ilikuwa ikichezwa na hakukuwa na suala la kupoteza muda. Tuliwashika kweli kweli Chelsea, kila mchezaji alifanya majukumu yake na hakika nimekoshwa na wachezaji wangu walichokifanya ndani ya uwanja japo matokeo yamekuwa mabaya kwetu.”